HARARE, ZIMBABWE
RAIS Robert Mugabe, ambaye huko nyuma dunia nzima ilimpenda, kutokana na uimara na upeo wake mkubwa wa kuwaongoza watu wake kupata uhuru, leo hii kwa sababu ya kutawala muda mrefu amejikuta midomoni mwa mamba ambao yeye mwenyewe aliwakuza.
Baada ya miaka 37 madarakani, Mugabe ambaye ana miaka 93 sasa, anaonekana kugeukwa na si tu na jeshi ambalo baadhi ya viongozi wake aliowangoza katika harakati za ukombozi, bali hata na maelfu ya wananchi ambao miongoni mwao katika siku za nyuma ilikuwa si rahisi kuona wakimpinga.
Jana, maelfu ya wananchi wakiwa wameambatana na wanajeshi, waliandamana katika mitaa mbalimbali jijini Harare kwa lengo la kumshinikiza Mugabe ajiuzulu wadhifa wake.
Wananchi hao waliandamana huku wakishangilia ‘kazi nzuri’ iliyofanywa na jeshi la nchi hiyo, kudhibiti shughuli zote za Serikali, ulinzi na usalama jambo ambalo limejenga ishara ya mwisho wa utawala wa miaka 37 wa kiongozi huyo mkongwe barani Afrika.
Hatua ya wananchi hao kuandamana, imekuja ikiwa ni siku tano tangu jeshi kuizingira nyumba ya Mugabe, kwa kile lilichosema kuwa kiongozi huyo amezungukwa na wahalifu, huku mkewe Grace akitajwa kuwa msingi wa kile kinachoshuhudiwa sasa.
Awali ilisemekana kuwa Grace amekimbia nchi, tetesi ambazo zilitiwa nguvu na kitendo cha Mugabe kuonekana hadharani akiwa peke yake juzi katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe (ZOU), lakini hata hivyo inaelezwa bado yupo ndani ya makazi yao na mumewe.
Kwa mujibu wa gazeti la Serikali la The Herald, maandamano hayo yameitishwa na viongozi wa Umoja wa Maveterani wa Zimbabwe, Chris Mutsvangwa, Victor Matemadanda na Douglas Mahiya, ambao siku chache zilizopita kabla ya jeshi halijaamua kuingilia kati, ilikuwa si rahisi kwao kumpinga Mugabe.
Akizungumza katika viwanja vya Highfield baada ya kukutana na waandamanaji, na kukaririwa na gazeti la NewsDay jana, Mutsvangwa alisema: “Hakuna jambo lolote lililopo juu ya mamlaka ya umma wa Zimbabwe na uamuzi unaochukuliwa na wananchi unapaswa kuheshimiwa hata na SADC.
Mutsvangwa alisema hayo kutokana na mkutano unaoendelea nchini Botswana wa Kamati ya Troika ya Siasa na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Troika).
Alisisitiza kuwa lazima Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Walter Mzembi, afukuzwe kwenye mkutano kwakuwa hajapata baraka zozote kutoka kwa wananchi.
“Kuna mkutano wa SADC-Troika unaendelea. Hatuna tatizo na mkutano huo, lakini kuna mtu kutoka Zimbabwe amehudhuria, kimsingi hakutakiwa kuwapo pale. Jina lake ni Walter Mzembi, nafasi yake aliyojiweka ni Waziri wa Mambo ya Nje.
“Mzembi, anatakiwa kwenda jela sasa chini ya jeshi, huyo ni sawa na wengine Jonathan Moyo (ambaye inasemekana kuwa mtu wa karibu na Grace), Saviour Kasukuwere na Ignatius Chombo.
“Mzembi yeye yupo kundi la wahalifu. Hastahili kuwakilisha Zimbabwe huko Botswana, tunataka kulinda sifa yetu na kesho (leo) ni siku yenyewe, tunamalizia kazi iliyoanzishwa na jeshi. Hakuna kurudi nyuma kuhusu suala la Mugabe. Anapaswa kuondoka,” alisema Mutsvangwa.
Inaelezwa kuwa maandamano hayo ambayo yalipangwa kuishia katika viwanja vya Highfield jijini Harare, yalikwenda mbali na kufika hadi Ikulu mbele ya vikosi vya jeshi.
Moja ya mabango ya waandamanaji lilisomeka: “Tunachotaka ni mabadiliko. Mugabe na mkewe wanapaswa kuondoka nchini,” lilisomeka bango moja.
Kiongozi aliyekuwa akiyaratibu maandamano hayo, aliwahamasisha waandamanaji kufika hadi katika makazi binafsi ya Mugabe kwenda kumshinikiza ajiuzulu.
Nje ya Ikulu ya Mugabe, Kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai aliwahutubia waandamanaji.
Mbali na Tsvangirai, viongozi wengine wa kisiasa walioungana na wananchi katika maandamano hayo ya kumpinga Mugabe, ambayo yameruhusiwa na jeshi na chama tawala cha ZANU-PF, ni pamoja na Patrick Chinamasa, Oppah Muchinguri na makamu wa rais wa Chama cha Movement for Democratic Change (MDC), Nelson Chamisa.
Uhusiano wa jeshi na ZANU-PF ni mkubwa sana.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), limesema kuwa waandamanaji walikuwa wakiwakumbatia wanajeshi wa nchi hiyo na kuimba nyimbo za kuwasifu.
Maveterani wa vita ambao hadi mwaka jana walikuwa watiifu kwa Mugabe, nao wanaunga mkono kuondolewa madarakani kwa kiongozi huyo.
“Kama Mzimbabwe, tunaliambia jeshi letu; Asante sana kwa mapinduzi ya amani.”
“Ni wakati mwafaka sasa wananchi wa Zimbabwe tuseme; Mugabe ondoka, lazima utoke kama jana. Hatutarajii kumwona tena anaongoza, ni mwanzo mpya.”
“Kwetu ni kuhusu mwisho wa utawala wa kiimla na tunaelekea kuirudisha Zimbabwe yetu mikononi mwetu.”
Hayo yalikuwa baadhi ya maneno yaliyokuwa yakisemwa na waandamanaji.
Mwanamke mmoja ambaye alikuwa amesimama nje ya Benki Kuu ya Zimbabwe, alisikika akisema: “Haya ni mapinduzi, yalikuwa yanakuja taratibu kwa muda mrefu.”
MUGABE CHINI YA UDHIBITI WA JESHI
Mugabe amedhibitiwa na jeshi tangu Jumatano lilipochukua uongozi wa nchi hiyo, lakini juzi alionekana hadharani kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Zimbabwe (ZOU) kufungua sherehe hizo kutokana na nafasi yake ya mkuu wa chuo hicho.
Jeshi la Zimbabwe lililazimika kuingilia kati mapema wiki hii mara baada ya Mugabe kumfukuza kazi Makamu wake, Emmerson Mnangagwa wiki iliyopita.
Taarifa zinasema kuwa Mnangagwa amekuwa akitazamwa kama mrithi wa kiti cha urais, hivyo kufukuzwa kwake kulitengeneza njia rahisi kwa Grace kukabidhiwa madaraka hayo makubwa Zimbabwe.
Juzi, jeshi lilikaririwa likisema kuwa mazungumzo na rais Mugabe yanaendelea, hivyo kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kusisitiza kuwa litawafahamisha kinachoendelea haraka iwezekanavyo.
HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA MUGABE
Wakati huo huo, Bunge la Zimbabwe linatarajiwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Mugabe.
Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la NewsDay, Mbunge wa Mabyuku-Tafara kwa tiketi ya chama cha upinzani cha MDC-T, James Maridadi, atawasilisha hoja binafsi ya kutokuwa na imani na rais.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho, mbunge huyo amemjulisha Spika wa Bunge, Jacob Mudenda, juu ya nia yake ya kuwasilisha hoja binafsi.
“Maridadi atawasilisha hoja binafsi na anaungwa mkono na wanasiasa kutoka pande tofauti. Wapo wabunge wa chama tawala cha Zanu-PF wamekubali kuwa Mugabe aondolewe. Kwa ujumla Spika wa Bunge amepewa notisi ya hoja binafsi siku ya Jumatano,” kilisema chanzo cha taarifa hiyo.
Hata hivyo, Spika Mudenda amekataa kupata taarifa hiyo. “Hapana. Sijaona hiyo taarifa,” alisema baada ya kuulizwa na NewsDay.
Maridadi hakuthibitisha wala kupinga juu ya mpango wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Mugabe.
Aliongeza: “Tafuta habari zote kwa watu waliokuambia suala hilo. Siwezi kuzungumzia taratibu za Bunge kwa jambo ambalo halijajadiliwa wala kuliona.”
Kwa upande wao Zanu-PF, kwa mujibu wa taarifa za ndani ya chama hicho, wana mpango wa kushinikiza Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Mugabe, baada ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 kudaiwa kukataa kuachia madaraka kama alivyoombwa na jeshi.
Taarifa zisizothibitisha zimeliambia NewsDay kuwa Mugabe amefanya jaribio la kumshinikiza Spika Mudenda kuahirisha Bunge bila mafanikio.
Spika alipouliza suala hilo, hakukataa wala kukubali, badala yake alisema: “Siwezi kusema lolote kuhusu suala hilo. Sisemi chochote.”
KURA YA HAPANA
Juzi, matawi 10 ya mikoa ya chama cha Zanu-PF, yalipiga kura ya hapana kumtaka Mugabe ajiuzulu kama rais na katibu mkuu wa chama hicho.
Pia yalikubaliana kuwa mkewe Grace anatakiwa kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho, pamoja na Mnangagwa kurudishwa katika nafasi yake ya ujumbe wa Kamati Kuu.
MAWAZIRI WAKAMATWA
Hata hivyo mkanganyiko umeibuka kutokana na jeshi kubainisha linawasaka wahalifu waliomzunguka Rais Mugabe pasipo kuelezea taarifa zaidi.
Mawaziri kadhaa wametajwa kukamatwa, wakiwamo Profesa Jonathan Moyo (Waziri wa Elimu ya Juu), Saviour Kasukuwere (Waziri wa Serikali za Mitaa, Maendeleo ya Miji na Makazi), Patrick Zhuwawo (Waziri wa Utumishi wa Umma, Kazi na Huduma za Jamii) na Ignatius Chombo (Waziri wa Fedha).
Aidha imeripotiwa kuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Jimbo la Manicaland, Mandi Chimene, hajulikani alipo hadi sasa licha ya tetesi kueleza kuwa huenda yuko China katika ziara ya ushirikiano wa Zimbabwe na nchi hiyo.
NAFASI YA MAVETERANI
Zimbabwe inajulikana kwa historia yake ya maveterani wa vita vya ukombozi wa uhuru, ambao wameunda chama chao.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zimbabwe, maveterani ndilo kundi kubwa lenye ushawishi na linatambulika kisheria.
Sura ya pili katika Ibara ya 23, 46 na 84 zinatamka haki, nafasi ya mavetarani kutambua umoja wao (chama) kuwa miongoni mwa alama za nchi, kama ilivyoidhinishwa katika makubaliano ya mwaka 1980 ya Lancaster kupitia mihimili yote; Serikali Kuu, Bunge na Mahakama.
Ibara ya 23(2) inatamka kuchukua hatua za msingi za kutunga sheria na kuwawezesha maveterani, wafungwa wa kisiasa, wapigania uhuru wote waliohusika na vita ya ukombozi wa Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Katiba, wanatakiwa kulipwa kiasi cha dola za Zimbabwe 50,000 na malipo ya kila mwezi dola 2,000.
Umoja wao sasa unaitwa Zimbabwe National Liberation War Veterans Association (ZNLWVA) na unaongozwa na Mutsvangwa.
ZNLWVA inajumuisha majeshi mengine, yakiwamo Jeshi la Wananchi (ZDF) na Jeshi la Ukombozi la Zimbabwe (Zimbabwe African National Liberation Army – ZANLA), ambayo yalipigana vita ya msituni ya Chimurenga kuikomboa Zimbabwe.