26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili yaweka rekodi kutengeneza jinsia ya kike

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeweka rekodi ya kihistoria kwa kufanya upasuaji wa kutengeneza jinsia ya kike kwa kijana aliyedhaniwa kuwa wa kiume.

Kijana huyo mwenye miaka 24 alitengenezewa jinsia ya kike kwa kutumia nyama za mwili wake ni kati ya wengine sita waliokuwa na tatizo la jinsia tata ambao wamefanyiwa upasuaji na kurekebisha.

Takwimu za kidunia zinaonyesha mtoto mmoja kati ya watoto 5,000 wanaozaliwa ana jinsia tata.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji kwa watoto waliokuwa na jinsia tata.

Akizungumza leo Februari 7,2024 na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Mohamed Janabi, amesema upasuaji huo wa siku 21 umefanywa na jopo la wataalam 20 kwa ushirikiano na nchi za Ireland na Jordan.

“Kuna wengine wamezaliwa na tundu moja tu, haja kubwa na ndogo zinatoka sehemu moja, tunarekebisha kwa kuangalia homoni zinaelekea upande gani zaidi.

“Unaweza kumkemea mtoto anafanya vitu vya kike lakini lawama hizi si nzuri, inawezekana homoni zake ziko XY (yaani mwanaume), lakini tabia zake zote za kike. Tuleteeni watoto tuwafanyie uchunguzi tupunguze kunyosheana vidole,” amesema Profesa Janabi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Idara ya Mkojo na Upandikizaji Figo, Gabriel Mtaturu, akizungumza kuhusu upasuaji kwa watoto waliokuwa na jinsia tata. Kulia ni Daktari Bobezi Upasuaji wa Watoto, Petronila Ngiloi.

Amesema ni muhimu jamii ielewe kuna changamoto hiyo na kuondokana na dhana potofu kwani tatizo hilo hutokea kwa bahati mbaya.

“Watoto wakizaliwa ni muhimu sana kuwachunguza badala ya kuwaficha, vitu vingi vinarekebishika. Hatuangalii tu tumeokoa fedha kiasi gani kwa kutowapeleka nje, nia yetu kubwa tunawarudisha kwenye hali zao za kawaida waweze kucheza na wenzao, kurudi shule,” amesema Profesa Janabi.

Naye Daktari Bobezi Upasuaji wa Watoto, Petronila Ngiloi, amesema kati ya watoto waliokuwa na jinsia tata wako ambao walikuwa wakionekana ni wavulana lakini kiuhalisia ni wasichana na wengine wasichana lakini kiuhalisia ni wavulana.

“Kundi la tatu ndio gumu zaidi mtoto anazaliwa na jinsia zote mbili; anakuwa mvulana na msichana kwa wakati mmoja.

“Wamama wengi hawana tabia ya kuwakagua watoto wao, hata kama una korodani moja bado ni tatizo na kama hakuna kabisa ni tatizo.

“Vinasaba vinavyotengeneza utu wa mtu vinaweza kutokea kitu kidogo kikanyofoka mtu akazaiwa na jinsia tata, hakuna wa kumlaumu ni bahati mbaya.

“Mtoto akiachwa na kukua hadi akawa mkubwa shida inakuja wakati wa balehe, anaanza kupata hedhi, anaota matiti, ngozi inakuwa nyororo na wengine umri ukiwa umeenda wanakataa kufanyiwa marekebisho kwa sababu ya mitizamo ya kijamii,” amesema Dk. Ngiloi.

Dk. Ngiloi amesema hakuna tafiti zilizofanyika nchini kuhusiana na tatizo hilo lakini akasisitiza kuwa lipo hivyo jamii ione umuhimu wa kupeleka watoto wenye changamoto hizo ili wafanyiwe uchunguzi.

Amesema mtu akifanyiwa upasuaji kuondoa maumbo ya kike atahitaji kupewa homoni aonekane mwanaume suala ambalo ni gharama kwa kuwa atatakiwa atumie katika maisha yake yote lakini akifanyiwa katika umri mdogo tatizo linatatuliwa.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Idara ya Mkojo na Upandikizaji Figo, Gabriel Mtaturu, amesema uchunguzi huo ulifanywa kwa kutumia vifaa vya kisasa kujua via vya ndani vya uzazi na baadhi walipenda kubaki na jinsia za kike.

“Tuliingiza kamera zinazotumika kufanya upasuaji wa matundu kwa sababu unaweza kuona mtoto ni mwanamke kumbe ndani ana korodani au ana via vya uzazi vya kike,” amesema Dk. Mtaturu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles