26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwaka 2015 mwisho wa manyanyaso kwa waandishi-Kibanda

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, amesema mwaka 2015 unahitimisha vitendo vya ukatili na manyanyaso kwa waandishi wa habari nchini.
Kauli hiyo ameitoa jana mjini hapa katika Kongamano la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani, ambalo liliwashirikisha wadau wa sekta hiyo.
Kibanda, alisema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya nne, sekta ya habari nchini imeshuhudia kuibuka na kushamiri kwa vitendo vya kikatili kwa vyombo vya habari na waandishi nchini kuliko utawala wowote tangu nchi ililipota uhuru mwaka 1961.
“Katika kipindi cha miaka 10 cha uongozi wa awamu ya nne, tasnia ya habari imeshuhudia vitendo vya ukatili kwa vyombo na waandishi wa habari kuliko utawala wowote. Sekta ya habari imeshuhudia kuuawa kwa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, waandishi kuvamiwa na kumwagiwa tindikali, kung’olewa kucha na jicho na kufungiwa kwa vyombo vya habari,” alisema Kibanda.
Kutokana na matukio hayo Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, aliitaka jumuiya ya kimataifa kutofumbia macho matukio ya aina hiyo na badala yake kuingilia kati ili kukomesha vitendo vya kikatili kwa waandishi wa habari.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA – TAN), Simon Berege, alimshauri Rais Jakaya Kikwete kwa kutosaini miswada ya sheria ya takwimu na uhalifu wa mtandaoni kutokana na miswada hiyo kuwa na vipengele vingi ambavyo vinakwaza uhuru wa habari.
Alisema kuwa hatua ya kwa Rais Kikwete kutosaini miswada hiyo ili irejeshwe bungeni iweze kujadiliwa upya na kushirikisha wadau mbalimbali hususani wahabari ili kuweza kutetea vipengele vinavyoweza kuwatetea katika utendaji.
Berege alisema, hivi sasa Serikali inafanya juhudi za kufifisha uhuru wa habari wakati ambapo taifa limeporomoka katika viwango vya kimataifa vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 69 hadi ya 75.
“Ulimwengu upo katika zama za taarifa na kwamba serikali isijaribu kufifisha au kuzuia kwani itasababisha kupitwa kama ambavyo imepitwa katika zama za mapinduzi ya viwanda,” alisema Berege.
Kwa upande wake Mwakilishi wa taasisi ya Konrad Adenauer (KAS), Stefah Reith alisema sheria hizo zinakandamiza uhuru wa maoni na demokrasia hapa nchini na hivyo kufanya nyanja ya upashaji wa habri kuwa katika kiwango cha chini.
Naye Makamu wa Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Jane Mihanji, alisema maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yanafanyika huku idadi kubwa ya waandishi wa habari wakiwa wanafanyakazi katika mazingira magumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles