25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mutharika agonga mwamba mahakamani kuzuia uchaguzi

Lilongwe, Malawi

MAHAKAMA ya kikatiba nchini Malawi imetupa maombi ya Rais Arthur Peter Mutharika ya kuzuia uamuzi uliotolewa mahakamani wa kufuta matokea ya uchaguzi uliomwingiza madarakani Mei mwaka huu.

Wiki iliyopita mahakama ilibatilisha matokeo ya uchaguzi ambayo yalishuhudia Mutharika akishinda kwa ushindi mwembamba, ikieleza kuwa yaligubikwa na uvunjifu wa sheria.

Kutokana na hayo mahakama hiyo iliamuru kufanyika kwa uchaguzi mwingine mpya wa urais ndani ya siku 150 pamoja na kufanyika kwa uchunguzi juu ya operesheni zote zinazoendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya nchini humo (MEC).

Lakini Mutharika na tume walikata rufaa hiyo ambayo imesikilizwa na mahakama ya juu.

Uamuzi wa sasa wa Mahakama kukataa maombi ya Mutharika uliamriwa jana jijini Lilongwe.

” Hii ni kesi ya sheria za umma na sheria lazima zitumike kwa uangalifu,” alisema Jaji Dingiswayo Madise.

Mahakama hiyo  pia ilikataa hoja ya tume ya uchaguzi kwamba uchaguzi mwingine utagharimu nchi  hiyo maskini.

“Demokrasia ni gharama. Haki za raia ni kubwa. Mahakama haitaacha harakati za uchaguzi wa kikatiba kwa sababu ya gharama,”  alisema Madise.

Mkuu wa tume ya uchaguzi hapo awali alikuwa ametetea utumiaji karatasi za matokeo ambazo zilibadilishwa na  kurekebishwa.

Akiwa mbele ya kamati maalum ya Bunge, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), Jane Ansah alisema hakuona chochote kibaya katika tume yake kwa kuwa ilikubali karatasi ambazo zilibadilishwa na kurekebisha linalojulikana kama Tipp-Ex.

Alidai kuwa matokeo ya jumla katika karatasi hayakuchezewa bali yalisahihishwa.

“Hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kama Tippex ilitumika kumpendelea mgombea mmoja,” alisema.

Mahakama ya Kikatiba pia ilibaini kuwa chini ya robo tatu ya matokeo kutoka katika vituo 5,000 vya kupigia kura yalithibitishwa na wakaguzi na kisha Ansah kumtangaza Mutharika kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Mjumbe mwingine wa MEC, Mary Nkosi ambaye alifika mbele ya  kamati hiyo jumatatu alikiri kuwa tume ilishughulikia vibaya matokeo hayo.

“Sikuona uthibitisho wa hiki. Lakini kulikuwa na kuharakisha kidogo  kuhakikisha matokeo yanakusanywa pamoja na kutangazwa,” alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa matokeo ya urais kufutwa mahakamani kwa misingi ya kisheria nchini Malawi tangu ipate uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1964,  na matokeo ya pili kufutwa katika bara la Afrika baada ya yale ya Urais wa Kenya mwaka 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles