24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MPINA AGUSA JIPU MRADI WA MIKOKO RUFIJI

Na MWANDISHI WETU-RUFIJI 



NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, amebaini madudu katika matumizi ya Sh milioni 396 za ufadhili wa Mfuko wa nchi masikini zaidi duniani (LDCF), chini ya mkataba wa dunia mabadiliko ya tabianchi katika utekelezaji wa mradi wa upandaji na uendelezaji wa mikoko kwenye Delta ya Kaskazini Mto Rufiji.


Katika mradi huo zaidi ya Sh milioni 364 matumizi yake hayaridhishi kutokana na mchanganuo kwa vikundi kutoeleweka sawasawa.
Kutokana na utata huo, imebainika kuwa baadhi ya vikundi vinavyodaiwa kulipwa fedha hizo vimekana kulipwa huku ikidaiwa hakukuwa na mkataba bali walifanya kazi kama vibarua kwa posho ya Sh 10,000 kila wanapomaliza kazi  kwa kuwa hawakuwa na mkataba wa kazi hiyo.


Kutokana na hatua hiyo, Mpina amemwagiza Mkaguzi wa ndani Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwatano Maganga, kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja anafanya uhakiki wa matumizi ya fedha hizo za mradi na kuelekeza hatua za kuchukua kwakuwa vielelezo alivyokabidhiwa na msimamizi wa mradi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji,  Sabastian Gaganijas, vina mashaka. 


“Naagiza ukaguzi ufanyike, lazima kuna ubadhirifu umefanyika katika utekelezaji wa mradi, baada ya ukaguzi makini, tutajua ukweli na kubaini hatua gani zitachukuliwa,” alisema Mpina.


Baada ya zoezi zima la kukagua Delta hiyo yenye kilomita zaidi ya tano,  Naibu Waziri Mpina, alisema amesikitishwa na utekelezaji wa mradi huo unaotumia  fedha za wafadhili zaidi ya Sh milioni 396 kuwa na madudu.


Alisema mradi huo ulikosa usimamizi huku akisema kuna dalili ya fedha hizo kutumika ndivyo sivyo kwakuwa hata hekta 792 kati ya 1,000 zilizodaiwa zimepandwa ni udanganyifu wa wazi.


“Huu ni uhuni ambao haukubaliki kwa Serikali hii ya awamu ya tano, tuliposema hapa kazi tu tulimaanisha kuwa hatuwezi kudanganywa, watu wamezoea kuona Waziri hawezi kuja kwenye mazingira kama haya nimejionea mwenyewe mikoko iliyopandwa haiendani na thamani ya matumizi ya fedha hizo na sehemu kubwa imevamiwa na kupandwa mpunga badala ya mikoko,” alisema.
Alisema katika mchanganuo aliokabidhiwa na msimamizi wa mradi, fedha hizo zaidi ya Sh milioni 364 zimedaiwa matumizi yake ni pamoja na kulipa vikundi 28 vilivyokabidhiwa mradi ambavyo sasa havipo.


Alisema cha kushangaza katika fedha hizo kipo kikundi kimelipwa zaidi ya Sh milioni 30 kwa kupanda hekta 3 huku kingine kikilipwa milioni 3 kwa hekta hizo hizo.


Awali mtaalamu wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu  wa Rais, Cretus Shengena, alisema uharibifu huo wa mikoko unaweza kusababisha kupotea kwa uoto wa asili na baiyonuwai katika eneo hilo kama udhibiti wa dhati usipochukuliwa kwa haraka kunusuru eneo hilo la Delta ya Rufiji Kaskazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles