27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awatumia salamu majangili

GRACE SHITUNDU

RAIS Dk. John Magufuli amewatangazia kiama wauaji wa tembo ndani na nje ya nchi na kumtaka Mkuu wa Hifadhi ya Selous kujipanga vizuri.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana, wakati akizindua barabara ya kilomita 193 ya Namtumbo, Kilimasera, Matemanga hadi Tunduru, katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

 “Washtakiwa wa eneo hili wengi ni wanaoua tembo, unakuta Watanzania wanashirikiana na majangili wa nchi jirani, wakiua tembo huku wanawapeleka kule na wakiua tembo kule wanawaleta huku.

“Mtandao wote tumeshaujua, mkae mwendo wa mchakamchaka, wapo wengine wanashirikiana na viongozi, ninafahamu circle.

 “Tunataka Selous iwepo, sasa anayehusika na Hifadhi ya Selous ajipange vizuri, wengine wanaoshirikiana na kutengeneza mtandao ni watendaji kazi wa Selous,” alisema.

Akizungumzia barabara hiyo, Rais Magufuli alisema ujenzi wa kilomita 193 si kazi ndogo na umetumia zaidi ya Sh bilioni 173.3.

Alisema fedha hizo zilizotumika kutengeneza barabara ya lami wangeambiwa wananchi wa Tunduru wachange hata kwa miaka 200 wasingeweza kufanikisha.

 “Jana tulikuwa kwenye mradi mwingine wa kutoka Mtambaswala kuja mpaka Tunduru kupitia Nakapanya jumla ya kilomita 202.5, pia kutoka Namtumbo kuelekea Songea mpaka Mbinga, barabara ile imeshamalizika kwa kiwango cha lami, kipande kilichobaki ni kutoka Mbinga kwenda Nyasa kilomita 67, ambazo nazo kandarasi anaendelea na kazi,” alisema.

 “Wapo wazee wetu wametangulia bila kuona lami na hata huko waliko ukiwaambia kuwa sasa Tunduru kuna barabara ngumu ukikanyaga unaumia, inawezekana wasikuamini, lakini hizi ndizo changamoto katika maendeleo.

 “Nikiwa Waziri wa Ujenzi nilijitahidi kwa kiasi changu, lakini wapo pia niliowaudhi, ninajua niliowaudhi watakuwa wamenisamehe, hao ni wale waliokuwa wamejenga kwenye hifadhi ya barabara hapa Tunduru na nikabomoa nyumba zao,” alisema.

Alisema mwingine aliyemuudhi ni kampuni ya kandarasi ya Progressive, ambaye alipewa maeneo yote matatu ajenge kwa kiwango cha lami, yeye akaweka vifaa bila kutengeneza chochote.

“Nikamchongea kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na wakati huohuo akamfukuza na vifaa vyake vikashikwa na kupigwa mnada,” alisema.

Akataa mkoa mpya

Kuhusu Tunduru kupewa mkoa wao, Rais Magufuli alisema haoni umuhimu wa kuongeza mikoa wakati wananchi bado wanahitaji huduma za maendeleo.

“Mmeimba wimbo kutaka hapa pawe Mkoa, ni mawazo mazuri, lakini inawezekana bado wakati haujafikia, kitu kikubwa katika kuleta maendeleo si kuwa na mkoa, bali kupeleka vitu vinavyohitajika katika eneo hilo.

“Ukiufanya mkoa wa Tunduru ukaacha kuwapelekea umeme, ukichukua fedha ukaanza kujenga majengo ya wakuu wa mikoa ambao utakuwa unawalipa mishahara halafu usiwapelekee maji utakuwa hujaisaidia Tunduru.

“Kwa sababu mahitaji ya watu wa Tunduru si kumwona Mkuu wa Mkoa na kitambi chake akitembea barabarani, wanataka shida zao wana-Tunduru zimaliziwe,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hata kuwa na mikoa 26 anaona hapakuwa na sababu, kwani ingewezekana kuwa na mikoa michache na gharama zinazotumika kuendeshea mikoa zikatumika kwa maslahi ya wananchi.

“Tukajenga hospitali, tukanunua dawa, tukajenga shule tukapeleka umeme, wakawa na magari ya wagonjwa, hapa mnalalamika kwamba mmejitolea kwa ajili ya hospitali ya hapa, mmechanga Sh milioni 189, sasa nitawaongezea milioni 200, sitaweza kutoa fedha hizi kwa ajili ya kujenga ofisi ya Mkoa wa Tunduru.”

Kuhusu maji

Kuhusu maji, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, kuwashughulikia makandarasi wanaokuwa na visingizio mbalimbali vya kukwamisha miradi ya maji wakati fedha zote zimeshalipwa.

Alisema katika wahandisi ambao wamekuwa wakifanya vibaya hapa nchini ni wale wa maji, pia miradi mingi ya maji haikamiliki sambamba na kuwa na miradi hewa.

“Nataka kuona makandarasi wa maji wakifukuzwa, kwenye kazi hizi za ujenzi ukiwa mpole hakuna mradi utakaomalizika, ni lazima kuwa kichaa kichaa.

Kuhusu kiwanda

Alisema wabinafsishaji walipewa viwanda hivyo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, lakini hawafanyi hivyo.

Alisema kwamba Tunduru kuna kiwanda cha korosho ambacho mwenye kiwanda aliuziwa kwa Sh milioni 75, ingawa kiwanda hicho thamani yake ni ya mabilioni.

“Kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua korosho tani 10,000, lakini hadi sasa hawajatengeneza hata tani 1,000, walikopeshwa na Serikali tani za korosho 588, hapo ndio unaweza kujua madhara ya ubinafsishaji,” alisema.

Akizindua Veta Namtumbo

Akizindua Chuo cha Ufundi VETA Namtumbo, kilichogharimu Sh bilioni 6.4, alisema wataalamu na watendaji wabadilike kuhakikisha miradi wanayofanya thamani yake inaendana na uhalisia.

Alisema amefurahi kuzinduliwa kwa chuo hicho, lakini  amekuwa na wasiwasi na thamani ya ujenzi wake.

 “Nimefurahi kuzindua chuo hiki, lakini ninachojiuliza je, ujenzi wa hiki chuo thamani yake ni bilioni 6.4? Chuo cha Kitangani nilichozindua siku nne zilizopita kiligharimu Sh bilioni 4.2.

“Na kina maghorofa matano, nyumba za walimu, ukumbi wa mihadhara, bwalo la chakula, maabara na umetuma bilioni 4.2 tu,” alisema.

Alisema wakandarasi wengi wazalendo wanaopata kazi ni asilimia 40, hivyo alimtaka mkandarasi wa chuo hicho kutoingia mkenge na kula nao asilimia 10.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles