32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mtandao wa simu za wizi Tanzania wanaswa Kenya

BENJAMIN MASESE-MWANZA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, limesema tayari limenasa mtandao wa mafundi simu wanaonunua simu za wizi  zenye thamani kubwa na kwenda kuziuza au kubadilishana na wahalifu wa nchi jirani ya Kenya ambao hukutana mpakani.

Akijibu maswali ya wadau mbalimbali katika semina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa watoa huduma za mawasiliano nchini, Mussa Zuberi, kutoka kitengo cha makosa ya mitandao Mkoa wa Mwanza, alisema mtandao huo umebainika baada ya kuanza kuwakamata mafundi simu na kuwahoji.

Alisema baada ya Jeshi la Polisi kupokea kesi nyingi za upotevu wa simu na kufuatilia, ilibainika hupelekwa kwa mafundi simu ambao huziondoa namba ya siri na kubadilisha namba ya utambulisho yaani IMEI kwa matumizi.

TCRA imeandaa semina kwa wadau mbalimbali wakiwamo kampuni za mawasiliano Tanzania, viongozi wa umoja wa mafundi simu, waandishi wa habari, viongozi wa dini  na wadau wengine wa sekta hiyo lengo likiwa ni kukumbushana taswira ya sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015 na changamoto zinazojitokeza.

Zuberi alifafanua kwamba, baadhi ya simu nyingine ambazo mafundi hao huzinunua huzipeleka mpakani mwa Kenya na Tanzania na kuziuza au kubadilishana na mafundi wa Kenya jambo ambalo huwafanya polisi kitengo cha makosa  ya mitandao kupata ugumu wa kuzipata kwani huwa hazionekani katika mfumo wa mtandao.

“Hadi tunapozungumza sasa tayari baadhi ya mafundi wanashikiliwa kwa vitendo hivyo na wametueleza namna biashara hiyo inavyofanyika, wanakwenda kule mpakani Sirari upande wa Tanzania wanakutana na wenzao wa Kenya wanabadilishana au kuuziana hizo simu za wizi, ndio maana mtu anaweza kuleta malalamiko tukashindwa kuipata simu yake.

“Tunapoitafuta kwenye mfumo wa mtandao  wetu haipatikani kwani inakuwa nje ya Tanzania, lakini mtumiaji yule anapokuja upande huu huwa inasomeka kwa muda na kutoweka sasa inakuwa vigumu kuifuatilia kwani tunakuwa mbali na mhalifu.

“Kikubwa tunachowaomba mafundi simu watambue kitendo cha kuanza kuchokonoa simu kwa kufuta namba ya siri iliyowekwa na mhusika sambamba na IMEI ni kosa, kosa la pili ni kuuza mali za wizi, hivyo tumewataka kuacha biashara hiyo na kushirikiana na polisi kuwakamata wale wanaowapelekea simu,” alisema.

Zuberi alisema hivi sasa wanatarajia kukutana na watu wa idara ya uhamiaji kuona namna ya kufanya ukaguzi mpakani Sirari mkoani Mara katika  mabegi ya abiria na pale wanapokuta mtu akiwa na simu nyingi ambazo hazimo katika maboksi rasmi au kutokuwa na stakabadhi za manunuzi zinapaswa kushikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Naye Mkuu Msaidizi wa Kitengo cha uhalifu wa kimtandao kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi, Joshua Mwangasa, alisema tangu mwaka 2015 takwimu za makosa zimekuwa zikiongezeka na kupungua.

“Ukiangalia mwaka 2015 tulipokea makosa 5,172,  2016  (9,441),  2017 (7,889) na mwaka 2018 tulipokea 8,708  hapo utaangalia yanapanda na kushuka lakini nasema tunakoelekea 2020 tunakwenda katika kiwango cha juu cha matumizi ya teknolojia ambacho kila mtu shughuli zake zitakuwa kwenye simu.

“Tukumbuke hata vitabu vitakatifu vimeandika siku za mwisho maarifa yataongezeka, hivyo kuanzia mwaka 2020 Watanzania wataanza kutumia kiwango cha 5GB, ni lazima sasa kama polisi na TCRA tukaanza kutoa elimu ya namna ya kuepuka kuingia kwenye makosa ya jinai.

“Matokeo ya matumizi mabaya ya mtandao wa kijamii yamegawanyika sehemu tatu, kwa upande wa kijamii  unaleta mmomonyoko wa maadili, upande wa siasa inaleta uvunjifu wa amani na kundi la mwisho lipo kwenye uchumi na athari zake ni kuharibu mfumo muhimu wa kitaifa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles