26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto wa miezi mitano afungiwa kabatini

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano, jijini Dodoma amekutwa amefungiwa kabatini na mwajiri wa mama mzazi wa mtoto huyo ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani.

Kitendo hicho cha kinyama alichofanyiwa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), kimewashtua watu wengi.

Mapema jana katika mitandao ya kijamii zilisambazwa picha za video zikimwonesha mtoto huyo pamoja na mama yake, hali iliyoibua mjadala mkubwa, wengi wakilaani tukio hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema anazo taarifa juu ya tukio hilo na tayari amechukua hatua kuwashughulikia wahusika.

“Tayari watu wangu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wanafuatilia. Pia RPC (Kamanda wa Polisi), Mkoa wa Dodoma amesema analifahamu vizuri na analishughulikia kwa karibu sana akishirikiana na mkuu wa mkoa huo, hivyo tusiwe na wasiwasi,” alisema Waziri Ummy.

Taarifa zilizosambazwa mtandaoni zilidai tukio hilo limetekelezwa na mwajiri wa mama mzazi wa mtoto huyo alikokuwa akifanya kazi za ndani.

Inaelezwa mama huyo pamoja na mwanawe hivi sasa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakipatiwa matibabu.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ibenzi Ernes, alithibitisha kupokewa na kulazwa kwa mama na mwanawe huyo.

Alisema mtoto amefikishwa hospitali hapo siku tatu  zilizopita na kwamba atatibiwa kwanza tatizo la ukosefu wa lishe (utapiamlo).

Dk. Ibenzi alisema mama wa mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui kwa kile kilichodaiwa kupigwa na mwajiri wake hadi kupoteza fahamu.

“Mtoto anaendelea na matibabu kwakuwa bado tunamfanyia uchunguzi zaidi ikiwemo kufuatilia kama alipatiwa chanjo zote stahiki, na sisi tunatibu wagonjwa tu, mambo mengine watayafuatilia wahusika,” alisema

Taarifa za awali zinadai binti huyo alipata ujauzito akiwa nyumbani kwa mwajiri wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu wa shule ya msingi jijini humo ambaye alimtaka kufanya siri ili majirani wasifahamu kama yeye ni mjamzito.

Baadaye alifanikiwa kujifungua na kuendelea kufanya siri na mtoto kuhifadhiwa kabatini, hadi juzi ambapo inadaiwa alimpiga binti huyo hadi kupoteza fahamu ndipo majirani walipofika eneo la tukio na kugundua kulikuwa na mtoto mchanga ndani ya kabati.

TUKIO LA MTOTO NASRA

Matukio ya ukatili kwa watoto yamekuwa yakijirudia ambapo tukio kama hilo, liliwahi kutokea mwaka 2014,  ambapo mwanamke mmoja aliyetambuliwa kuwa ni Mariamu Said mkazi wa Kiwanja cha Ndege mkoani Morogoro, alijikuta akishushiwa kipigo na wananchi kutokana na kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne.

Tukio hilo ambalo lilivuta hisia kwa Taifa, lilitokana na majirani zake kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.

Zongo alisema majirani hao walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa nje.

Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu Mgagala na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo na kumhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa akijibu kwa kubabaika.

Moja ya maswali aliyoulizwa ni idadi ya watoto wake na akajibu kuwa ana wawili lakini wakati akiendelea kujibu maswali, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na kumkuta mtoto Nasra akiwa ndani ya boksi.

Ofisa mtendaji huyo alisema wakati wakimtoa mtoto huyo ndani ya nyumba, kundi kubwa la watu waliokuwa na fimbo na mawe walianza kumshambulia mwanamke huyo na kumlazimu mtendaji kutoa taarifa polisi.

Alisema muda mfupi baadaye, polisi waliwasili na kumkamata Mariam na kumpeleka katika ofisi ya kata ambako aliwekwa chini ya ulinzi.

Baadaye aliwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa Jamii.

Akijibu maswali ya polisi, mwanamke huyo alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na umri wa miezi tisa baada ya mama wa mtoto huyo kufariki dunia mwaka 2010.

Pia mtuhumiwa alikiri kwamba mtoto huyo hajawahi kupewa chanjo yoyote wala kupelekwa kliniki.

Alikuwa akitoa maelezo hayo huku akiwa amemshikilia mtoto huyo aliyetapakaa uchafu ikiwamo haja kubwa na ndogo alizokuwa akitoa ndani ya boksi na kusema kwamba mara ya mwisho alimwogesha Julai mwaka jana.

Mtoto huyo alikuwa akiwekewa chakula na maji ndani ya boksi lililokuwa nyuma ya mlango wa chumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles