28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mwakamo afanya ziara kituo cha afya Mlandizi

Na Gustafu Haule, Pwani

MBUNGE wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amefanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya Mlandizi mkoani Pwani na kubaini changamoto ya upungufu wa vitanda unaosababisha wajawazito kulala zaidi ya wawili kitanda kimoja.

Mwakamo,amefanya ziara hiyo Machi 3,2023 akiwa na baadhi ya viongozi wa CCM wakiwemo madiwani wa vitimaalum Rehema Chuma na Rehema Jongo.

Mbunge huyo ametembelea kituo hicho ikiwa ni sehemu ya kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani Machi 8, mwaka huu.

Akiwa katika kituo hicho Mwakamo amekutana na changamoto ya wajawazito kulala zaidi ya wawili kitanda kimoja ambapo amesema changamoto hiyo lazima itafutiwe ufumbuzi wa haraka.

“Leo nimeamua kufanya ziara ya kushtukiza hapa katika kituo cha afya Mlandizi lakini nilipofika hapa nimekuta changamoto ya wajawazito kulala katika mazingira ya hatari ,hivyo changamoto hii nimeichukua na nitakwenda kuisemea bungeni,” amesema Mwakamo.

Aidha, amesema wakati akijipanga kwenda kulisemea bungeni jambo hilo amemshauri Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini kuona namna ya kukamilisha kwa haraka wodi ya wajawazito inayojengwa katika Hospitali ya wilaya iliyopo katika eneo la Disunyara.

Muuguzi kiongozi wa wodi ya wazazi katika kituo hicho Exaveria Kapulula,amesema kuwa wodi hiyo inauwezo wa kuhudumia wajawazito 77 kwa mwezi lakini kwasasa wanahudumia wajawazito 282 mpaka 300.

Kapulula,amesema hali hiyo inapelekea vitanda vya kujifungulia pamoja na vifaa vingine vya uzazi kuwa vichache na hivyo kuathiri utendaji kazi katika utoaji wa huduma ya uzazi.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Wilford Kondo amesema kwasasa wanaelekeza nguvu katika kukamilisha wodi ya wazazi iliyopo katika Hospitali ya Wilaya, Disunyara,

Kondo amesema kuwa katika hospitali hiyo tayari huduma ya X-RAY na Ultrasound imeshafungwa na kwasasa huduma zinatolewa masaa machache ikiwa kuanzia asubuhi mpaka saa tisa alasiri lakini endapo wodi hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza mrundikano wa wajawazito katika kituo cha afya Mlandizi.

Hatahivyo, Kondo amemuomba mbunge huyo kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto za kiafya zilizopo katika Halmashauri hiyo kwani licha ya ukosefu wa vitanda lakini kuna changamoto ya ukosefu wa magari ya wagonjwa na hata ukosefu wa uzio katika kituo hicho cha afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles