27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MSUVA MTU MBAYA, MSUVA MASHINE

Na THERESIA GASPAR-Dar es Salaam

 

WINGA Simon Msuva amethibitisha kuwa yeye ni mchezaji wa kulipwa, baada ya jana kufunga mabao mawili yaliyoiwezesha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana, katika mchezo wa kalenda ya Fifa uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Msuva, ambaye kwa sasa anaichezea Difaa Al Jadid, inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, aliiandikia Stars bao la kuongoza dakika ya tano ya kipindi cha kwanza, baada ya kugongeana vema na Mzamiru Yasini, kabla ya kufunga la pili dakika ya 61, akipokea pande la Shiza Kichuya.

Katika mchezo huo, Stars  ilionekana mapema kupania kuibuka na ushindi, baada ya kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Botswana, yaliyosaidia kuandika bao kupitia kwa Msuva

Baada ya bao hilo, Botswana ilirejea mchezoni na kufanya shambulizi kwenye lango la Stars, ambapo dakika ya 17, Lopang Mosige aliachia mkwaju akiwa nje ya 18, lakini hata hivyo, ulipaa juu ya lango

Stars ilikaribia kupata bao la pili dakika ya 23, wakati Kichuya alipowalamba chenga mabeki wa Botswana, lakini akapiga shuti hafifu lililotua mikononi mwa kipa wa Botswana, Mwampule Masule.

Dakika ya 37 kipa wa Stars, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada baada ya kupangua kiki kali ya Ontireste Ramathakwana.

Kipindi cha pili Botswana iliongeza mashambulizi langoni mwa Stars kwa lengo la kutaka kusawazisha bao, ambapo dakika ya 51 kiki ya Segolame Boy ilipanguliwa na Manula.

Dakika ya 56, mwamuzi Elly Sasii alimwonyesha kadi ya njano Mathumo Simisani, baada ya kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Stars,  Mbwana Samatta.

Dakika ya 57 Samatta aligongesha mwamba wa Botswana, baada ya kuachia kiki akiwa nje ya 18.

Kocha wa Stars, Salum Mayanga, alifanya mabadiliko dakika ya 58 kwa kumtoa nje Mzamiru Yassin na kumwingiza Raphael Daud, huku Botswana akitoka Segolame Boy na nafasi yake kuchukulia na Tumisang Orebonye.

Msuva aliwaamsha tena mashabiki wa Tanzania baada ya kuifungia Stars bao la pili dakika ya 61, akipata pande la Kichuya

Dakika ya 62, Mosha Gaolaolwe alioneshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi beki wa Stars, Gadiel Michael

Mayanga alifanya mabadiliko mengine dakika ya 65, ambapo alimtoka Kichuya na kumwingiza Farid Mussa.

Dakika ya 70, Botswana ilifanya mabadiliko mengine, ambapo alitoka Ditshup Maano na kuingia Katlego Masole.

Dakika ya 71 Katlego Masole alijaribu kumtungua kipa wa Stars, Manula, lakini kiki yake ilipaa.

Botswana ilifanya mabadiliko zaidi ambapo alitoka Mosha Gaolaolwe na kuingia Jackson Lesole, Edwin Olerile na kuingia Lesenya Ramoraka.

Ili kuhakikisha analinda ushindi, Stars nayo ilifanya mabadiliko ambapo dakika ya 81, Hamis Abdallah alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na  Said Ndemla, Emmanuel Martin aliingia kuchukua nafasi ya  Msuva, pia Elias Maguli akichukua nafasi ya Samatta.

Mabadiliko hayo hata hivyo hayakubadili matokeo, kwani mpaka dakika 90 zinamalizika, Stars ilichomoza kwa ushindi wa mabao 2-0

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mayanga alisema bao la mapema walilopata katika mchezo huo ilikuwa chachu ya ushindi wa kikosi chake.

Naye kocha wa Botswana, David Bright, aliwasifu wachezaji wake kwakusema walicheza vizuri, licha ya kupoteza mchezo huo.

Vikosi: Taifa Stars: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Nyondani, Saimon Msuva, Himid Mao, Hamis Abdallah, Mzamiru Yassin, Mbwana Samatta na Shiza Kichuya.

Botswana: Mwampule Masule, Mosha Gaolaolwe, Edwin Olerile, Simisani Mathumo, Lopang  Mosige, Alphonce  Modisaotsile, Maano Ditshupo, Gift Moyo, Segolame Boy, Kabelo Seakanyeng na Ontiereste Ramatlahakwana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles