MINNESOTA, MAREKANI
MBUNGE wa kwanza mwenye asili ya Somalia, Ilhan Omar, amechaguliwa kutoka katika Jimbo la Minnesota, nchini humo, eneo ambalo kuna idadi kubwa la raia wa Marekani wenye asili ya Somalia.
Mbunge huyo, mwenye umri wa miaka 33, ameingia katika historia ya nchi hiyo na kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo kutoka katika jamii ndogo ya Wasomali.
Ilhan, ambaye aliingia Marekani akiwa na miaka 8 kama mkimbizi akiwa na familia yake, amekuwa akifahamika sana kwa kutetea haki za binadamu, lakini pia wanawake na anafahamika sana kwa mtindo wake wa kuvaa hijab.
Hadi kuchaguliwa kwake, amekuwa akishirikiana na chama cha Democratic na kuingia kwake bungeni kumeleta matumaini kwa jamii ya Somalia ambao wamekuwa wakihisi kutopewa kipaumbele nchini humo.
Wakati wa kipindi cha kampeni, Donald Trump ambaye ameshinda urais aliwashutumu watu wenye asili ya Somalia kwa kuchangia ukosefu wa usalama katika jimbo hilo na kujiunga na makundi ya Islamic State.
Takwimu za mwaka 2010, zinaonesha kuwa jamii ya Wasomalia ina watu 25,000 nchini humo na hasa katika jimbo hilo la Minnesota.
Kuhusu ushindi wa Trump, mbunge huyo mpya amesema haifahamiki ni kitu gani kitafanyika na kuongeza kuwa huu ndio wakati wa jamii hiyo kuanza kujipanga upya.