26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO POLISI ALIYETAJWA DAWA ZA KULEVYA ARUDISHWA KAZINI

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

ALIYEWAHI kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Christopher Fuime, ambaye alisimamishwa kazi takribani miezi tisa iliyopita sambamba na askari wengine 11 waliotajwa kujishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, amepewa cheo kingine, MTANZANIA Jumapili linaripoti kwa uhakika.

Gazeti hili linafahamu kuwa Fuime kwa sasa anaongoza Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kiuchumi, ambacho ofisi zake zipo maeneo ya Kamata, Dar es Salaam.

Kitengo hicho ndicho ambacho hivi karibuni kilimuhoji Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kwa tuhuma za kutoa takwimu za ukuaji wa uchumi zinazopingana na za Serikali.

Februari mwaka huu, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, alitangaza kuwasimamisha kazi Fuime na askari wenzake kwa lengo la kupisha uchunguzi kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria.

Askari hao sambamba na baadhi ya wafanyabiashara, wasanii na wanasiasa, ni wale waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa tuhuma za kujihusisha na ama biashara au matumizi ya dawa za kulevya.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Boaz, licha ya kukiri kwamba baadhi ya askari hao wamepangiwa kazi nyingine, alisema ofisi yake bado inaendelea na uchunguzi.

MTANZANIA Jumapili haikuweza kupata taarifa iwapo askari hao wote 12 wamerejeshwa kazini au la.

Awali kabla ya DCI Boaz hajathibitisha hilo, MTANZANIA Jumapili lilifika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuonana na Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Simon Sirro, ili kufahamu sababu za kuwarudisha kazini baadhi ya askari hao.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi hilo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa, alilitaka gazeti hili kuwasiliana na DCI Boaz na si Sirro kwa kuwa suala hilo lilikuwa katika hatua za uchunguzi.

Itakumbukwa Sirro ndiye alilishughulikia kwa ukaribu suala hilo kwa maana ya kuwaita na kuwahoji baadhi ya watuhumiwa wakati akiwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akishirikiana na Makonda na IGP wakati huo akiwa Mangu.

DCI Boaz pamoja na kukiri kuwa Fuime amepangiwa kazi nyingine, lakini alisisitiza kuwa bado ofisi yake inaendelea na uchunguzi wa tuhuma za askari hao 12.

Alisema askari waliorudishwa kazini ni kwa sababu ya uwepo wa mamlaka tofauti za kuwachukulia hatua.

“Ni kweli IGP wa wakati ule alitangaza kusimamishwa kwa askari hawa ili kupisha uchunguzi, lakini sio wote, waliosimamishwa ni wale ambao wapo chini ya mamlaka yake tu, wengine wanaripoti katika mamlaka za juu, hata huyo uliyemtaja (Fuime) kama yupo kazini ujue hauhusiki na IGP, wenye uwezo wa kumuwajibisha ni mamlaka za juu zaidi,” alisema DCI Boaz.

Alisema mamlaka za uwajibishaji wa askari ambao wamefanya makosa ya jinai, zipo tatu ambazo ni IGP na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Katibu Mkuu na Rais kulingana nafasi aliyonayo askari husika.

Boaz alisema Fuime hawezi kuchukuliwa hatua na IGP kwakuwa yeye anapaswa kuwajibishwa na Rais  ambaye uamuzi wake pia utategemea na matokeo ya uchunguzi wa tuhuma hizo kutoka katika ofisi ya DCI.

Aliongeza kuwa katika kundi la askari hao, wapo pia wanaopaswa kuchukuliwa hatua na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ambao nao hawawezi kuwa wamesimamishwa kazi na IGP.

Hata hivyo, Boaz alipotakiwa kutoa mchanganuo kulingana na makundi kwa askari hao waliotuhumiwa, aliahidi kutoa wiki ijayo.

“Kwa sasa nimesafiri nipo nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, naomba uje ofisini kwangu Jumatatu, nitakupatia majina ya askari waliotajwa na watu ambao wana mamlaka nao wa kuwawajibisha kwa  tuhuma walizonazo,” alisema.

Wakati Boaz akisema hayo, IGP aliyepita, Mangu katika mkutano wake na waandishi wa habari, miongoni mwa askari aliotangaza kuwasimamisha kazi ni Fuime.

Mbali na Fuime wengine waliotangazwa kusimamishwa kazi na Mangu ni aliyekuwa Ofisa wa Operesheni Kituo cha Oysterbay, Inspekta Jacob Swai, Sajenti Steven Ndasha na Sajenti Mohamedi Haima.

Wengine ni Sajenti Steven Shaga, Koplo Dotto Mwandambo, Koplo Tausen Mwambalangani, Koplo Benatus Luhaza, Koplo James Salala, Koplo Noel Mwalukuta, D/C Gloria Massawe na D/C Fadhili Mazengo.

Kutokana na maelezo hayo ya Boaz, MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na mamlaka ya Fuime ambayo ni Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Gerson Msigwa ili kufahamu matokeo ya uchunguzi dhidi yake na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli.

Msigwa alisema Rais Magufuli hahusiki na kusisitiza kuwa suala hilo aulizwe DCI kwani wao ndio wanaoendesha kesi hiyo.

“Rais hahusiki na mambo hayo, muulizeni DCI huko huko,” alisisitiza Msigwa.

MTANZANIA Jumapili halikuishia hapo, liliwasiliana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rodgers Siyanga, ambaye kupitia kwa msaidizi wake, alisema kuwa jalada kuhusu tuhuma za askari hao halijawahi kufika kwake na kwamba lilikuwa linashughulikiwa na polisi wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles