25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MRUHUSU MTOTO AISHI UTOTO WAKE

Na CHRISTIAN BWAYA


UNA mtoto asiyesikiliza unachomwambia. Unajaribu kumweleza nini anapaswa kufanya lakini haonekani kujali umesema nini. Tatizo liko wapi? Ufanye nini ili akusikilize?

Pamoja na sababu nyingine nyingi zinazoweza kupunguza usikivu wa mtoto, mara nyingi kutarajia watoto wafikiri na kutenda kama watu wazima inaweza kuwa sehemu ya tatizo. Ninatumia mfano wa Ben, mtoto wa miaka sita anayesoma darasa la kwanza.

Wazazi wake wanalalamika mtoto wao wa pekee, Benson ni mkorofi. Mbali na kutokusikiliza anachoambiwa na wazazi wake, wazazi wanafikiri  wakati mwingine Ben anavutiwa kufanya yale anayojua  yatawakasirisha wazazi wake. Niliwaomba ufafanuzi.

“Akirudi shule ni michezo muda wote. Hana muda wa kufanya kazi za shule hadi umkumbushe,” anaeleza mama Ben. Kwa nini anafikiri hili ni tatizo? “Natamani atulie ndani. Sipendi kuona mtoto anarukaruka muda wote.”

Inavyoonekana, mama Ben ana matarajio makubwa kwa mwanawe kuliko hali halisi. Kwa umri wake wa miaka sita, Ben anahitaji kucheza. Michezo ndio nyenzo kuu ya kujifunza. Kutarajia atulie nyumbani kama mtu mzima ni kumkuza kuzidi umri wake.

“Nakuelewa. Lakini  ugomvi wangu na yeye (Ben) ni kutokusikiliza. Ninatamani nikimwambia kitu afanye,” anafafanua mama Ben.

Ninachofikiri usikivu ni matokeo, mtoto husikiliza kirahisi unapomweleza jambo analoweza kulielewa. Hakikisha mtoto anaelewa vizuri kile unachotarajia akifanye.

Unajua kuna mambo sisi watu wazima hatupa shida kuyaelewa, ufahamu wetu unatosha kuchambua mantiki. Tunajua matokeo ya yale tunayoyafanya. Pia, tunajua nini kitatokea ikiwa hatutafanya yale tunayopaswa kuyafanya. Lakini, kwa mtoto mdogo kama Ben, inaweza kuwa vigumu kwake kuelewa kwa usahihi ule ule tunaouona sisi.

Kwa hiyo, jambo jema linaweza kuwa gumu kueleweka kwa mwanao kama hutatafuta namna nyepesi ya kumwelewesha. Kabla hujatarajia alifanye, tafuta namna rahisi ya kufafanua jambo lieleweke.

Lakini pia, wakati mwingine watoto wanakosa usikivu kwa sababu sisi wenyewe tumeshindwa kuwa wasikivu. Huwezi kusikilizwa na mtu anayejua kabisa kuwa humsikilizi. Kuna uwezekano Ben hasikilizi kwa sababu hajasikilizwa.

“Una maana gani unaposema simsikilizi?” anauliza mama Ben. Hapa nina maana ya kujenga mazoea ya kumshirikisha mtoto kwenye uamuzi unaomhusu kadiri inavyowezekana. Badala ya kumpa sheria anayotakiwa kuiheshimu ‘bila shurti’ fikiria kumshirikisha kutengeneza sheria husika.

Kwa mfano, badala ya kumtaarifu muda upi atatakiwa kutazama televisheni, mshirikishe kutengeneza utaratibu mzuri wa kuangalia televisheni kwa kuzingatia mtazamo wake. Pale unapoona mtazamo wake unaweza kuleta athari asizoziona, fanya jitihada kumsaidia kuelewa kwa nini unafikiri tofauti.

Ushirikishwaji wa namna hii una faida kuu mbili. Kwanza, unamfanya mtoto ajisikie mzazi wake anajali mahitaji na hisia zake. Binadamu bila kujali umri anahitaji kuthaminiwa. Ukimthamini anakuwa mwepesi kushirikiana na wewe.

Lakini pia, ushirikishwaji unapunguza upinzani usio wa lazima. Wakati mwingine ubishi anaoonesha mtoto ni ujumbe kuwa anafikiri hujatambua nafasi yake na pengine haelewi kwanini afanye unachomwelekeza kufanya.

“Kwahiyo, una maana mtoto hatakiwi kuwa mtii hata pale asipoelewa?” anauliza baba Ben. Sina maana hiyo. Tuwafundishe watoto kutambua mamlaka lakini tuelewe kuwa utii ni matokeo. Huwezi kwenda benki kuomba kuchukua kiasi cha fedha ambacho hujakiweka.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles