Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
MVUA za vuli zinazoendelea kunyesha mikoa mbalimbali nchini, zimeleta athari huku baadhi ya barabara zikifungwa kwa muda kuhofia usalama wa watu na mali zao.
MTANZANIA lilitembelea baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kuona athari za mvua hizo zilizoanza jana saa 11 alfajiri na kushuhudia nyumba zaidi ya 30 katika eneo la Jangwani zilizopo pembezoni mwa Barabara ya Morogoro zikiwa zimezingirwa na maji.
Wakazi wa nyumba hizo wamejikuta wakizikimbia na kuacha mali zao ikiwamo mifugo.
Pia Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walilazimika kuifunga barabara hiyo zaidi ya saa tano kutokana na mvua kupita juu ya barabaara na kusababisha magari kushindwa kupita kirahisi.
Katika eneo hilo, kulikuwa na msururu wa magari na watembea kwa miguu, ambao wengine walilazimika kulipa fedha kwa vijana waliokuwa eneo hilo wavushe.
Akizungumza na MTANZANIA, Said Nassor, alisema ni vyema Serikali ikafanya jitihada za kurekebisha kasoro zilizopo katika eneo la Jangwani ili kuondoa adha waipatayo wananchi mara kwa mara.
Alisema eneo hilo awali lilikuwa na madaraja manne, lakini baada ya barabara hiyo kujengwa upya yamebaki matatu.
“Eneo hili kinachosumbua ni uhaba wa madaraja na ukuta wa kituo cha mabasi yaendayo kasi ndio yamekuwa yakichangia maji kutopita kirahisi na kusababisha mafuriko,” alisema Nassor.
Alisema wanachoshukuru mvua hiyo leo (jana) ilianza alfajiri hivyo watu wameweza kuhamisha baadhi ya mali zao ndani, lakini ingeanza usiku wa manane, ingesababisha vifo na uharibu wa mali nyingi.
Pia mabasi yaendayo kasi (UDART), nayo yalilazimika kusitisha safari kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Mabasi mengine na magari madogo yalilazimika kutumia njia nyingine mbadala ili kuendelea na safari zao kama kawaida.
MTANZANIA lilishuhudia pia daraja la Mongolandege, Kata ya Ukonga wilayani Ilala likiwa limefurika na kusababisha adha kwa wakazi zaidi ya 13,000 ambao walishindwa kwenda kwenye shughuli zao huku wanafunzi wakikwama kwenda shule.
Mkazi wa eneo hilo, Martha John, alisema wamekuwa wakikabiliwa na adha ya ukosefu wa daraja katika eneo hilo zaidi ya miaka 13 jambo ambalo linasababisha vifo vya mara kwa mara pindi mvua zinaponyesha.
“Tunaomba viongozi wetu wa jimbo ifike wakati sasa waone umuhimu wa kutujengea daraja hili kwani limekuwa na madhara, hasa nyakati za mvua na bidhaa nyingi zimepanda kwa sababu ya kutumia pikipiki kwa kila safari,” alisema Martha.
Diwani wa Kata ya Ukonga, Jumaa Mwipopo (Chadema), alisema atatoa taarifa za hatua zilizochukuliwa hadi sasa za ujenzi wa daraja hilo.
Alisema binafsi anakerwa na daraja hilo lililoharibika tangu mwaka 2003 baada ya kusombwa na mvua, lakini hadi leo ujenzi wake umekuwa ukisuasua.
“Nasubiri niongee na mamlaka zinazohusika kuhusu adha hii kwani nimekwishatoa taarifa mara kwa mara na hata juzi tulipita pale na mbunge wetu Mwita Waitara, na alijionea hali halisi ilivyo,” alisema Mwipopo…
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA