27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif kitanzini kugombea urais Zanzibar

GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

MWAKILISHI wa Jimbo la Shaurimoyo (CCM) Hamza Hassan Juma amewasilisha hoja binafsi  katika Baraza la Wawakilishi itakayowabana wanachama wapya kupewa nafasi ya kuwania  nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo urais.

Hoja hiyo ambayo iliwasilishwa jana mbali na urais pia inaweka kikwazo kwa wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani  kuwania nafasi hizo kabla ya kutimiza miaka miwili ya uwanachama katika chama chochote.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Hamza na katika mahojiano yake na gazeti hili amedai kuwa endapo hoja yake hiyo itajadiliwa na kupitishwa  katika baraza hilo itapunguza pia utapeli wa kisiasa unaofanywa na baadhi ya wanasiasa wa kuhamahama vyama.

Taarifa za kupelekwa kwa hoja hiyo binafsi, imezua mijadala katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku baadhi ya wadau wa mambo ya siasa wakidhani kuwa ni ajenda ya chama tawala kutaka kuwabana wapinzani visiwani humo.

Ikumbukwe ni hivi karibuni tu aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharrif  Hamad alikihama chama hicho sambamba kundi kubwa wa wafuasi wa chama hicho na kuhamia chama cha ACT Wazalendo.

Inahofiwa kuwa endapo hoja hiyo binafsi ya Mwakilishi wa Shaurimoyo itajadiliwa na kupitishwa na wajumbe itakiathiri kwa kiasi kikubwa chama cha ACT Wazalendo ambacho kilijizolea wanasiasa wakongwe katika siasa za Zanzibar.

Wanachama hao ndio wanaoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuleta upinzani mkali dhidi ya CCM katika kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka huu visiwani humo na hata kupewa nafasi kubwa ya ama kuchukua nafasi hiyo au kushiriki kwenye  Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumamosi Hamza alisema kuwa hoja hiyo haitawabana wanasiasa wa upinzani tu bali hata wale waliokuwa katika chama tawala.

Alisema amepeleka hoja hiyo binafsi wa Spika wa Baraza la Wawakilishi amefuata utaratibu wote unaotakiwa ukiwemo kukitaarifu chama chake cha CCM.

“Hii ni haki yangu kikatiba, kisheria na kikanuni kama mwakilishi ninaruhusiwa kupeleka hoja binafsi ninayoona inafaa katika Baraza la Wawakilishi.

“Kwa sasa kumekuwa na tabia ya watu kupewa nafasi ya kuwania uongozi kupitia vyama ambavyo hawajavitumikia, hawajui misingi yake wala sera za chama hicho”, alisema.

Aliongeza kusema, “Jumuiya ya Umoja wa Vijana katika chama chochote imewekwa kwa ajili ya kuwatengeneza kuwa viongozi wa baadae, lakini sasa kutokana na utapeli na tamaa za baadhi ya wanasiasa inafanya vijana hao kukosa nafasi wanazostahili”.

Alisema katika miaka ya karibuni CCM imefanikiwa kupata wanachama wengi waliovihama vyama vyao na wengine walikuwa wabunge na madiwani ambao walipata tena nafasi ya kugombea tena nafasi hizo lakini endapo kungekuwa na masharti ya  ya kuwataka kutimiza miaka miwili wasingeweza kukubali kuhama.

“Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walilalamika, kuwa CCM inawanunua wanachama hao ambao nao kwa upande wao hawakuwa na shaka wala hofu kwa kuwa walikuwa wanapewa nafasi ya kugombea tena nafasi zao,”alisema Hamza.

Alisema  endapo kutakuwa na masharti kama hayo hakutakuwa na mtu wa kukubali kuhama chama na hivyo kupunguza chaguzi ndogo za mara kwa mara.

“Mbowe (Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema) na Zitto Kabwe (Kiongozi wa ACT-Wazalendo) walilamika sana sasa sisi tunawasaidia pia na wao katika hili kwani endapo itaendelea hivi unaweza kushangaa hata baada ya uchaguzi ujao mtu anahama tu baada ya mwaka hali ambayo inaongeza gharama zisizokuwa na sababu kwa Serikali” alisisitiza Hamza.

Hamza alisema kwamba ameshapeleka hoja yake hiyo kwa Spika na anachosubiri kwa sasa ni lini Spika ataiweka kwenye ratiba.

“Tayari imeshafika kwa spika na ninachosubiri ni maamuzi ya Spika yeye ndiye atajua ratiba, endapo muda utaruhusu kwa vikao hivi au vikao vijavyo”alisema Hamza.

Uchaguzi katika visiwa vya Zanzibar unatarajiwa kuwa wa moto kutokana kwamba katika Uchaguzi mkuu huu Wazanzibar watachagua Rais atakayemrithi Dk. Mohamed Shein ambaye anamaliza vipindi vyake viwili baada ya kuiongoza Zanzibar kwa miaka 10.

Pia vuguvugu la uchaguzi ni kubwa  baada ya mabadiliko makubwa yaliyotokewa katika chama kikuu cha upinzani kisiwani humo cha CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles