HARARE, ZIMBABWE
RAIS wa zamani wa Zimbawe Robert Mugabe (94) hawezi kutembea kutokana na afya yake kudhoofu, kwa mujibu wa Rais Emmerson Mnangagwa.
Mugabe amekuwa nchini Singapore akipata matibabu kwa ugonjwa usiojulikana katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Rais huyo wa zamani pia alifanya safari kadhaa kwenda kupata matibabu wakati wa siku za mwisho za uongozi wake.
Mnangagwa alichukua usukani kama rais mwaka mmoja uliopita baada ya Mugabe kuondolewa madarakani na jeshi lililoingilia kati kwa kile lilichoona Taifa kuburuzwa na mkewe Grace.
Hadi kipindi hicho Muganbe alikuwa amekaa madarakani kwa miaka 37, akianzia kama waziri mkuu na baadaye rais.
Rais Mnangagwa alikuwa akiongoza mkutano sehemu moja iliyo nyumbani kwa Mugabe wakati alipozunguzia afya ya mtangulizi wake.
“Sasa yeye ni mzee, na hawezi kutembea lakini chochote anachotaka tunampa,” Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) lilimkariri akisema.
Wakati Mugabe alipokuwa madarakani maafisa walisema alikuwa akitibiwa matatizo ya macho na kukana madai kuwa alikuw akiugua saratani.
Licha ya kushindwa kutembea, Mnangagwa alisema kiongozi huyo wa zamani anaendelea vyema na atarudi nyumbani wiki ijayo.
“Tunamhudumia. Yeye mwanzilishi wa taifa la Zimbabwe, Yeye ni baba yetu wa Zimbabwe iliyo huru,” Rais Mnangagwa, ambaye serikali yake inagharimia matibabu hayo ya Mugabe aliongeza.