25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mtanzania aliyewekwa rehani Pakistan utata mtupu

unga-237x3001

JONAS MUSHI na TUNU NASSOR, Dar es Salaam

MATUMANI ya kumpata kijana Adamu Akida, akiwa hai nchini Pakistan, yanazidi kufifia huku Serikali ikishindwa kutoa majibu kuhusu hatima ya Mtanzania huyo.

Adamu  amewekwa rehani nchini humo na ndugu yake Juma Mwinyi.

Video zake (Akida) zilizokuwa zikisambaa kwenye mitando ya jamii Julai mwaka huu,   alikuwa akiomba msaada wa kuokolewa kutoka kundi la watekaji hao wenye silaha nzito.

Tangu kuripotiwa kwa tukio hilo miezi minne iliyopita, ukimya umeendelea kutawala licha ya Polisi nchini kuwahi kuahidi kuwasiliana na serikali ya Pakistan ili kumwokoa Akida.

Hata hivyo, hadi sasa  suala hilo   limeghubikwa na giza nene huku hatima ya kijana huyo ikiwa haijulikani.

MTANZANIA limefuatilia suala hilo na kubaini kuwa hakuna matumaini ya kuokolewa kwa kijana huyo kwa vile   ndugu wa karibu na vyombo husika vya Serikali hawalipi kipaumbele.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na ile ya Mambo ya Nje na Ushirikianao wa Afrika Mashariki zimekuwa zikirushiana mpira huku jeshi la polisi likionekana kulisahau suala hilo.

MTANZANIA ilipofika katika Wizara ya Mambo ya Nje na kutaka kuonana na Msemaji wa Wizara hiyo iliishia mapokezi baada ya simu kupigwa kwa mtu ambaye baadaye alijitambulisha kuwa ni Katibu Muhutasi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake.

Alipoelezwa sababu za kutaka kuonana na Msemaji wa Wizara hiyo baada ya kuhoji, alisema suala hilo limekwisha kutolewa majibu kwamba linashughulikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Kipindi kile ulipokuja kuulizia suala hilo uliambiwa kuwa suala hilo linashughulikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu linahusu uhalifu na sisi hatuna taarifa mpya kuhusu suala hilo,” alisema.

Katika Wizara ya Mambo ya Ndani, MTANZANIA ilizungumza na  Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara hiyo, Christina Mwangosi, ambaye alisema: “Suala lolote linalotokea nje ya nchi huwa tunategemea kupata taarifa kutoa Wizara ya Mambo ya Nje.”

MTANZANIA ilipomtafuta kwa   simu Msemaji wa Jeshi la Polisi,   Advera Bulimba, ambaye ndiye aliwahi kunukuliwa   akiahidi kufuatilia suala  hilo, zamu  hii alionekana kusahau na kumtaka mwandishi amkumbushe vizuri kwa kumwandikia ujumbe mfupi wa maneno kama ifuatavyo:

MTANZANIA: Jeshi la Polisi lilinukuliwa likisema kuwa litawasiliana na Serikali ya Pakistan ili kumwokoa kijana Mtanzania aliyetekwa na genge la wauza unga. Je mefikia wapi?

Advera: “Nani alisema Jeshi la Polisi litafuatilia suala hilo?

MTANZANIA: Wewe  (Advera) ndiye uliyenukuliwa.

Advera: “Sikumbuki hicho kitu kwa sababu Jeshi la Polisi lina mambo mengi hebu niandikie ujumbe mfupi wa maneno unikumbushe.

MTANZANIA ilipomwandikia kumpa historia ya suala hilo wiki iliyopita, hakujibu chochote na hata alipopigiwa simu hakupokea hadi kufikia jana.

Kwa upande wa ndugu, MTANZANIA ilizungumza na Baba mdogo wa Adamu, Kessy Baharia.

Alisema tangu ahojiwe na vyombo vya dola wakati wa suala hilo (miezi minne illiyopita)hajawahi kupewa taarifa zozote.

Alipoulizwa kama aliwahi kufuatilia kwa viongozi wa serikali za mtaa na jeshi la polisi alisema: “Mimi sifuatilii suala hilo tangu nilipotoa maelezo kwa vyombo vya dola sijawahi kufuatilia na sina taarifa yeyote.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles