32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Muujiza wa mtoto wa mtaani

mtz11-5

Na FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM

KATIKA dunia hii tunayoishi unaweza kujiona kuwa wewe una matatizo makubwa lakini kumbe kuna wenye shida zaidi ambao iwapo ungepata nafasi ya kujua matatizo yao usingethubutu kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Wengi wetu hudhani kuwa hali ya kukosa fedha ni mtihani mkubwa jambo ambalo ni jepesi mno ikilinganishwa na maisha aliyopitia, James Yustar (27).

Licha ya kwamba kwasasa ana akili timamu za kuweza kupambanua mambo ikiwamo kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku, lakini amepitia mitihani mizito ya maisha ikiwamo kutupwa jalalani na kuangukia kwenye midomo ya mbwa na hata kutaka kujaribu kuuza figo yake bila mafanikio.

Yustar ambaye hakuwahi kuwafahamu baba wala mama yake na mahali alipozaliwa, lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kufikiria kujiua bali alijipa moyo na kupambana na changamoto za maisha akiwa chini ya mikono ya wasamaria wema.

Licha ya kuitwa mwizi, mtoto wa mtaani, chokoraa, kunusurika kuliwa na mbwa baada ya kutupwa kama kichanga, kufukuzwa na kupigwa vita kila pamoja na kunyang’anywa mali alizoachiwa na mlezi wake, haikuwa sababu ya Yustar kushindwa kutimiza ndoto yake.

Anasema hadi leo hakuwahi kuwafahamu wazazi wake ambao walimtelekeza na kuangukia mikononi mwa mbwa.

“Sikuwahi kufahamu wapi nilizaliwa, lini na nani aliyenizaa na kunitupa jalalani niliwe na mbwa

“Hii inatokana na historia ambayo nilisimuliwa na mama msamaria mwema ambaye alijitolea kukabiliana na mbwa waliokuwa wakipigania kukatisha uhai wangu mara baada ya kutupwa jalalani na mama yangu ambaye simfahamu mpaka leo hii.

“Maisha yangu yalianza mara baada ya kuokotwa na mtawa aliyejulikana kama Yusta ambaye ni marehemu kwasasa. Niliambiwa kuwa aliniokota katika eneo la mji wa Lamu, Mombasa nchini Kenya kabla ya kuhamia jijini Arusha, alipokuwa akielekea kwenye misa ya alfajiri katika moja ya kanisa lililopo mjini hapo.

“Alinieleza kuwa wakati akielekea kanisani alfajiri ya Mei 25, 1989 ndipo aliposhtuka baada ya kuwaona mbwa wakigombania mfuko ambao ulikuwa umefungwa huku ukivuja damu nyingi.

“Mtawa yule ambaye awali nilikuwa nikidhani kuwa ni mama yangu mzazi, aliniambia kuwa mara baada ya kuusogelea mfuko huo alikuta mwili wa kichanga ndani yake ambaye nilikuwa ni mimi na kukichukua kisha kwenda kukilea kwa sababu hata yeye alikuwa ameokotwa na msamaria mwema raia wa Ujerumani kwenye tundu la choo na hivyo akaamua kwenda kulipa wema wake kwangu,” anasema Yustar.

Yustar anasema mtawa huyo ndiye aliyempa jina hilo na kwamba licha ya kutokuwa na wazazi lakini mtawa huyo alimlea katika maisha ambayo yalimfanya awe mwenye furaha na maadili ya kumtambua Mungu jambo lililomfanya ajihisi kuwa alikuwa mikononi mwa mama yake mzazi.

Anasema mtawa huyo ambaye alihamia jijini Arusha mara baada ya kuachana na huduma ya utawa, hakudumu muda mrefu kwani alifariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

“Mama huyu aliyekuwa akinilea alifariki dunia 1997 na kuniachia urithi wa maduka ya dawa, nyumba kubwa na magari matatu, lakini hata hivyo mali hizo zilikuwa ni chanzo cha maisha yangu mengine yenye machungu makubwa.

“Kwani nilijikuta nikiporwa kwa nguvu na mmoja wa watumishi ambaye alikuwa mfanyakazi wake ambaye nilipenda kumuita mjomba. Aliniomba nimpe hati ya nyumba na funguo mbalimbali lakini nilikataa kumwonyesha na hivyo akaamua kuniundia mpango wa mimi kutekwa nikiwa shule,” anaseme Yustar.

Anasema siku ya tukio, akiwa shuleni ilikuja gari ambayo huwa inatumiwa na mjomba wake iliyomtaka apande kwa madai kuwa mjomba wake huyo alikuwa akiumwa.

Hata hivyo, baada ya kupanda gari hilo alitupwa porini baada ya mpango wa kuuliwa kushindikana kufuatia radi kali iliyopiga na kuwauwa watu hao.

“Nilizibwa mdomo na vitambaa hatua ambayo imenifanya mpaka leo nibakie kuwa na kigugumizi kufuatia kuwa na maumivu makali, mjomba alikuwa ameandaa mpango wa kutaka kuniondoa duniani ili aweze kumiliki mali zote.

AOKOLEWA NA WAMASAI

“Mara baada ya kutupwa kwenye pori lenye misitu mikubwa niliokolewa na jamii ya Wamasai ambao hata hivyo walitaka kunitelekeza kwa kuamini kuwa nilishakufa siku nyingi baada ya kukaa siku tatu bila kuamka. Mara baada ya kuamka nilijikuta sijui hili wala lile jambo ambalo lilinilazimu kuanza kuchunga ng’ombe pamoja nao,” anasema Yustar.

Anasema baada ya kurejea kwenye hali yake ya kawaida wafugaji hao walimkabidhi ng’ombe wawili kwa nia ya kuwauza ili apate nauli ya kurejea Arusha.

“Baada ya kurejea Arusha nilikuta mambo yamebadilika kwani nilikuta palipokuwa na nyumba ya marehemu palishajengwa nyumba nyingine baada ya eneo hilo kununuliwa na raia mmoja wa kigeni na hivyo ikawa ngumu kwangu kuweza kuingia ndani.

“Ndipo nilipoamua kuingia mtaani na kuanza kufanya biashara ndogondogo kwani nilikuwa na akiba ya Sh 20,000 ambayo ilisalia kwenye nauli. Sikuwa na uwezo wa kwenda kushitaki popote kutokana na umri wangu kuwa mdogo na hivyo kuwa ngumu kupata haki zangu zingine,” anasema.

Anasema baada ya hapo alianza kufanya biashara ya kuuza mifuko ya plastiki, pipi, sigara na karanga huku akishindia mihogo ya kuchoma na kulala kwenye maboksi ya kordo za maduka yaliyoko mjini humo.

Chupuchupu kuuza figo

Kijana huyo anasema kuna wakati alifikia hatua ya kutaka kuuza figo yake moja ili aweze kumudu maisha ya kila siku baada ya kuchoshwa na yale ya mtaani.

“Ndipo nilipokutana na wasamaria wema ambao waliniambia kuwa kwa kuuza figo hiyo kwa Sh 500,000 kusingekuwa suluhisho la matatizo yangu.

“Walinisaidia na kunishauri nimrudie Mungu jambo ambalo limenisaidia sana, nimefanikiwa kuoa na nina mtoto na maisha yangu yanakwenda vizuri,”anasema Yustar.

AANDIKA KITABU

Yustar amefanikiwa kuandika kitabu cha ‘Maisha halisi ya watoto wa mitaani’, sambamba na kuanzisha mfuko wa James Foundation ulioko jijini Dar es Salaam.

“Kutokana na kuishi mtaani nimeweza kubaini kuwa kuna matukio ya kikatili ambayo watoto wa mitaani wanayapitia jambo ambalo limenifanya niyasimulie kwenye kitabu changu ili jamii iweze kuyafahamu.

“Watoto wengi walioko mtaani licha ya kwamba wanaonekana ni wezi na wadokozi lakini hayo yote yanasababishwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiachiwa kama walezi wao, hivyo kitabu hiki ambacho nimekiandika kwa msaada wa watu mbalimbali nataka kiufikie umma wa Watanzania ili wafahamu maisha yanayoendelea mtaani,” anasema.

Anasema jamii imekuwa ikiamini kuwa jukumu la kuwalea watoto wasio na wazazi ni la wafadhili pekee au serikali jambo ambalo ni kinyume, kwani wengi huhisi kuwa iwapo watatoa msaada kwa watoto wa mtaani basi wanaweza kugeuka na kuja kuwaibia baadaye wakati si kweli.

Anasema kwasasa haitaji watu wampe fedha mkononi isipokuwa anataka wamsadie kulipia gharama za uchapaji wa kitabu hicho ili viweze kuwa vingi na kuwaelimisha Watanzania wote.

Anasema amekuwa akipokea oda nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wanaotaka kujifunza juu ya maisha ya watoto wa mitaani.

“Nimeshindwa kuchapa nakala nyingi kwa sababu sina fedha na hata hivi vichache nilivyonavyo nimesaidiwa na wasamaria wema tu, hivyo nikipata fedha za kuchapa nakala nyingi nitakuwa nimewasaidia Watanzania wengi kupata elimu juu ya suala zima la watoto wa mtaani,” anasema Yustar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles