Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iemuonya mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, kuhusu mawakili wake kujitoa katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Agosti 23 wakili aliyekuwa anamtetea Msigwa, Jeremiah Mtobesya alijitoa kwa madai yakutoridhishwa na mwenendo wa mahakama katika uendeshaji wa kesi hiyo na wiki iliyopita Novemba 8, wakili mwingine Jamhuri Johnson, alijitoa kwa sababu hizo hizo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Wilbard Mashauri ametoa siku tano kwa Msigwa kuhakikisha anapata wakili wa kumtetea katika kesi hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 23, mwaka huu.
Msigwa na viongozi wengine wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, wanashtakiwa kwa makosa tisa likiwamo la uchochezi na kuhamasisha mkusanyiko usio halali.