30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mongella awatahadharisha wahandisi

Yohana Paul – Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewatahadharisha wahandisi wenye leseni zilizoisha muda wake kuwa hawatapata nafasi ya kufanya kazi ndani ya mkoa wake kuanzia Aprili.

Alitoa tahadhari hiyo wiki iliyopita mkoani hapa, wakati akizungumuza na wahandisi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wakati wa kikao kilicholenga kutoa tathmini ya kazi za uhandisi nchini pamoja na nafasi ya wahandisi wazawa katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kitaifa.

Mongella alisema kuanzia sasa wahandisi wote wanatakiwa kuwa na leseni halali, hivyo wote wenye leseni zilizoisha muda wanatakiwa kulipia.

Alitoa nafasi hadi Machi 31, kila mmoja awe na leseni, kinyume na hapo atazungumza na wakuu wa wilaya wote wasifanye kazi nao.

“Serikali tangu imeingia madarakani imetoa kipaumbele kwa wahandisi wazawa kwa kuwa inaamini ndio mnaweza kulifikisha taifa katika uchumi wa viwanda pasipo kikwazo chochote na bila hujuma.

“Naomba mtambue ili mhandisi uweze kuaminika na kupewa kazi bila kutiliwa shaka, lazima uwe na leseni iliyohuishwa kwa maana ya ile ambayo inatambulika na mamlaka husika, hivyo nami kama kiongozi wa mkoa niwaambieni nitafanya kazi na wenye leseni zilizo ndani ya matumizi tu na si vinginevyo.

“Binafsi napenda kufanya kazi na kila mhandisi aliyekidhi kigezo, sitegemei baada ya muda wa mwisho wa kuhuisha leseni nilioutoa kuisha, kuona mhandisi mwenye leseni iliyoisha muda anakuja kuomba kazi Mwanza, nawaambia hakuna mhandisi atafanya kazi.

“Pia nakumbusha kazi ya uhandisi kama mnavyojua ni kazi ya kiapo, ndiyo maana leo pia kuna wenzenu wamekula kiapo, hii ni ishara kuwa kazi yenu inabeba roho za watu, inategemewa, jitahidini kufanya kazi kwa kuzingatia kiapo chenu ili kazi yenu iwe na manufaa kwa taifa lenu na si vinginevyo,” alisema Mongella.

Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi Tanzania (ERB), Patrick Barozi alisema hadi sasa kuna wahandisi waliosajiliwa 26,618 nchi nzima ambapo miongoni mwao, 2,925 ni wanawake sawa na asilimia 21.

Alisema kazi ya uhandisi mbali na kuwa ni taaluma, pia ni kama dhamana kwa kuwa inahusisha kiapo.

“Unapokuwa mhandisi unakuwa na nafasi kubwa ya kuisaidia nchi yako kwa kufanya kazi ama kwa kushauri jinsi ya ujenzi wa miradi mbalimbali.

“Nawaomba wahandisi wote, ikiwamo hawa 40 waliokula kiapo leo, wafanye kazi kwa kuzingatia kiapo na kwa kutambua thamani ya taaluma ya uhandisi.

“Kwani kuzingatia kiapo itasaidia kulinda maadili ya uhandisi na hii itaondoa changamoto ya wahandisi kufanya kazi bila mikataba, changamoto ambayo sisi wahandisi ni lazima tusimame pamoja kukemea.

“Na niiombe Serikali yetu kuhakikisha wahandisi wanakuwa na mikataba wanapofanya kazi sehemu yeyote ili kuepusha sintofahamu ambazo hujitokeza.” alisema Barozi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania(MSCL), Erick Hamis aliwataka wahandisi wote hasa wale wanaohitimu vyuoni kuwa na uthubutu wa kufanya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles