Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyo ya Serikali (NACONGO) na Mtandao wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wameiomba serikali kuhakikisha mchakato wa uhakiki wa asasi zisizo za  raia hautatumika vibaya kwa kuzidhibiti baadhi kwa hila zozote.
Kauli ya viongozi hao imetolewa kutokana na tangazo la serikali lililotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu msajili wa mashirika yasiyo ya  serikali kuanza uhakiki wa mashirika hayo ifikapo Agosti 21 hadi 31 mwaka huu.
Mratibu wa Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alikuwa akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana.
Alisema wanaisihi serikali kuhakikisha  a mchakato huo wa uhakiki hautumiki vibaya na baadhi ya viongozi kama njia ya kudhibiti na kuzipoteza au kuzifuta baadhi ya asasi kwa sababu zisizoeleweka.
Alisema wanaamini endapo hatua hiyo itafanyika vizuri na kwa nia nzuri  inaweza kuleta manufaa kwa taifa.
Alisema mchakato huo pia utasaidia kuondoa kwenye orodha mashirika yaliyoshindwa kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu na kufanya orodha ya mashirika kuwa halisi na yenye tija kwa jamii.
“Kwa muda mrefu sasa mchango wa asasi za  raia umekuwa hautambuliwi kitaifa pamoja na kwamba sekta hiyo hutoa ajira kwa Watanzania wengi, huingiza fedha za kigeni na kuchangia kwa asilimia kubwa katika makusanyo ya kodi na maendeleo ya watanzania kwa ujumla,’’alisema Olengurumwa.
Alisema   uhakiki umetangazwa kufanyika katika kanda tano za nchi lakini   wasiwasi upo katika muda uliopangwa na suala la umbali.
Alisema itakuwa vigumu kwa mashirika yasiyo ya serikali yaliyoko katika maeneo ya mbali kufika kwa urahisi katika ofisi za usajili katika kanda na wengi watashindwa kushiriki.
Pia alisema   kutokana na ukosefu wa rasilimali ambao mashirika mengi mikoani yanakabiliwa nayo,   itakuwa vigumu kwa mashirika yasiyo ya  serikali kusafiri kwenda kwenye ofisi za kanda zilizotengwa kwa muda wote wa uhakiki.
Katibu wa NACONGO, Ismail Suleiman aliyataka mashirika yasiyo ya serikali kuhakikisha   yanalipa uzito unaostahili suala hilo kwa kufika mapema katika ofisi za kanda zilizopangwa   kufanya uhakiki katika muda uliowekwa.
Pia alitoa wito kwa wasajili wasaidizi kote nchini kuhakikisha  wanaanza kutoa barua za utambulisho   haraka kadri AZAKI zitakavyokuwa zinaomba kupewa barua hizo.