22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Msikiti wa Mtambani waungua tena

Msikiti wa Mtambani ukiwaka moto
Msikiti wa Mtambani ukiwaka moto

NA EVANS MAGEGE, Dar es Salaam

MSIKITI wa Mtambani uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, jana uliungua kwa moto na kuteketeza chumba kimoja kinachotumiwa na wanafunzi wa sekondari kujisomea na kulala.

Tukio la kuungua kwa msikiti huo lilitokea muda mfupi kabla ya swala ya Ijumaa na tayari baadhi ya waumini walikwishaingia kwa ajili ya kuswali.

Akithibitisha kutokea tukio hilo, Katibu wa Msikiti huo, Sheikh Abdallah Mohamed Ali, alisema moto mkubwa ulizuka ghafla katika chumba ambacho huwa kinatumiwa na wanafunzi wa sekondari ambayo ipo ndani ya eneo la msikiti kwa ajili ya kujisomea na kulala.

Ali alisema ndani ya chumba hicho hapakuwa na mtu isipokuwa vifaa vinavyotumika kukifanyia ukarabati kwa kuweka mfumo mpya wa nyaya za umeme.

“Ilikuwa imebaki kama robo saa kuanza kwa swala ya Ijumaa ndipo ghafla ukatokea moshi mzito katika eneo la nyuma ulioambatana na moto mkali uliokuwa unaenea kwa kasi, wote tulishikwa na taharuki lakini kwa kuwa tulikuwa wengi tukaungana kwa pamoja kuudhibiti,” alisema Sheikh Ali.

Alisema msikiti huo umekatiwa umeme tangu tukio la awali la kuungua moto lilipotokea mwezi mmoja uliopita jambo  ambalo linaacha maswali yasiyokuwa na majibu kuhusu chanzo cha kuzuka kwa moto wa jana.

“Kwa kweli tukio hili linashangaza sana, hapa hakuna umeme kabisa sasa sijui moto huu umetokana na nini,” alisema.

Naye Imamu wa msikiti huo, Sheikh Suleiman Abdallah, alisema wakati moto huo unatokea yeye alikuwa ofisini mwake akiandaa hotuba.

“Siwezi kuzungumza lolote kwa sababu wakati moto unatokea nilikuwa ofisini kwangu naandaa hotuba kwa maana hiyo kilichofuata ni taharuki, hivyo sifahamu chanzo chake ni kipi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura ambaye alikuwapo eneo la tukio alisema moto huo ulianzia katika chumba kinachotumiwa na wanafunzi wa kike kujisomea.

Alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana hivyo uchunguzi unaendelea ili kubaini kilichosababisha ajali hiyo.

Kamanda Wambura alisema kuwa moto huo umeteketeza magodoro manne na vitu kadhaa vilivyokuwa vikitumiwa na wanafunzi hao.

“Wakati tukio likitokea wanafunzi hawakuwapo ndani ya chumba hicho na kwa maelezo ya awali niliyoyapata waliondoka tangu jana (juzi), pia jengo lote halina umeme hivyo uchunguzi wa kina unafanywa ili kubaini chanzo cha moto huo,” alisema Kamanda Wambura.

Agosti 13 mwaka huu tukio lingine la moto lilitokea katika msikiti huo na kuteketeza madarasa ya Shule ya Msingi Mtambani ambayo ipo katika majengo ya msikiti huo.

Moto huo ulianzia kuwaka katika eneo la mabweni ya wanafunzi wa shule hiyo.

Msikiti wa Mtambani ni moja ya misikiti maarufu jijini Dar es Salaam, umaarufu wa msikiti huyo unatokana na kutumiwa kama kituo cha wanaharakati wa Kiislamu tangu miaka ya 1990.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kama ingalikuwa nikanisa hili lililoungua basi ungalisikia Waislam washakamatwa na wale Masheikh wa Uwamsho waliobaki washakwenda kuchukuliwa na kupewa kesi ya Ugaidi. lakini madhali ni Msikiti hata ukiungua mara 100 utaambiwa Waislam wawe watulivu na uchunguzi unaendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles