- DERICK MILTON-BARIADI
ANTONY Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, kiongozi ambaye kila siku amekuwa akiamini katika kutekeleza ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Amekuwa mwanasiasa na kiongozi ambaye haamini katika uongozi wa kutoa matamko ambayo anaeleza hayana msingi wala hayatatui shida za wananchi wake.
Machi 11, 2019 taasisi ya Mwalimu Nyerere chini ya Mkurugenzi wake Joseph Butiku, waliendesha mdahalo kuhusu uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote ambao ulifanyika mjini Bariadi.
Katika mdahalo huo ambao mkuu huyo wa mkoa alikuwa mgeni rasmi, ulihudhuriwa na wakuu wa wilaya zote za mkoa huo, wenyeviti wa halmashuari, wakurugenzi na makatibu tawala wa wilaya.
Akifungua mdahalo huo Mtaka alionekana kutokubaliana na viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini ambao wamekuwa wakiamini zaidi kuongoza kwa matamko.
Mtaka aliwataka viongozi wenzake katika maeneo yao ya kazi, kutumia nguvu kubwa kujifunza kuliko kutumia nguvu kubwa kutoa matamko na kutumia madaraka yao vibaya.
Alisema kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wamepewa nguvu kubwa na Rais, ambapo alisema kama nguvu hizo watazitumia kutatua changamoto za wananchi Tanzania itakuwa nchi yenye maendeleo makubwa.
Alisema kuwa kiongozi yeyote lazima ujifunze kwanza kuliko kukimbilia kutoa matamko ambayo hayana tija kwa wananchi ambao ni wanyonge na maskini.
“ Kama ukuu wako wa mkoa, wilaya ni kujiongezea walinzi na wafuasi huo ni ujinga, viongozi lazima tutumie nguvu kubwa kujifunza kuliko kutumia nguvu kubwa kutoa matamko, kwa sababu hautaki kujifunza.
“Unataka kuamua, unaamua hata usiyoyajua, hapo huwezi kufanikiwa, Rais asubuhi anakuteua kuwa DC, DED jioni unaanza kuwaweka watu lokapu, wewe utaendesha uchumi wa wapi? Alihoji Mtaka.
Mtaka alisema kuwa kama viongozi wenzake wanataka kupata maendeleo yale ambayo Rais Magufuli anayahitaji kwa wananchi wake lazima watoke katika kapu la kimadaraka.
Anaeleza kuwa ikiwa viongozi wote wataona kuna haja ya kujifunza kutoka kwa wasaidizi wao na kuwasikiliza, changamoto za wananchi zitaweza kutatuliwa na kufikia maoni ambayo Rais magufuli anayahitaji kwa wananchi wake.
“Mimi nimekuwa nikijisikia faraja na kujiona kuwa ni mkuu wa mkoa, pale ninaposhauriwa na wasaidizi wangu, kwenye sheria, kilimo na sehemu nyingine, huo ndiyo uongozi ambao hata Mwalimu Nyerere aliamini,” alisema Mtaka.
Mtaka alisema kuwa ikiwa viongozi wote wanaomsaidia Rais Magufuli wataweza kumtafsiri vyema katika utendaji kazi wake, wengi wataepuka kufanya kazi kwa matamko haya yale ambayo hayana tija.
“ Kama viongozi wote tungeliweza kutohoa kwa yale ambayo Rais wetu anafanya kwa Watanzania, maana yake ni jambo la kuchukua (copy), kuweka (paste) na kutekeleza (Implement),” anasema Mtaka.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutekeleza kwa vitendo maono ambayo alikuwa nayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha jambo na kulitekeleza.
“Baba wa Taifa alipinga rushwa, leo tunaye Rais ambaye anatekeleza hilo jambo kwa vitendo, ametekeleza mradi wa umeme Rufiji, Reli ya umeme, ununuzi wa ndege, yote hayo yalikuwa matamanio ya Mwalimu,” alisema.
Viongozi kugombana.
Mkuu huyo wa Mkoa aligusia baadhi ya matukio ya viongozi kugombana wakati wako katika eneo moja la utawala, ambapo alieleza kitendo hicho ni kumdharau Rais.
Mtaka alisema kuwa viongozi walioko kwenye eneo moja hawapaswi kugombana na badala yake wanatakiwa kushirikiana na kupendana ili kuwaletea wananchi maendeleo.
“Viongozi kugombana huo ni ujinga na kwangu haliwezi kutokea, wewe mkuu wa wilaya au mkurugenzi una gari zuri, nyumba, mshahara mzuri, posho, unapewa pesa ya maji, umeme, kwa nini ugombane na mwenzako, huu ni ujinga na haufai tena kuitwa kiongozi,” alisema Mtaka.
Alibainisha kuwa katika mkoa wake jambo hilo haliwezi kutokea kuona viongozi wanagombana, wala yeye hawezi hata siku moja kugombana na katibu tawala wake, kwani uongozi ni kushirikiana na kusaidiana.
“Tunamsumbua Rais badala ya aongelee maendeleo ya nchi na kufanya kazi kuwaletea maendeleo wananchi wake, anaanza kufanya kazi ya kuongelea watu wanaogombana.
“Anatumia muda wake
kusuluhisha watu wanaogombana, hii ni kumdharau Rais, viongozi lazima tuheshimu
hii nafasi ambayo Rais wetu Magufuli ametupatia,” alisema Mtaka.
“Wakati mwingine nawashauri viongozi wenzangu kuwa, itakusaidia nini wewe ni mkuu wa wilaya kwenye eneo lako kauli zako zinaleta tension (mvutano) hata kwa unawaongoza.
“ Kauli zako zinabomoa hapo hapo ulipo, hilo jambo kama sisi mkoa tumeliepuka, huku Simiyu kila mkuu wa wilaya anacho kitu cha kujivunia kuwa amekifanya kwa ajili ya wananchi na si migogoro,” alisema Mtaka.
“ Hata hawa wakuu wa wilaya nawaambia kila siku hizi, kazi zetu za kuteuliwa siyo kusema kuna tume ya utumishi itakuja kufanya ukaguzi ili upandishwe daraja, kwa nini umpe shida anayekuteua ajiulize maswali ya kwanini nimrudishe huyu DC au Ded kwenye nafasi hiyo,” anasema Mtaka.
Simiyu kuishangaza nchi.
Mtaka alisema kuwa Mkoa wa Simiyu utawashangaza wengi, kwani umekuwa na viongozi ambao wanawasikiliza wananchi, kushirikiana katika jambo wala si mkoa wenye matamko.
“Nasema hapa mkoa huu utawashangaza wengi, kama mkoa tunataka kufikia maono ambayo Rais Magufuli anayataka kwa Watanzania wake, mimi ni kiongozi wao nasema hapa tutashangaza wengi.
“Tunataka kuwapunguzia watu kwenda kujifunza nje ya nchi, Rwanda, Japani, watu watakuja Simiyu kwa ajili ya kujifunza, ndani ya mwaka mmoja tutavuka malengo ya Rais Magufuli,” alisema Mtaka.
Alisema kupitia ushauri ambao walitoa kwa serikali, ilianzishwa mfumo wa kutolewa kwa pesa za miradi ya kimkakati, ambapo Wilaya ya Maswa wamepewa kiasi cha Sh.bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha chaki na vifungashio.
Alisema mbali na hilo serikali pia imetoa pesa kwa ajili upanuzi wa kiwanda cha maziwa kilichopo wilayani Meatu, huku wilaya ya Bariadi wakitarajia kujenga kiwanda cha vifaa tiba.
“Huko nyuma serikali ilikuwa inatoa pesa kwa halmashauri kwa ajili ya kujenga stendi na vitu vingine, tukawashauri kwa miaka mitatu, kwa nini pesa hizo zisitolewe kwa ajili ya kuongeza thamani mazao ya wananchi wa chini kabisa.
“Unatoa pesa kwa ajili ya kujenga stendi, huku nyanya za mkulima zinaliwa na mbuzi, kwa nini tusijenge kiwanda ili kumsaidia huyu mkulima, nimekuwa nawaambia halmashuari tuachane na fikra hizi za ushuru wa nyanya, mchicha na tuanzishe miradi mikubwa,” alisema Mtaka.
Alisema katika Mkoa wa Simiyu, wamefanikiwa kufikia yale maono ambayo Rais magufuli amekuwa akiyatamani na ndio maana katika mabadiliko mbalimbali ya viongozi Simiyu haijawahi kuguswa.
“Nimekuwa nikiona au kusoma kuwa kesho au baadaye Rais atatangaza mabadiliko ya viongozi, mimi huwa sina wasiwasi wala kuwaza ninakuwa busy na mambo yangu, maana najua Rais hawezi kugusa Mkoa wa Simiyu.
“Hawezi kugusa kwa sababu anajua Simiyu tuko vizuri, angalieni mara nne anafanya mabadiliko lakini wote bado tupo tangu atuteue maana anajua tunachapa kazi, tunashirikiana na tunatatua changamoto za wananchi,” alisema.
Butiku anena.
Awali akizungumza katika mhahalo huo Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku aliwataka viongozi kumuenzi Mwalimu nyerere katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Butiku alisema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ni kiongozi wa mfano kutokana na utendaji kazi wake, ikiwa ni pamoja na kutambua thamani ya kiongozi kwa wananchi.
Butiku alisema viongozi wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kubishana katika masuala ambayo hayana msingi wala kuliletea taifa maendeleo na kuwataka kubadilika.
“Tuache kubishana katika masuala ambayo hayana maana, tuwahudumie wananchi, Rais wetu amekuwa mkali kila siku, si kuwa ni mkali, bali anawataka viongozi muwatumikie wananchi wake. |
“Madaraka mliyopewa myatumie kwa faida ya watu, msibaki huku juu mkaacha kwenda kwa wananchi, mkibaki juu mtashindwa kuwasaidia wananchi kutoka kwenye umaskini,” alisema Butiku.
Mwisho….