BRUSSELS, UBELGIJI
MJUMBE wa Umoja wa Ulaya, Michel Barnier na wawakilishi wa Uingereza wamemaliza mazungumzo juu ya kufikia makubaliano yatakayoishuhudia Uingereza ikiondoka katika umoja huo kwa amani kwa kuambulia patupu.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini hapa yalilenga kufanikisha mpango huo ujulikanao kama Brexit utakaoweza kuungwa mkono na wabunge wa Uingereza walioukataa ule uliofikiwa awali.
Hilo limetokea huku zimesalia siku 24 kabla ya nchi hiyo kuondoka Umoja wa Ulaya.
Barnier alikutana na Mwanasheria Mkuu wa Uingereza, Geoffrey Cox na Waziri anayeshughulikia suala la Brexit, Stephen Barclya.
Hata hivyo, mazungumzo hayo kati ya wajumbe hao watatu yaliyochukua muda wa zaidi ya saa tatu yalimalizika bila kupatikana makubaliano yoyote.
Vyanzo kutoka pande zote mbili vimesema mazungumzo kati ya maofisa wa ngazi ya chini yataendelea.
Awali Jumamosi iliyopita, Barnier alisema Umoja wa Ulaya upo tayari kuipa Uingereza uhakikisho zaidi.
Aidha alipendekeza viongozi wa Ulaya wairefushie Uingereza muda zaidi ili kuiwezesha isiondoke kwenye umoja huo ifikapo Machi 29 bila kuwapo makubaliano.
Alisema kwa kufanya hivyo pia kutalipa Bunge la Uingereza muda zaidi kuweza kuidhinisha rasmi mkataba wa mwisho.