Na Raymond Minja, Iringa
Mkurugenzi wa Halimashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Netho Ndilito, amemkabidhi gari ya kisasa aina ya Landcruiser mpya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Festo Mgina ili iweze kusaidia kutoa huduma katika vituo vya afya na hospitali zilizoko katika halmashauri hiyo .
Gari hiyo mpya iliyonunuliwa na serekali kwa Sh milioni 170 itasaidia kupunguza changamoto za utoaji huduma kwa wagonjwa walioko mbali ambao walikuwa wanashindwa kufika vituo vya afya ama hospitali kutokana na changamoto ya usafiri.
Akizungumza kabla ya kukabidhi gari hilo Ndilito alisema idara ya afya katika Halmashauri ya Mufindi inaendelea kufanya vyema kwani mpaka sasa imefanikiwa kuwa na Ambulance tano ambazo kila kituo cha Afya na Hospitali ya wilayani humo kuna huduma za gari la kubebea wagonjwa.
Ndilito ameishukuru serikali kwa kujenga vituo viwili vya Afya vyenye thamani ya Sh milioni 800 pamoja na hospitali ya Wilaya yenye thamani ya Sh bilioni 1.8.
Ndilito alisema kuwa halmashauri hiyo kwa kutumia mapato yake ya ndani itaendelea kujenga zahanati kila kijiji na vituo vya afya kila kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ili kuwasogezea wananchi huduma karibu ili wasitumie muda mrefu kufuata huduma jambo ambalo litasaidia kuokoa maisha yao.
Hata hivyo Ndilito alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/21 halmashauri hiyo inajenga kituo cha afya chenye thamani ya Sh milioni 400 katika kata ya Mapanda itakayosaidia wananchi wa kata hiyo kupata huduma karibu zaidi.
“Mwenyekiti gari hili ninalowakabidhi ni kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya lengo ni kupunguza vifo hasa kwa akina Mama, Watoto,cWazee na Vijana,” amesema.