29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaka: Ni aibu Tanzania kuagiza lishe Marekani

Derick Milton -Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema ni aibu kwa Tanzania kuendelea kuagiza vyakula vya lishe kwa ajili ya watoto wenye matatizo utapiamlo kutoka nchini Marekani.

Alisema Tanzania siyo nchi ya kuagiza vyakula hivyo kutoka Marekani, kwani kuna kila kitu kama ardhi nzuri yenye rutuba, maabara za kupima vyakula hivyo pamoja na vyakula vyenyewe.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo jana  wakati akipokea vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 92 kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya lishe vilivyotolewa na shirika la USAID kupitia mradi wa boresha afya.

Aliongeza kuwa mbali na  uwezo wa kuzalisha vyakula hivyo, Tanzania ina Chuo Kikuu Cha Kilimo Sokoine (SUA) chenye watalaamu wa kutosha, maabara kutoka TMDA na TBS ambao wanaweza kutengeneza hivyo vyakula hapa nchini.

“Kama leo Marekani wakisema hawatengezi tena hivyo vyakula lishe? Kwa hiyo watoto wetu watanzania wenye utapiamlo watakufa? Kwa kukosa hivyo vyakula tunavyoviagiza Marekani?’’ Alihoji Mtaka.

“Hii inashangaza sana wakati tunao maafisa lishe pamoja na Wizara ya Afya, ambako wapo watalamu wanafahamu vitu gani vinahitajika na hapa nchini vinapatikana kwa wingi lakini wameshindwa kuanzisha hata mradi mdogo wa kutengeza vyakula hivyo’’ Alishangaa  Mtaka.

Alisema maofisa lishe pamoja na wizara wanatakiwa kutumia nafasi hii kama fursa kwao kwa kuanzisha mradi wa kuzalisha vyakula hivyo ndani ya nchi kwa kuwa mahitaji ni makubwa.

Aidha alisema kuwa ikiwa kitaanzishwa kiwanda cha kuzalisha vyakula hivyo, kitakuza uchumi wa nchi pamoja na kupunguza tatizo la utapiamlo kwa kiwango kikubwa.

Awali akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu huyo wa Mkoa mratibu wa mradi huo mkoa wa Simiyu na Shinyanga, Dk. Hellen Mwaifwani alisema vifaa hivyo vimetolewa ili kusaidia uboreshaji wa huduma za lishe.

Dk. Hellen alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya Mkoa mzima zaidi ya 200, ambapo vitasaidia pia kuboresha taarifa za lishe mkoa.

“Huko nyuma ilionekana mkoa unakuwa na taarifa ambazo siyo sahihi za lishe kutokana na kutokuwa na vifaa hivyo kwa kiasi kikubwa, hali ambayo imeufanya mkoa kuwa wa mwisho kila wanapowasilisha taarifa za lishe kwenye vikao vya kitaifa,’’ alisema Dk. Mwaifwani.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Shirika hilo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, waliona umuhimu wa kusaidia vifaa hivyo ambavyo wanaamini Mkoa wa Simiyu utafanya vizuri kwenye lishe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles