Na Arodia Peter, Dodoma
MUSWADA wa Habari unaotarajiwa kupelekwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, umeelezwa kuwa ni kandamizi na tishio kwa usalama wa nchi.
Muswada huo umepingwa ikiwa ni siku chache baada ya Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) kuwataka wabunge wasiupitishe kwa sababu hauna maslahi kwa taifa.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo, Waziri Kivuli, Joseph Mbilinyi (Sugu), alisema kambi hiyo inaungana na wadau wote wanaoupinga muswada huo kandamizi.
Sugu aliitahadharisha Serikali kutopeleka muswada huo katika Bunge la bajeti bila kuurudisha kwa wadau wake wakubwa na kufanya nao maridhiano kwa kurekebisha vifungu vinavyoendeleza ubabe wa Serikali na kunyima uhuru wa habari hususan kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba wa mwaka huu.
Sugu ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alisema maandalizi ya muswada huo ni mwendelezo wa sheria mbili kandamizi ikiwamo Sheria ya Makosa ya Mitandao na ile ya Takwimu ambazo zote zina lengo la kukandamiza uhuru wa waandishi wa habari na vyombo vyao.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalaani taarifa za kutishiwa maisha kwa mmiliki wa kituo cha televisheni cha ITV, Dk. Reginald Mengi eti kwa madai kuwa kituo chake kimekuwa kikitoa habari za uchochezi kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
“Hivi karibuni, vyombo vya habari vya kimataifa likiwamo gazeti kongwe la Washington Post la Marekani lilianika ubabe na kushinikiza wafadhili na wahisani na Benki ya Dunia (WB) kusimamisha misaada kuibana wa Serikali ya Tanzania kuzirekebisha sheria kandamizi ambazo zimesainiwa na rais,”alisema Sugu.
Katika hotuba hiyo, Sugu alisema changamoto kubwa inayowakabili vijana ni ukosefu wa ajira, lakini Serikali haijaonyesha dhamira ya dhati ya kushughulikia tatizo hilo.
Kutokana na hali hiyo, Kambi ya Upinzani ilipendekeza kuanzishwa Baraza la Vijana kuende sambamba na uanzishwaji wa mfuko wa vijana kuwezesha baraza hilo kujiendesha badala ya kuwa tegemezi kwa Serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Albert Ntabaliba alisema wamebani utoaji wa fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unashuka wakati idadi ya vijana inaongezeka.
Alisema kutokuwatengea rasilimali fedha ya kutosha kwa ajili ya mikopo, mafunzo ya ujasiriamali na ufuatiliaji wa shughuli za vijana ni hatari kubwa kwa taifa.