MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho, amedai kuwa thamani ya kiungo wake mshambuliaji, Paul Pogba, itashuka ndani ya misimu miwili ijayo kutokana na bei ya wachezaji kubadilika kila msimu.
Mchezaji huyo alijiunga na klabu hiyo wakati wa majira ya joto mwaka jana akitokea klabu ya Juventus, usajili wake uliweka rekodi mpya duniani na kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa katika usajili, lakini Mourinho anaamini misimu miwili ijayo thamani ya wachezaji itakuwa zaidi.
Mourinho amedai kuwa, kwa sasa klabu zinasajili mchezaji kwa fedha nyingi kuliko uwezo wake, hivyo anatarajia kuona baadhi ya wachezaji wenye kiwango nusu ya Pogba wakisajiliwa kwa fedha nyingi zaidi.
Pogba mwenye umri wa miaka 23, alisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 89 ambazo ni zaidi ya bilioni 100 pamoja na majumuisho mengine, usajili huo ulifunika wa nyota wa Real Madrid, Christiano Ronaldo ambaye alijiunga na klabu hiyo akitokea Man United kwa kitita cha pauni milioni 80, wakati huo Gareth Bale akijiunga kwa pauni milioni 85.
“Ninaamini Pogba kwa sasa anajisikia kuwa katika hali nzuri ya maisha yake kutokana na historia ya usajili wake, lakini anatakiwa kujua thamani yake ya fedha inatakiwa kuendana na kila anachokifanya uwanjani.
“Kuna uwezekano mkubwa misimu miwili ijayo tunaweza kuona mchezaji mwenye uwezo wa kawaida akisajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha kuliko kile cha Pogba, ninaamini hivyo kutakuwa na wachezaji ambao uwezo wao hata nusu ya Pogba haujafikia lakini fedha ambazo zitawasajili zitakuwa ni nyingi zaidi.
“Miaka michache iliyopita wachezaji walikuwa wananunuliwa kwa kiasi kidogo cha fedha kama vile pauni milioni 25, lakini kwa kipindi hicho zilionekana ni fedha nyingi, lakini kwa sasa pauni milioni 25 inaonekana hakuna kitu.
“Tusubiri kuanzia msimu ujao wakati wa majira ya joto, dunia inaweza kushangaa kutokana na thamani ya wachezaji kuwa kubwa zaidi, kuna uwezekano mkubwa thamani ya Pogba kuwa mchezaji aliyenunuliwa kwa fedha nyingi duniani ikashuka kabisa na linaweza kuwa jambo zuri kwa wachezaji wengine,” alisema Mourinho.
Hata hivyo, kocha huyo amesema anaamini si kila klabu itakuwa na uwezo wa kusajili wachezaji kwa fedha nyingi kama walivyofanya Manchester United kwa Pogba, lakini bei ya wachezaji itazidi kuwa juu.