Cape Town, South Africa
Balozi wa Rwanda, nchini Afrika Kusini, Vincent Karega, ameitwa na serikali hiyo baada ya mtandao unaoipendelea serikali yake kumkashfu Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Lindiwe Sisulu.
Taarifa ya mtandao huo unaoipendelea serikali ya Rwanda, ilikuwa na kichwa kinachomuita Waziri Sisulu kahaba.
Msemaji wa Sisulu, Ndivhuwo Mabaya, ameviambia vyombo vya habari kuwa matamshi hayo hayatakubaliwa na lazima yachukuliwe hatua ili kukomesha tabia hiyo.
Sisulu alikosolewa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na ofisa wa cheo cha juu wa Rwanda, baada ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa alikutana na mkuu wa zamani wa majeshi nchini Rwanda Faustin Kayumba Nyamwasa, mjini Johannesburg.
Nyamwasa, amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini, tangu mwaka 2010 baada ya kutofautiana na rais wa Rwanda Paul Kagame.
Hata hivyo Balozi wa Afrika Kusini, mjini Kigali, George Twala, ameitwa kwenda Prerotia, kwa majadiliano.