25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaka apiga marufuku wakopeshaji kushikilia kadi za benki za walimu

Derick Milton – Itilima

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, amepiga marufuku taasisi ndogo za kifedha ambazo huwakopesha watumishi wa umma wakiwemo walimu, kuacha utaratibu wa kushikilia kadi zao za benki (ATM) kama dhamana pindi wanapowakopesha.

Mtaka alisema taasisi yoyote ambayo itabainika au kukutwa na kadi hizo, haitaruhusiwa tena kufanya kazi hiyo ndani ya mkoa wake.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Wilaya ya Itilima waliofanya vizuri mitihani ya kitaifa mwaka jana.

Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Lagangabilili, aliwataka wamiliki wa taasisi hizo kuacha mara moja utaratibu huo kwani utawagharimu.

Alieleza kuwa taasisi hizo zimekuwa zikiwapatia mikopo watumishi, wengi wao wakiwa walimu, hasa kutoka Wilaya ya Itilima, huku sharti likiwa kuweka rehani kadi zao za benki (ATM) na nywila (Password).

“Ni marufuku kwa taasisi yoyote ya pesa ambayo imemkopesha mwalimu, kukutwa na kadi ya benki ya mwalimu aliyepewa mkopo, tukikubaini au kukukuta na kadi hizo, hatua kali tutazichukua ikiwa pamoja na kukufukuza kufanya kazi Simiyu,” alisema Mtaka.

Aidha aliwataka walimu kutumia elimu waliyonayo kuacha tabia ya kuacha nywila pamoja na kadi zao za benki kwenye taasisi hizo, huku akiwataka kuchukua mikopo kwa malengo kwani wengi wao wameweza kukimbia madeni.

Mtaka alisikitishwa na vitendo vya walimu mkoani humo, kuendelea kudanganywa na watu ambao hawajasoma kwa kutakiwa kuacha kadi hizo ikiwa pamoja na kutapeliwa pesa zao.

“Ofisini kwangu kuna kesi zaidi ya 40 ambazo walimu wa kike wamewakopea wapenzi wao pesa, kisha kuachwa ambapo wapenzi wao hao wanakimbilia kusikojulikana, hili jambo ni aibu sana kwa walimu ambao wamesoma,” alisema Mtaka.

Mbali na hilo, alisema kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakiweka rehani vyeti vyao vya elimu ili waweze kukopesheka kwenye taasisi hizo ndogo za kifedha, ambapo aliwataka kuacha tabia hiyo.

Awali akiongea kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itilima, Elzabert Gumbo alisema kuwa kumekuwepo na wimbi kubwa la walimu wa kike kuomba uhamisho.

Gumbo alimwomba Mtaka kuwasaidia katika kupambana na jambo hilo, kwani wilaya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, hasa wa kike huku akibainisha wilaya hiyo kuendelea kufanya vizuri kweye mitihani hiyo.

Naye Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga alisema kuwa ofisi yake imeweka mikakati kuhakikisha kila shule ya sekondari wilayani humo inajengewa bweni kwa watoto wa kike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles