NA MOHAMED KASSARA
-DAR ES SALAAM
BAADA ya kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser, amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha wachezaji wao nyota hawaondoki badala yake wanasalia katika kikosi chao.
Mtibwa Sugar ilikata tiketi kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ilipoichapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali.
Baadhi ya wachezaji muhimu wa Mtibwa Sugar wanahusishwa na mipango ya kutaka kuihama timu hiyo na kujiunga na klabu kubwa nchini ambazo ni pamoja na Simba, Yanga na Azam.
Wachezaji wanaotajwa kuingia katika rada za klabu hiyo kwa lengo la kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni kiungo, Hassan Dilunga, ambaye anahusishwa kutaka kurejea Yanga na kipa Benedict Tinoco, anayesemekana kunyatiwa na Azam.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Bayser, alisema wanataka kusuka kikosi imara kitakachoshindana na si kushiriki michuano ya kimataifa.
“Baada ya kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi, tumepanga kufanya maboresho makubwa kwenye kikosi chetu, lengo ni kukisuka upya ili kiwe na sura ya ushindani wa kimataifa.
“Kwanza lazima tutahakikishe wachezaji wetu mahiri wanabaki,” alisema Bayser.
“Kama unavyojua Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limebadili ratiba ya michuano ya kimataifa, ilikuwa inaanza Februari, lakini sasa itaanza Desemba, hili limetufanya kubadili mipango yetu, hatutakuwa na timu imara kama tutaendelea kuuza wachezaji wetu muhimu, lazima tuwadhibiti,” alisema Bayser.