Christina Gauluhanga, Dar es salaam
Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir ameagiza madrasa zote nchini kufungwa kuanzia leo Jumatano Machi 18, ili kupunguza ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Akizungumza na Mtanzania leo Jumatano Machi 18, jijini Dar es Salaam Sheikh Zubeir amesema agizo hilo linapaswa kutekelezwa haraka iwezekanavyo na kwamba taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Amesema kuhusu Swala ya Ijumaa na ile ya Jamaa zitaruhusiwa kwa sasa na huenda itabadilishwa kulingana na mazingira ya ugonjwa huo.
“Kuanzia sasa swala za Jamaa zinapaswa kuswaliwa kwa kuachiana nafasi na kuzingatia usafi ili kupunguza maambukizi,” amesema Sheikh Zubeir.
Amesema kwa maeneo ambayo yanawashukiwa wa ugonjwa huo na yamewekwa karantini hairuhusiwi kuendelea na swala hizo kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kuwa ni dhambi kumuambukiza ugonjwa mwenzio kwa makusudi,” amesema.
Amesema muislamu yeyote atakayepata na maradhi haya ni haramu kwake kuhudhuria swala za Ijumaa na Jamaa kama ambavyo ni haramu kwake kuchanganyika na wengine kwani kufanya hivyo ni kuisambaza na kueneza ugonjwa huo kwa wenzake.