20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Hivi ndivyo malaria inavyowamaliza wajawazito, watoto

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

RIPOTI ya utafiti wa viashiria vya malaria ya mwaka 2017/18 inaonesha kiwango cha maambukizi ya malaria kimepungua kwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na ripoti ya mwaka 2015 ambapo ilikuwa asilimia 14.4.

Ripoti mpya inaeleza bado kuna maeneo ambayo kiwango cha maambukizi kipo juu, huku Mkoa wa Kigoma na wilaya zake nyingi zikibainika kuongoza kwa maambukizi.

Malaria ni kati ya magonjwa yanayotajwa kusababisha vifo vingi nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu za sasa, katika kila wagonjwa 1,000 wa malaria, tisa hufariki dunia.

Wajawazito na watoto hasa walio chini ya umri wa miaka mitano, ndiyo kundi lililopo hatarini zaidi kuathiriwa na ugonjwa huo ikilinganishwa na makundi mengine.

Ripoti ya WHO

Tafiti mbalimbali zinaonesha bado dunia inakabiliwa na changamoto ya maambukizi ya ugonjwa huu, hasa katika nchi zilizopo Bara la Afrika.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inaeleza katika mwaka 2016 watu milioni 216 walipata maambukizi ya ugonjwa huo na 445,000 walifariki dunia.

WHO linasema japo idadi ya vifo vilivyotokana na malaria kwa upande wa eneo la Afrika Mashariki ilipungua, bado raia wa mataifa hayo wapo hatarini kukumbwa na maambukizi mapya.

Ripoti hiyo inasisitiza kundi la wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ndilo lililopo katika hatari zaidi kuliko makundi mengine.

Shirika hilo limeweka lengo la kidunia kwamba ifikapo 2030 malaria iwe imetokomezwa duniani.

Kila nchi sasa inajikita kuhakikisha inafanya kila namna kukabili na kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo ili kufikia lengo la maambukizi sifuri.

Jitihada za MUHAS

MTANZANIA limezungumza na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), anayeshughulikia taaluma ya utafiti na ushauri wa kitaaluma, Profesa Aporilnary Kamuhabwa, ambaye anaeleza namna wanavyoshiriki  kuhakikisha Tanzania inafikia lengo hilo la kidunia.

“Majukumu ya chuo kikuu ni pamoja na kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu, huwa tunaangalia maeneo ambayo nchi imeweka kipaumbele, malaria ni miongoni mwa magonjwa tunayopambana nayo,” anasema.

Anasema kwa kuzingatia suala hilo, waliamua kujikita kufanya utafiti kuangazia mapambano dhidi ya malaria kwa wajawazito na watoto.

“Ni kweli serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanya kazi kubwa kupambana na malaria na sasa kiwango cha maambukizi kimeshuka kwa kiasi kikubwa.

“Hata hivyo, bado kwenye maeneo kadhaa kuna changamoto, mengine kiwango kipo chini na mengine kipo juu zaidi ya wastani wa kitaifa, hili kundi la wajawazito na watoto linatajwa kuwa hatarini zaidi kupata maambukizi,” anabainisha.

Profesa Kamuhabwa anatoa mfano wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwamba tafiti zinaonesha kiwango cha maambukizi kipengua na kufikia chini ya asilimia moja, lakini bado maeneo mengine yanakabiliwa na changamoto.

Tafiti

Anasema utafiti mmoja uliofanywa na wataalamu wa chuo hicho, ulihusisha wajawazito 1,191 waliokuwa wakihudhuria kliniki katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.

Anasema matokeo ya awali yanaonesha wajawazito wanaohudhuria vema kliniki na kupatiwa dawa kinga dhidi ya malaria kulingana na kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), hujifungua watoto wenye uzito timilifu kuliko wale wanaosua sua.

“Malaria ni miongoni mwa visababishi vya mtoto kuzaliwa na uzito pungufu, hali hiyo huambatana na changamoto mbalimbali kwa mtoto husika kipindi cha ukuaji wake,” anasema.

Anasema katika utafiti walioufanya, wataalamu wao waliangalia iwapo dawa aina ya SP inayotumika kuwakinga wajawazito, inasaidia kukabili ugonjwa huo au la!

“Dawa hiyo huwa wanapatiwa wajawazito wanapohudhuria kliniki hasa mimba ikiwa imefikia wiki ya 13 na kuendelea baada ya uchunguzi, hupatiwa kila wiki kulingana na sera ya WHO na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Matokeo ya awali yanaonesha mafanikio – inasaidia. Tumejaribu kuangalia walitumiaje dawa hiyo ya SP, tulichunguza hadi kondo la nyuma kuangalia iwapo vimelea vya malaria vilibaki, kwa sasa tunafanya majumuisho kati ya Machi na Aprili, mwaka huu, tunatarajia kukamilisha,” anabainisha.

Anasema kimsingi kadiri mjamzito anavyotumia vizuri dawa hiyo, ndiyo inavyosaidia kuzuia madhara kwa mtoto anayezaliwa hasa kuwa na uzito pungufu na kukabili tatizo la upungufu mkubwa wa damu kwa mama husika.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwahimiza wajawazito kuhudhuria kliniki, pamoja na utafiti huu tunafanya pia mwingine huko Rufiji mkoani Pwani, tukiangazia aina nyingine ya dawa kinga ambayo inaweza kuwa mbadala wa SP ikiwa itaonesha usugu katika kukabili ugonjwa huo,” anasema.

Anasema dawa hiyo inayofanyiwa utafiti imependekezwa na WHO, ineonesha mafanikio Tanzania kama ilivyo kwa Kenya na Uganda.

“Tupo kwenye majumuisho kuitafiti kabla haijaruhusiwa kuanza kutumika rasmi lazima nasi tujiridhishe,” anasisitiza.

Anasema pamoja na tafiti hizo, MUHAS kwa kushirikiana na wadau wengine sasa zinaendelea pia kufanya mbalimbali kumchunguza mbu aenezaye ugonjwa huo na mazingira ya mazalia kwa ujumla wake.

NIMR

Naye Mtafiti wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) – Tanga, Deus Ishengoma, anasema upo mkakati wa kidunia ulioundwa na WHO unaolenga nchi zote ifikapo 2030 ziwe zimetokomeza malaria na ifikapo 2040 ziwe zimeiondoa kabisa kwenye uso wa dunia.

“Mkakati huo unalenga kutumia mbinu za kitaalamu na kiubunifu kuhakikisha tunatokomeza malaria, ikiwamo kutumia vyandarua na dawa za kutibu kama mseto.

“Kufanya ufuatiliaji mzuri wa kujua wagonjwa wapo wapi, wapi kuna kiwango kikubwa cha malaria na wapi kimepungua, ili kuhakikisha taarifa tunazozitoa ziwe msaada zaidi.

“Tanzania tuna mpango mkakati 2015-2020, ulilenga kuhakikisha ifikapo 2020 tunapunguza malaria ili tunapoelekea 2030 tuitokomeze kabisa.

“Taarifa za mwaka jana zilionesha tunaweza kufikia malengo, kudhibiti malaria, wadau walikaa na kuangalia mbinu mpya za kupambana na malaria ili tuweze kufikia malengo,” anasema.

Anaongeza: “Wanataka kujaribu kuikabili malaria kutegemeana na hali ilivyo katika maeneo mbalimbali, kwamba yale yenye malaria kali mbinu za kuikabili ziwe tofauti kabisa na maeneo ambayo yana kiwango kidogo.

“Changamoto katika utafiti, upande wa fedha, kwa hali ilivyo sasa, tunategemea wafadhili kutugharamia kufanya tafiti zetu kitaifa, matokeo yake hatuwezi kufanya tafiti ambazo tumeziibua sisi wenyewe kuangalia matatizo yetu kama Watanzania.

“Kwa sababu wale wanaoleta fedha zao wanakuwa na malengo yao na sisi tunakuwa na malengo yetu, ili tuweze kwenda mbele tunahitaji serikali itusaidie kama ilivyokuwa imeahidi kutoa asilimia moja ya pato la Taifa kwa ajili ya kuwezesha tafiti, itupe walau kidogo, ili tuweze kutoa tafiti ambazo zinaibua majibu.

“Tunahitaji tafiti za kugundua, tumfahamu vizuri huyu mbu anayesababisha malaria, kimelea kinachoambukiza, mbu wanaoeneza tunaweza kuwakabili vipi, mbinu gani zinafaa na wapi?

“Tunatakiwa kuzichukua na kuzifanyia kazi ili tunavyokwenda kupambana na malaria tutumie mbinu ambazo wananchi wamekubaliana na sisi ili twende pamoja nao katika mapambano haya.

“Shida kubwa ni rasilimali fedha, wataalamu tupo wengi tu, fedha tunazotumia zinatoka nje, inakuwa vigumu kuwaelekeza katika maeneo tunayoyataka, watatuelekeza wao,” anabainisha.

MWISHO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles