29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

CCM: JPM ni ajenda ya maendeleo kwa taifa

MWANDISHI WETU-MOROGORO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kwa sasa Rais Dk. John Magufuli ndiyo ajenda kuu ya maendeleo ya nchi.

Pia kimesema kiongozi huyo wa nchi amekuwa akipigania haki za wanyonge na kuonyesha misingi ya uongozi bora kwa Taifa na watu wake.

Hayo yalisemwa jana mjini Morogoro katika mdahalo wa uzalendo wa vijana la kuadhimisha miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM na Katibu wa Mkoa wa huo, Shaka Hamdu Shaka.

Katibu huyo alisema ni lazima Watanzania waungane na mkuu huyo wa nchi ili kuweza kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya viwanda na yenye kutegemea uchumi wa kati.

Alisema pamoja na hali hiyo bado hata vijana ambao wazee hao wamenufaika na mfumo wa CCM ndio wamekuwa mstari wa mbele kulitukana taifa na viongozi wake jambo ambalo si sahihi na kinyume na utamaduni wa Watanzania.

“Dk John Magufuli sasa amekuwa kioo cha maendeleo yetu na ajenda kuu katika  kupigania haki za wananchi  wote huku akionyesha uongozi bora ndani ya nchi yake lazima Watanzania tuonyeshe kuguswa kimitazamo na kimkakati na kuendelea kumuombea kutimiza dhamira na ndoto za kuivusha Tanzania katika maendeleo endelevu kiuchumi kijamii na kisiasa.

“Kwa masikitiko makubwa wakati tukijadili dhana hii ya uzalendo, uongozi na hatma ya Taifa letu baadhi ya viongozi na watoto wao ambao wameneemeka kwa  jasho la CCM wamekuwa maadui hatari kwa muktadha wa utawala wetu, wengine  miongoni mwao tunajua   kama wasingelibebwa na viongozi wetu  wala wasingefahamika, wasingefikiriwa kuwa viongozi na kuitwa wanasiasa,” alisema Shaka.

Kutokana na hali hiyo Shaka, aliwataka vijana kujadili kuhusu uongozi na uzalendo kwa kutambua kwao wao ndio warithi na viongozi wa Taifa  hivyo wakati wote wanapaswa kukemea, kukosoa kwa adabu na heshima na kupaza sauti pale taifa linapohatarishiwa kutaka  kuyumbishwa kwa masilahi ya wachache.

“Tunawambia mabeberu wa ukoloni popote walipo duniani wakati  umefika kutambua wajibu wao licha ya mataifa yao kulitegemea Bara la Afrika kimaendeleo kutokana na rasilimali zake, mataifa hayo  kiuhalisia hayapaswi tena kuingilia uhuru wetu, utu na demokrasia tunayoiamini au pale tunapotaka kujipangia hatma na aina ya uongozi.

 “Baadhi ya mabeberu hao tunawakanya waache kupalilia chuki na hasama za kisiasa kwa kuwatumia vibaraka wasiozitakia mema nchi zao  pia kutotupangia  hatamu za  kiutawala na kidemokrasia kwa  aina ya uongozi tunaoutaka. Masuala ya Tanzania yatapangwa na Watanzania wenyewe na  watu wake na  kwa  mitazamo ya serikali zake,” alisema.

Katibu huyo ambaye pia aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, alisema Afrika haitoingiliwa katika sera zake na uendeshaji wa na nchi za ulaya.

“Kwa vile  waafrika hawaiingilii masuala ya kisera wala ya kimaendeleo ya nchi zingine, mataifa ya kigeni nayo  ni vyema yakabaki kuwa washirika wa maendeleo na si kututungia masharti.

  “Tanzania chini ya Chama Cha Mapinduzi hailazimiki kufuata matakwa ya Taifa lolote duniani badala yake serikali za  CCM  zinawajibu wa kuendelea kuheshimu  na kudumisha mahusiano mema pia  kuendeleza ushirikiano wa kijamii, kisiasa na kiuchumi na mataifa rafiki yanayoheshimu mambo yetu ya ndani.

“Kwa kutumia jukwaa hili la maashimisho ya miaka 42  kuzaliwa CCM,  tunawahimiza vijana wetu wote Afrika wajitume kupata  elimu zaidi, wapime mambo na kuyatafakari kabla ya kutenda,” alisema.

Alisema inapotokea baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Afrika wanapokubali kirahisi kuuza utu wao, kuhongwa fedha na kufanywa makuwadi wa kisiasa ili kuzigombanisha nchi zao ili  watu wake wamwage damu ni jambo la kuhuzunisha.

“Patrice Lumumba huko DRC ameuawa kinyama kwa njama za Waafrika wenzetu, mamluki wengine wa Afrika wameyakatisha maisha ya kina Abeid Amani Karume Zanzibar, Jenerali Murtala Mohamed wa Nigeria na Marian Ngwabi wa Kongo Brazaville.

“Mashujaa wengine ni Kepteni jasiri na mzalendo  wa kweli Thomas Sankara wa Bukinafasso, William Turbert wa Liberia, Samora Machael wa Msumbuji na Kanali Muamar Gaddafi wa Libya ili kuwafurahisha na kuwaneemesha mabeberu.

“Tuendelee kuyasoma na kujifunza kutoka kwao  waasisi wa TANU, ASP na Chama Cha Mapinduzi pia kuwaenzi  wapigania uhuru wa  Afrika  kina Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dk. Kwame Nkrumah, Tseres Khama, Mfalme Haile Sellasie, Dk. Kenneth Kaunda  na Gamal Abdi Nasser.

“Wengine ni Mzee Jomo Kenyatta, Dk Milton Obote, Abdul Diofu, Ahmed Sekou Toure, Agostino Netto, Nelson Mandela na Mzee  Robert Mugabe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles