Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MTAALAMU wa lishe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mariam Nyamwaira, amesema uji wa ulezi si mzuri kwa afya na ukuaji wa mtoto.
Akizungumza na MTANZANIA jana hospitalini hapo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Lishe, Nyamwaira alisema watoto wengi wanaolishwa uji huo wa ulezi wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali ambayo huathiri ukuaji wao.
Aliyataja matatizo hayo kuwa ni kupata choo kigumu na wakati mwingine kupata mzio (allege) na hivyo kuathiri maendeleo ya afya zao.
“Wazazi na walezi wengi hudhani uji wa lishe lazima utengenezwe kwa kuchanganya nafaka nyingi jambo ambalo si sahihi. Unakuta uji umetengenezwa kwa kutumia mahindi, mtama, soya, maharagwe, karanga na ulezi kwa wakati mmoja.
“Uji uliowekwa vitu vingi namna hiyo si mzuri kwa lishe ya mtoto, hapa Muhimbili katika kliniki yetu tunapokea watoto hawana afya nzuri licha ya kwamba kila siku wanalishwa uji wa ulezi,” alisema.
Alisema wamekuwa wakitoa elimu hiyo kwa wazazi wanaokwenda katika kliniki yao kupunguza au kuachana na matumizi ya nafaka hiyo.
“Ulezi una ‘complication’ nyingi, kwanza si rahisi kupatikana sokoni kama ilivyo kwa mahindi na nafaka nyinginezo na kama nilivyoeleza hapo awali, husababisha mtoto kupata choo kigumu na hata mzio,” alisema.
Alisema ni vema uji wa mtoto ukatengenezwa kwa kutumia nafaka chache kuliko kuzichanganya zote kwa wakati mmoja.
“Uji wa lishe si lazima utengenezwe kwa kuchanganya nafaka nyingi kwa wakati mmoja, tena ni vizuri zaidi ukatengeneza uji wa dona ukachanganya na karanga ambazo na zenyewe ziwe zimesagwa pembeni.
“Ukisaga mahindi na karanga kwa wakati mmoja unga wako ni rahisi kuharibika na kupoteza virutubisho, kwa kawaida karanga huota, nawashauri msage mahindi peke yake na karanga peke yake, hii itasaidia kila nafaka kuiva kwa wakati sahihi na mtoto atapata virutubisho vyote,” alisema.
Aliongeza: “Ukitaka kuamini uji wa dona ni mzuri, mtazame mtoto anayelishwa uji wa ulezi na yule anayelishwa uji wa dona, utaona tofauti yao kiafya. Yule anayelishwa uji wa dona utaona afya yake ni nzuri ikilinganishwa na yule anayelishwa uji wa ulezi,” alisema.
Alisema iwapo wazazi watatengeneza uji wa lishe kwa kutumia nafaka chache, itasaidia pia mtoto kupata hamu ya kula.