MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MPIGA picha wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Aika Kimaro, ameibuka mshindi wa pili katika shindano la kupiga picha za habari.
Mshindi wa kwanza katika shindano hilo alikuwa mpiga picha wa kujitegemea, Imani Isamula ambaye aliibuka kidedea kwa kura 57 dhidi ya kura 43 alizopata Aika.
Washindi hao walitangazwa juzi jijini Dar es Salaam katika mdahalo katika mdahalo ulioandaliwa na Ubalozi wa Netherland katika mwendelezo wa maonyesho ya picha (World Press Photo 2018) ambayo yanaendelea.
Imani aliibuka kidedea kutokana na picha zake za walemavu wa miguu ambapo mlameavu mmoja ni mwanamke ambaye amekimbiwa na mume wake na kuachiwa watoto ambao anawalea peke yake.
Katika picha nyingine mlemavu wa kiume ambaye licha ya ulemavu wake anaonekana kujishughulisha na shughuli za uvuvi wa samaki.
Kwa upande wa Aika moja kati ya picha zakie mbili zilizoshinda, inamuonyesha mwanamke aliyebeba mzigo wa magunia mawili yaliyofungwa kwa kamba yakiwa na chupa tupu za plastiki huku amebeba mtoto mgongoni anavuka barabara.
Akifafanua kuhusu picha hizo, Aika alisema mama huyo licha ya kuwa na shuguli nyingi nyumbani ambazo hazimuingizii kipato ameamua kumbeba mtoto wake mgongoni na kuamua kuingia mtaani kujitafutia chochote kwa ajili ya watoto wake.
“Katika picha ya pili, hawa ni watoto wanaonekana wakiwa na magunia wanaokota makopo na chupa za maji ili wakauze, picha hii inazungumza mengi, kwanza hawa ni watoto ambao wamekosa haki zao za msingi kama haki ya kusoma na haki ya kucheza,” alisema.
Washindi hao wamezawadiwa wamepata ufadhili wa Euro 500. Maonyesho hayo ya picha yanaendelea hadi Februari 6, mwaka huu katika Viwanja na Alliance Francaise jijini Dar es Salaam.