NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila, amesema ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Northern Dynamo, wamemaliza kazi iliyobaki watakapokwenda ugenini.
Mtibwa iliibuka na ushindi huo dhidi ya Northen Dynamo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho uliochezwa juzi Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Ushindi huo ulikuwa mwanzo mzuri kwa Mtibwa Sugar ambayo imerejea katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho Afrika (Caf), baada ya kuikosa kwa miaka 15.
Mara ya mwisho timu hiyo yenye makao yake makuu mkoani Morogoro, ilishiriki michuano ya Caf mwaka 2003, kabla ya kufungiwa miaka mitatu, baada ya kukacha mchezo wake wa marudiano dhidi ya timu ya Santos ya Afrika Kusini.
Mtibwa iliupotezea mchezo huo na kukutana na rungu la Caf, baada ya kucharazwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Baada ya ushindi wa juzi, Mtibwa itaifuata Northern Dynamo kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Desemba 4, nchini Shelisheli.
Akizungumza baada ya mchezo na Northern Dynamo kumalizika, Katwila alisema ushindi huo utawafanya vijana wake kujiamini zaidi na kufanya vema katika mchezo wa marudiano.
“Kama vijana wangu wangekuwa makini basi leo tungeweka historia kwa kufunga mabao mengi.
“Lakini mabao 4-0 si haba, ushindi huu umetufanya tuamini kwamba tumebakisha kazi ndogo mbele yetu kabla ya kusonga hatua inayofuata, lengo letu kufanya vizuri katika kila mchezo.
“Tunakwenda kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza, lakini kubwa wachezaji wanatakiwa kufahamu kwamba, uhakika wa nani atakayecheza kikosi cha kwanza upo kwa mchezaji ambaye atafanya vema mazoezini,” alisema Katwila.
Naye kocha wa Dynamo, Cliff Nolin-Sina, alisema walifanya kosa kubwa kutowafuatilia mapema wapinzani, hatua iliyosababisha wapoteze mchezo kwa idadi kubwa ya mabao.
“Hatukuwafuatilia wapinzani wetu kabla ya mchezo huu, inawezekana hii ikawa sababu ya kufungwa kwetu, ila katika mchezo wa soka kila kitu kinawezekana hivyo si ajabu katika mchezo wa marudiano tukafanya maajabu,” alisema Cliff Nolin-Sina.