25.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

‘MSTARI MWEKUNDU’ KUPIGWA LEO UHAKIKI MALI ZA VIGOGO

Maofisa wakiwasili katika ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Dar es Salaam jana kuwasilisha fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni. PICHA SILVAN KIWALE

 

NA GRACE SHITUNDU - DAR ES SALAAM

WAKATI urejeshwaji wa fomu za tamko la rasilimali na madeni katika ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma linatarajia kufungwa leo, viongozi mbalimbali wameendelea kupigana vikumbo kuwahi kabla ya milango ya ofisi hiyo haijafungwa.

Urejeshwaji wa fomu hizo umechukuliwa kwa umakini baada Rais Dk. John Magufuli kurudisha fomu zake na kuitaka sekretarieti hiyo kutopokea fomu za yeyote atakayeshindwa kuzipeleka baada ya leo ambayo ndiyo siku ya mwisho na anataka aone sheria itafanyaje.

Pia Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Harold Nsekela, aliviambia vyombo vya habari jana kuwa viongozi waliokuwa hawajarudisha fomu zao wamepata nafasi kwa siku za Jumamosi (jana) na Jumapili (leo) ili kukamilisha kabla ya muda kumalizika leo saa 10 jioni.

“Viongozi ambao hawajarudisha fomu wamepata nafasi ya leo (jana) na kesho (leo), hivyo tunafungua ofisi zetu muda wa kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni, sasa mtu akikosa hapo itakuwa ni yeye mwenyewe.

“Leo siwezi kuongea chochote kwa kuwa watu wanaendelea kurudisha, naweza kuzungumza kesho baada ya mchakato huu kukamilika na Januari 2, mwakani ndiyo tunaweza kujua nani kawasilisha na nani hajawasilisha,” alisema.

Jaji Nsekela alisema leo ndiyo siku ya mwisho kwa viongozi kurejesha fomu hizo na baada ya hapo adhabu mbalimbali zinaweza kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria dhidi ya wale wasiozirejesha.

Alisema ofisi za makao makuu zitaendelea kuwa wazi pamoja na ofisi za Kanda ya Kati Dodoma, Kanda ya Ziwa Mwanza, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya, Kanda ya Kusini Mtwara, Kanda ya Magharibi Tabora, Kanda ya Kaskazini Arusha na Kanda ya Mashariki Kibaha kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 10 jioni.

MTANZANIA Jumapili jana liliendelea kupiga kambi katika ofisi za sekretarieti hiyo zilizopo eneo la Posta Mpya, Dar es Salaam katika Jengo la Sukari House na kushuhudia vigogo wa Serikali wakimiminika kuzirejesha fomu zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi hao walishukuru kupatiwa nafasi hiyo kwa kuwa wengine walishindwa kurudisha kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali.

Meneja Kiongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dickson Awanga, alisema kuwasilisha kwa wakati ni vizuri zaidi kwa kuwa kunapunguza usumbufu ingawa amewasilisha wakati wa lala salama.

“Nilishindwa kurudisha mapema kutokana na majukumu mbalimbali ya kazi, lakini nashukuru kwa kupata nafasi hii nimeweza kukamilisha leo (jana),” alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa, Jonathan Mgaiwa, alisema miaka yote amekuwa akirudisha kwa wakati, lakini safari hii alishindwa kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kikazi nje ya mkoa.

“Nashukuru nimepata hii nafasi kwa sababu wasingeongeza siku na mimi ningekuwa katika hatari ya kutorudisha fomu,” alisema.

Pia alisema sekretarieti hiyo inawafanya watu wasiishi kwa kufichaficha mali zao ingawa watu wanatofautiana, wengine hawapendi kujulikana wanayofanya jambo ambalo kwa mtumishi wa umma si sahihi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Imalamakoye wilayani Urambo, Tabora, Emmanuel Segembe, alisema yeye yupo Dar es Salaam kwa matibabu, lakini amepata nafasi ya kurejesha fomu hizo baada ya ofisi hiyo kuongeza siku hizo mbili.

“Nimekuwa hapa kwa matibabu kwa muda mrefu, sasa agizo lililotolewa na Rais Magufuli hivi karibuni limenifanya nifanyie hapa hapa jijini kwa sababu ningesema nirudi Tabora ningechelewa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwakumbusha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu wote na viongozi wote walioko katika ngazi za uteuzi, wahakikishe wanatimiza takwa hilo ambalo liko kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.

Kwa mujibu wa kifungu cha 9 Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma ya mwaka 1995, sura ya 8 inawataka viongozi wote wa umma  kujaza fomu za kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma (Tamko la Rasilimali na Madeni) na fomu ya Ahadi ya Uadilifu mara wanapoteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Lengo la kujaza fomu hizo ni kuwa na uwajibikaji kwa kiongozi juu ya uadilifu wake wakati wote anapokuwa mtumishi wa umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles