20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Shamrashamra ya waandamanaji Algeria yaweza isidumu

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA

AKIONA maji yamemzidi kimo baada ya maandamano makubwa ya mitaani, Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika aliye madarakani kwa miaka 20 sasa, alitengua uamuzi wake wa awali chukizo la vijana wengi wa kuwania urais kwa muhula wa tano.

Lakini pia akaahirisha Uchaguzi Mkuu uliokuwa ufanyike Aprili 18, kwa ahadi ya kufanya kwanza mageuzi kadhaa katika mfumo wa kisiasa na Katiba ya Algeria.

Bouteflika alidai kufikia uamuzi huo ili kufanya marekebisho katika serikali yake haraka iwezekanavyo na kwamba mabadiliko hayo yanatokana na madai ya wananchi hao wa Algeria.

Kupitia ujumbe aliomtuma msaidizi wake, alibainisha kuwa ataunda jopo, ambalo litapanga tarehe mpya ya uchaguzi.

Honi za magari zilisikika barabarani kwenye maeneo ya katikati ya miji, huku baadhi wakipepereusha bendera za taifa hilo kushangilia kile wanachokiona ushindi.

Taarifa zinaeleza kuwa polisi hawakuonekana mitaani wakati wa shamrashamra hizo, wakidai kuelewa hisia za watu na kuwa wapo pamoja nao.

Kiongozi huyo amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipougua kiharusi mwaka 2013 huku akitembelea kiti cha magurudumu.

Hivyo, mbali ya kudumu muda mrefu, udhaifu wa afya yake, kukosa uwezo wa kuongoza, waandamanaji kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia matatizo ya rushwa pamoja na sera mbaya za kiusalama.

Walifahamu fika uwapo wa Bouteflika kwa muktadha wa afya yake, anavyotumika kwa maslahi ya kundi la wateule wachache kamwe hawezi kuondoa matatizo hayo.

Ilikuwa ngumu kwao kuelewa ni kwa vipi rais wao mwenye miaka 82, mgonjwa na anayepata shida kutembea au kuzungumza anaweza kuongoza nchi.

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika

Hakuna aliyeamini ilipotangazwa kuwa Bouteflika anawania awamu ya tano, hata mwenyewe hakujitokeza binafsi siku ya mwisho ya kujiandikisha kuwania urais.

Walimu, wanafunzi, wanasheria hata waandishi wa habari waliingia mitaani kuandamana wakiwa na hasira, walionekana kutokubaliana na hatua ya kuongozwa na mtu ambaye haonekani.

Wengi walikuwa na hofu kuwa kutopatikana kwa mrithi wa Rais Bouteflika, ambaye aliingia madarakani mwaka 1999, kunaweza kusababisha hali ya usalama kuyumba nchini humo.

Kwa mara ya mwisho alionekana akihutubia umma mwaka 2014, hotuba ya shukrani kwa raia wa Algeria kwa kuuamini utawala wake baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka huo.

Safari hii kabla ya kubanwa kutengua uamuzi wake, alikuwa ameahidi kutodumu kwa muhula wote na ahadi ya kutekeleza suala la mgawanyo wa madaraka, kuupa nguvu upinzani na kuhakikisha haki za raia zinafuatwa.

Baadhi waliona kuwa hii ni ishara ya mabadiliko ya sera katika uongozi, lakini hakuwa na ushahidi wa namna yatakavyoendeshwa kutokana na kutoonekana kwake kwa muda mrefu.

Raia wa nchi hiyo wamekua wakibahatika kumuona mara chache kwenye televisheni akisalimiana na ujumbe kutoka nchi za kigeni unaofika nchini Algeria.

Au kumuona kwenye ufunguzi wa mkutano mwaka 2016, akionekana amekaa kwenye kiti cha magurudumu, akionekana dhaifu, mchovu lakini akiwa katika tahadhari

Mpaka mwaka 2018, ikawa wazi kuwa Chama chake kimempendekeza kuwania tena uchaguzi wa mwaka huu.

Akaonekana kwenye ufunguzi wa msikiti na vituo vya treni za umeme katika mji mkuu wa Algiers.

Wiki chache baadae alikua kwenye ziara kutazama ujenzi wa msikiti mkubwa wa tatu duniani uliogharimu dola za Marekani bilioni mbili.

Wachambuzi wa siasa za nchini Algeria wanaona kuwa vijana wenye nguvu wananyang’anywa nguvu zao za uongozi na wazee. Lakini pia wa wanaona nchi imekabidhiwa mgombea ambaye ‘yu karibu kufa’.

Licha ya kushangilia batilisho la uamuzi wake huo, ambao ni kama ushindi kwa Waaligeria wengi, bado raia hao wanaotamani mabadiliko kuna uwezekano mkubwa wasipate kile wanachotaka.

Kundi hili la wateule wachache linalomzunguka Kiongozi huyo mkongwe linalohusisha wanasiasa na wafanyabiashara tajiri vigogo, maofisa wa usalama, ambao wamenufaika sana na utawala wake huu wa miaka 20 pamoja na udhaifu wa kambi ya upinzani ni kikwazo kikubwa cha kufanikiwa kwa hizo ndoto zao.

Si kama hakuna mtu mwingine licha ya tatizo la Bouteflika la kukwamisha wengine kupanda chati ya uongozi. Bali kundi hili teule lilimtaka mtu yule yule, ambaye katika udhaifu wake wa kimwili. Kiafya na kiakili ni fursa kwao kupora utajiri kirahisi.

Angalia katika uchaguzi wa mwisho 2014 licha ya udhaifu wa kiafya aligombea na kushinda huku katika kampeni shemu kubwa kilichokuwepo  kikiwa kivuli chake tu. Ni moja ya vichekesho katika siasa za ulimwengu huu hususani Afrika!.

Lakini ukubwa wa maandamano, ambayo hayakupata kuonekana tangu kumalizika kwa vita ile ya 2001, ilibidi vigogo hao wasalimu amri kwa kumruhusu mtu wao abatilishe uamuzi wa kuendelea kuongoza.

Hawakuwa wajinga, walifahamu fika kumng’ang’ania mzee wa watu kutaivuruga nchi na kubomoa ustawi wao waliouchuma vilivyo kifisadi katika miongo hiyo miwili.

Lakini pia walicheza vyema, kuhakikisha anachomeka katika tangazo lake hilo kipengele chake cha kusogeza uchaguzi huo. Kwanini?

Mwisho wa utawala wa Rais Bouteflika, kunamaanisha pia mwisho wa mbinu zake za kutawala pamoja na nguvu za wateule hao.

Hivyo katika tangazo lake la kubatilisha uamuzi wa kutogombea tena kulikuwa kama tulivyoona vitu viwili muhimu kwa raia wa taifa lake: kwamba hatowania urais katika uchaguzi mkuu ujao na ; kwamba hatofanya uchaguzi kwa sasa ili kuandaa mageuzi kwanza.

La kwanza lililenga kuwafurahisha Waaligeria na la pili kwa ajili ya wateule hawa katika kile kinachoonekana kutoa muda wa kupanga safu mpya ya uongozi wanaoitaka bila yeye, ukizingatia pia upinzani ni dhaifu na hivyo hauna nafasi katika kushinda uchaguzi.

Kwa sababu hiyo ni makosa kwa wanaohesabu tangazo la rais kama fanikio lingine la upepo wa mabadiliko katika mataifa ya Kiarabu, miaka minane baada ya kuibuka kwa kuanzia nchini Tunisia.

Hatua hiyo inaacha maswali machache yasiyojibiwa, ambayo yana uwezekano mkubwa wa kuendeleza maandamano kama yanayoonekana sasa.

Milio ya honi, kupeperusha bendera na kuimba mitaani itachukuliwa muda si mrefu na wimbi jipya la maandamano ya mitaani, ambayo umma utashinikiza kufahamu uchaguzi mkuu ujao lini utafanyika na iwapo ni mipango ya Bouteflika kuchukua fursa ya kipindi chote hiki kizima kabla ya kura, lengo ni kubakia rais.

Bouteflika aliahidi kufanya mjadala wa kitaifa kuhusu kubadili katiba na kuendesha mageuzi ya kiuchumi yatakayotoa ajira zaidi na kupunguza hali ya ukosefu wa usawa.

Lakin pia kuna wasiwasi kuahirisha chaguzi kutaipeleka Algeria katika kipindi cha mkwamo wa kiuchumi na kuimarisha nguvu ya kundi teule la vigogo wasotaka mabadiliko.

Vigogo hawa tayari wameanza tayari kuhakikisha rais yeyote ajaye atalinda hadhi walizofurahia kwa miaka 20, ambayo Bouteflika alikuwa madarakani.

Kadiri Bouteflika anavyobakia madarakani, vigogo hawa wa kisiasa, ambao wamejikita katika chama tawala cha National Liberation Front, pamoja na wale wa kibiashara walio karibu na rais – wanaweza pia kubainisha aina ya mageuzi wanayoweza kukubaliana nayo na kuumba mabadiliko ya katiba.

Hiyo ndiyo maana ya swali kuu la iwapo mwisho wa utawala wa Bouteflika utamaanisha pia kukoma kwa mbinu zake za uongozi na nguvu ya kundi hilo?

Au utakuwa mfumo ule ule uliozoeleka ukiondoa tu badiliko la mtu mmoja aliye kilingeni?

Sehemu ya jibu la swali hilo inategemeana na  jeshi, ambalo kwa kawaida limekuwa likiamua nani na namna ya kuiongoza nchi hiyo.

Kwa miaka mingi, uhusiano baina ya Bouteflika na makamanda wa jeshi uliumbwa kwa ushirikiano lakini pia shuku, kutoaminiana na vitisho.

Bouteflika ana mafaili ya taarifa mbaya za wakuu wa jeshi la usalama, wengi wao wakiwa wale walioshiriki kwenye vita katili ya kudai uhuru dhidi ya Ufaransa.

Kufichua siri hizi kungesababisha kelele za umma na shinikizo la kutaka kufunguliwa kwa mashitaka ya uhalifu wa kivita dhidi yao.

Wengine wangeweza kushitakiwa kwa matendo ya kihalifu yaliyotendeka wakati wa vita ile ya wenyewe kwa wenyewe iliyoibuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1991, ambao jeshi uliufuta baada ya kilichokuwa chama cha kidini cha Islamic Salvation Front (FIS) kuelekea kushinda.

Lakini vigogo wa kijeshi na kifedha pia wana siri za kutosha kumhusu Boutflika, ambaye aliikimbia nchi baada ya kushukiwa ufisadi mkubwa na kurudi baada ya miaka 16 ya kuishi mafichoni Uswisi.

Na ndio maana haikuwa ajabu lilimuona ni mtu sahihi wa kumweka madarakani, likimpa kila aina ya msaada uliorejesha utulivu katika taifa hilo kufuatia ile vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa minajiri ya wao kuruhusiwa kuchuma pia na kulindiwa uchafu wao.

Huku kukiwa na upinzani wa kiraia, jeshi linafahamu kuwa matumizi makubwa ya nguvu yanaweza kusababisha machafuko makubwa kwa taifa, ambayo yatakuwa kazi kuponya makovu.

Ni wazi kuna uwiano dhaifu wa madaraka baina ya jeshi na vigogo wa kisiasa na kifedha kwa upande mmoja na wananchi walio nyuma ya vuguvugu la upinzani kwa pande mwingine. Kusawazisha uwiano huo, kunahitaji pande zote kufikia maelewano yatakayoruhusu kila upende kutangaza ushindi.

Wakati vigogo hao, wakiwa hawako tayari kupoteza maslahi yao, ria pia wanachotaka ni kutimizwa kwa matakwa yao vinginevyo hakieleweki.

Algeria ina faida kiasi ambayo Misri, Tunisia na pengine Libya na Yemen hazikuwa nazo.

Hata kama ni dhaifu kuna vyama vya upinzani wenye uongozi wa kueleweka badala ya tu wapo vuguvugu za vijana wasiojulikana kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Kiarabu.

Mfumo huo unatoa fursa ya kuwapo msukumo wa hatua za kisiasa zenye kueleweka.

Iwapo utawala utatangaza tarehe za uchaguzi mapema, vuguvugu hizi zitatoweka haraka kwa vile zitakuwa zimemaliza kazi kwa kuwaachia wanasiasa.

Lakini kadiri uchaguzi unavyocheleweshwa, ndivyo uwezekano kwa makundi yenye itikadi kali za kidini kuibuka na vuguvugu hizi za upinzani, zikitumia fursa za ombwe hilo kusukuma ajenda na itikadi zao.

Mwenendo huo unaweza pia kutambua msimamo wa jeshi kuelekea maandamano na upinzani na migomo.

Wakati vyombo vya usalama vikiwa vimeuchukulia upinzani  unaendelea hadi sasa ‘poa’, vimefikia hatua ya kutangaza jeshi na umma vinaoana katika hatima ya nchi – hilo linaweza kubadilika baadaye.

Iwapo maadamano yatafanyika kwa mirengo ya kiitikadi, jeshi linaweza kuasili njia ya kikatili zaidi ambayo itachochea machafuko na makabiliano makubwa.

Hali ya sasa inategemeana na vitendo vya Bouteflika, ambaye ni mzee na mgonjwa na washauri wake wa karibu.

Bouteflika (82) hakuwa mfano mzuri wa kiongozi mkubwa wa kidemokrasia; aliwategemea maofisa wasio wa kuchaguliwa na jeshi na kukwamisha muibuko wa viongozi imara ndani ya chama chake.

Lakini pia moja ya heshima mbali ya kufanikiwa kuinua uchumi baada ya vita, alikuwa kiongozi ambaye aliweza kuhitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, ambayo watu 200,000 waliuawa na kuongoza juhudi za maridhiano.

Vita hiyo ilitokana na uamuzi kama tulivyoona wa jeshi kuamua nani ashinde, kuufuta uchaguzi huo wa 1991 na kuibua kundi la wanamgambo wa msituni wa FIS waliopambana na Serikali kwa miaka kadhaa na kuibua kundi lingine la itikadi kali la GIA.

Hata hivyo, kwa machinjo yaliyoshuhudiwa FIS ilipoteza uungwaji mkono, kabla ya kufikia makubaliano na Serikali na baadaye kugeukiwa na GIA, ambalo lilitoweka baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles