Na MOHAMED KASSARA, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIOAJI Mohamed Rashid amesema anaamini KMC ni mahali sahihi kwake kurudisha makali yake ya kucheka na nyavu kama alipokuwa na kikosi cha Tanzania Prisons msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Rashid amejiunga na KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, kwa mkopo wa miezi sita, akitokea Simba aliyojiunga msimu huu akitokea Prisons ya jijini Mbeya.
Kabla ya kutua, Simba, Rashid alikuwa kinara wa mabao katika kikosi cha Prisons aliyoifungia mabao 10 msimu uliopita na kuisadia kumaliza nafasi ya nne, nyuma ya Simba iliyoibuka bingwa , Azam FC iliyoshika nafasi ya pili na Yanga iliyomaliza ya tatu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Rashid alisema aanamini kutua katika timu hiyo kutafufua upya makali yake ya ufungaji mabao, kwakua huko anaamini atakuwa na nafasi ya kutosha ya kucheza tofauti na ilivyokuwa Simba.
“Nafurahi kocha Etienne Ndayiragije kuniamini na kuniita nifanye nae kazi, hii itakuwa fursa mpya kwangu kurudisha kiwango changu, nimejipanga kuhakikisha najitoa kwa uwezo wangu wote kuisadia timu ipate matokeo mazuri katika michezo yetu ijayo, nitashirikiana na wachezaji wenzangu kufanikisha hilo.
“Najua KMC ni timu nzuri, kuja hapa haimaniishi nitapata nafasi moja kwa moja, kuna Elias Maguli hapa, hivyo natakiwa kuongeza juhudi ili kupata nafasi ya kuanza, nataka kurudisha makali yangu, nafikiri itawezekana kwa kuwa bado kuna michezo mingi, alisema Rashid.