Na FRANCIS GODWIN -IRINGA
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amepiga marufuku wananchi kutumia eneo lenye mgogoro kati ya Kijiji cha Ilambilole Wilaya ya Iringa na Irole Wilaya ya Kilolo hadi hapo watakapotuma wataalamu kubainisha mpaka unaotenganisha wilaya ya Kilolo na Iringa.
Mbali ya kuzuia kutumia eneo hilo, Waziri Mabula, amemzuia mmoja kati ya wafugaji wa jamii ya Maasai kuendelea na ujenzi wa nyumba katika eneo hilo huku akiliagiza Jeshi la Polisi wa wilaya hizo kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayepuuza agizo hilo.
Alisema mpaka wowote lazima useme ni gazeti gani la Serikali lilitangaza katika mipaka ya Kilolo na Iringa ambayo ilizaa Kilolo waliweka GN yao namba 366 ya mwaka 2002 hivyo mipaka hiyo ndiyo inayotambuliwa na si vinginevyo.
“Mbali na utambuzi wa mipaka hiyo ni marufuku kwa mtu yeyote kuendelea na shughuli yoyote iwe ya ufugaji, kilimo ama ujenzi katika eneo hilo hadi wataalamu watakapobainisha mipaka hiyo.
“Iwapo kama mpaka wa wilaya na wilaya hauna tatizo, iweje kuwe na mgogoro wa mipaka ya kijiji wakati mipaka ya wilaya ipo sawa, naomba kusema mwananchi wa Kilolo kulima eneo la Iringa ama mwananchi wa Iringa kulima ama kufanya shughuli zake katika Wilaya ya Kilolo si tatizo na huwezi sema ni mgogoro, mtu anaweza kulima ama kufanya shughuli zake popote pale ili mradi asivunje sheria,” alisema Mabula.
Awali Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa wananchi wa Irole ndio ambao wana uhitaji mkubwa wa eneo hilo na ndiyo sababu wamefika katika mkutano huo tofauti na wenzao wa Ilambilole.
“Siku zote mgogoro huo ni wa pande mbili ila katika hilo inaonyesha wananchi wa Ilambilole hawana shida na eneo hilo isipokuwa mtu mmoja kulitaka kwa manufaa yake,” alisema Mwamoto.