KOCHA wa timu ya Manchester United, Jose Mourinho, amesema kipigo cha 4-0 walichopata kutoka kwa Chelsea kimetokana na makosa ya ajabu ya kiulinzi.
Mabao kutoka kwa Pedro Hernandez, Gary Cahill, Eden Hazard na N’Golo Kante yalimpiga Mreno kipigo kikubwa zaidi katika maisha yake ya Ligi ya England aliporejea Darajani Stamford.
“Tulikuwa na mwelekeo wa kimakosa, tulitaka kutengeneza nafasi, tulionesha hivyo baada ya kupigwa 1-0,” alisema Mourinho akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports News.
Mourinho alisema bao la pili na la tatu yalikuwa mabao ya shambulizi la kushtukiza na kudai kwamba kama wangefunga bao wangepata 2-1 na mambo yangekuwa tofauti.
“Leo (jana) ni siku ambayo tumempa fursa mpinzani wetu kwa kutofanya chochote anachotaka. Tulifanya makosa ya ajabu sana ya kiulinzi, makosa yetu binafsi ndio ambayo yalitugharimu.
“Kwa upande wa pointi, tumepata pointi sufuri, tumepoteza pointi tatu. Tunapungukiwa pointi sita kumfikia kinara wa ligi, tatu dhidi ya timu ya nne, tunahitaji sasa kushinda mechi nyingi,” alisema Mourinho.
Mreno huyo alisema kuwa baada ya kipigo hicho wanajipanga kushinda michezo yao jambo ambalo si rahisi kutokana na kuhitaji kuziba mapengo, baada ya michezo mitatu ya mwisho.
Matokeo hayo yameiacha United nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi baada ya mechi tisa, wakati Chelsea ikikwea hadi nafasi ya nne.