25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wawaka majimboni

Na WAANDISHI WETU – DAR /MIKOANI

MOTO umewaka. Ndivyo unaweza kusema baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufungua milango kwa wanachama wake wanaotaka fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Uchukuaji na urejeshaji fomu hizo za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge na udiwani umeanza jana na kuendelea hadi Julai 17 saa 10 jioni ambayo itakuwa mwisho.

Hata hivyo katika uchaguzi wa mwaka huu ndani ya CCM wanachama wenye majina makubwa wamejikuta wakipigana vikumbo vya kusaka fomu za kuomba kuteuliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa wanachama waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Mkurugenzi wa Sport Pesa, Abbas Tarimba ambaye alichukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Kinondoni, Askofu Josephat Gwajima akiomba Jimbo la Kawe na Mkurugenzi mstaafu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei alichukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania Jimbo la Vunjo lililokuwa likiongozwa na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi.

HALI JIJINI DAR

Katika Wilaya ya Kigamboni kwa siku ya jana, wanachama 29 walijitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa akiwamo mbunge aliyemaliza muda wake, Dk. Faustine Ndugulile na msanii wa vichekesho, Mjuni Sylivester maarufu Mpoki.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kigamboni, Yusuphu Mabena alisema wanatarajia kuona idadi hiyo ikiongezeka kutokana na demokrasia kuwa pana zaidi kiasi cha kuwaruhusu hata wasionacho kuweza kushiriki.

Mabena alisema wanatarajia kuona idadi hiyo ikiongezeka zaidi kutokana na watu wengi ambao awali walifika kutia nia kutokuchukua fomu hadi sasa.

“Hadi sasa (jana saa tisa alasiri) tuna watu 29 waliofika kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwenye Jimbo la Kigamboni, tunatarajia kuona orodha hiyo ikiongezeka zaidi.

“Hatua hii inatokana na kukua kwa demokrasia ndani ya CCM na kutoa nafasi hata kwa wasiokuwanacho waweze kushiriki, hivyo bado idadi hii itaongezeka zaidi hadi kufikia mwishoni mwa zoezi hili Julai 17,” alisema Mabena.

Aliwataja waliojitokeza hadi jana kuchukua fomu hizo za kuomba kuwania ubunge Kigamboni kuwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Ndugulile aliyechukua fomu, kuijaza na kuirudisha ndani ya dakika 20 na msanii wa vichekesho, Mpoki.

Wengine ni Wakili Tumaini Lyimo, Rwegasira Themi, Frank Chalamila, Kassim Juma, Edwin Mwesigabo, Chrian Holu, Daniel Sarungi, Ali Malima, January Tamanywa, Wandeti Kasaja, Kwessi Ukwaju, Lilian Wasira, Eliud Mganga, Sogone Wambura, Christopher Saruati, Mhandisi Daniel Madushi, Rashid Jumbe, Ally Msati na Francis Mgisha.

ILALA

Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Idd Mkowa, alisema hadi jana jioni zaidi ya wanachama 80 walijitokeza kuchukua fomu kugombea ubunge katika majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea.

Kulingana na katibu huyo, wanachama 40 walijitokeza kuchukua fomu kugombea ubunge Segerea wakati Ukonga ni 43 na Ilala 9.

Alisema mwitikio wa wanachama kuchukua fomu ni mkubwa na kwamba umetokana na kukua kwa demokrasia ndani ya CCM.

“Watu wengi wameitikia baada ya kuona demokrasia katika chama imepanuka na zoezi hili linaendeshwa kwa uwazi na ufanisi wa hali ya juu.

“Mwitikio ni mkubwa zaidi, wenyewe mmeona foleni nje hapo, kwa hiyo hadi keshokutwa wagombea wengi watakuwa wamejitokeza.

“Mtu anatakiwa aje na ada ya Sh 100,000 kisha ajaze fomu na kuirudisha, hatuhitaji vikao visivyo rasmi au makundi mtaani, kura ataziomba ukumbini,” alisema Mkowa.

Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) aneyeongoza Idara ya Sheria Binafsi ambayo ni moja kati ya Idara Kuu tatu za Shule Kuu ya Sheria chuoni hapo, Dk. James Jesse ni miongoni mwa waliochukua fomu kuwania ubunge Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CCM.

Alichukua fomu huku akibainisha kuwa baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama mtumishi wa umma, sasa ameona ni wakati mwafaka kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendekeo kwa njia nyingine.

“Chama kinataka watu watakaoweza kuwaletea wananchi maendeleo na mimi nimejitafakari nimeona uwezo huo ninao kama chama kitanipa ridhaa,” alisema Dk. Jesse.

Msomi huyo ambaye alikuwa askari wa Jeshi la Polisi kwa miaka 10, alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kusimamia vyema rushwa kwa maelezo kuwa utaratibu unaotumika sasa CCM umepunguza vurugu, hasa mitaani.

“Chama kimeandaa utaratibu mzuri kwa wagombea utakaosaidia kupunguza vurugu kwenye majimbo, mgombea akishachukua fomu anajaza na kuirejesha kisha anasubiri siku ya uteuzi, ni jambo zuri kwa kweli,” alisisitiza Dk. Jesse.

Akieleza sababu za kujiunga na Jeshi la Polisi licha ya kufaulu alama za juu kidato cha sita na kuchaguliwa kujiunga na UDSM alisema, “Nilikuwa nikifurahishwa sana kila nilipokutana na polisi njiani. Mavazi yao na jinsi walivyokuwa waking’arisha viatu vyao yalinifurahisha. Kujiunga polisi niliona nimetimiza ndoto.”

Alisema alipangiwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wakati akilitumikia jeshi hilo aliendelea na masomo UDSM hadi alipoacha na kujikita katika taaluma yake ya sheria na kuwa mhadhiri wa chuo hicho.

“Nina shahada nne katika sheria. Niliamua kusoma kwa sababu mtu yeyote akiwa UDSM kama mhadhiri anapaswa kuwa na uelewa mpana sana wa mambo. Kwahiyo kadiri anavyosoma ndivyo anarutubisha ubongo wake,” alisema Dk. Jesse.

Aidha kwa upande wa udiwani, wanachama mbalimbali wamejitokeza katika ofisi za CCM kwenye kata mbalimbali wilayani Ilala kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama kugombea.

Miongoni mwa waliochukua fomu hizo na kata wanazogombea kwenye mabano ni Heri Shaaban (Tabata), Onesmo Kapinga (Buyuni) na Mabindo Ngulu (Kipawa).

KINONDONI

Wanachama 111 wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu katika Wilaya ya Kinondoni, yenye majimbo ya Kinondoni na Kawe.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuhitimisha utoaji wa fomu katika siku ya kwanza jana, Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Sure Mwasanguti alisema

mwitikio umekuwa mzuri kwa wanachama wengi kujitokeza katika siku ya kwanza na kuwaomba wengine kujitokeza zaidi.

Alisema katika ufuatiliaji, wagombea wote waliochukua fomu wamefuata kikamilifu maelekezo ya utaratibu uliowekwa na chama hicho.

“Leo watia nia wa ubunge katika majimbo mawili ya wilaya yetu wameanza kuchukua fomu. Kwa utaratibu wa chama chetu, tuliagiza kuwa hatuhitaji sherehe wala shamrashamra.

“Pia tulielekeza kuwa hatuhitaji kundi la watu wengi isipokuwa kama ikibidi wasindikizaji mmoja au wawili.

“Wote waliochukua fomu leo walifuata maagizo hayo na utaratibu wa chama, tunawaomba wengine watakaokuja pia waige mfano huo,” alisema Mwasanguti.

Akitoa ufafanuzi wa watu waliochukua fomu, alisema katika Jimbo la Kinondoni wamechukua wanachama 31 na wawili tayari wamesharudisha jana hiyohiyo.

Alisema katika Jimbo la Kawe waliochukua fomu ni wanachama 80 na wanne tayari walishazirejesha baada ya kukamilisha taratibu za ujazaji.

Mwasanguti alisema utaratibu wa uchukuaji fomu na kuzirejesha unaendelea hadi Julai 17 na kuwataka watia nia wote wanaokwenda kuchukua kuheshimu taratibu zilizowekwa na chama hicho.

Miongoni mwa waliochukua fomu wamo wasanii na watu maarufu, wakiwemo Mchungaji Joseph Gwajima kwa Jimbo la Kawe na Abbas Tarimba Jimbo la Kinondoni.

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kinondoni, Said Abdalla Subeti na Naibu Meya Kinondoni, George Manyama.

Baadhi ya wasanii waliojitokeza kuchukua fomu ni Asha Baraka, Ado Novemba na Mwijaku.

TEMEKE

Hekaheka katika uchaguzi wilayani Temeke zimepamba moto kwa wagombea ubunge na udiwani kupigana vikumbo.

MTANZANIA lilifika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Temeke na kushuhudia wanachama wa chama hicho kwa nyakati tofauti wakipishana.

Wengine wakifika na wapambe wao, lakini walizuiliwa kutokana na agizo lililotolewa na uongozi wa ngazi ya juu kutoruhusu shamrashamra zozote wakati wa uchukuaji na urejeshaji fomu.

Akizungumza jana, Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Temeke, Ally Kamtande alisema mwamko wa uchukuaji fomu ni mkubwa kuanzia nafasi ya udiwani na ubunge.

Alisema hadi jana jioni zaidi ya wanachama 60 walijitokeza kuchukua fomu za kuomba uteuzi wa chama kwa nafasi za ubunge na udiwani.

Miongoni mwa waliofika katika ofisi hizo kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea ubunge, majimbo na kata zao kwenye mabano ni mwandishi wa habari mkongwe, Shija Richard (Mbagala), Kika Tunutu (Temeke), Omary Ally (Temeke ) na Albert Modest (Temeke).

Wengine ni Nicholous Mpangala (Temeke), aliyekuwa Katibu wa Yanga, Saimon Luhwago (Temeke), Imani Mwanahamba (Mbagala) na Abbas Mtemvu (Temeke)

Kwa upande wa Viti Maalumu udiwani, waliojitokeza ni msanii Sabrina Lupia (Mtoni Kijichi), Fatma Ally (Mbagala Chamazi), Farida Mkwanyu (Kata ya Mtoni), Fatma Mbotoni (Mbagala Kuu) na Albertina Mbaji (Temeke).

NJOMBE

Mwanasheria mwandamizi wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Philip Filikunjombe ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Ludewa mkoani Njombe.

Dk. Filikunjombe alikuwa mwanachama wa nane kujitokeza kwa siku ya jana akitanguliwa na mbunge aliyemaliza muda wake Deo Ngalawa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM Wilaya ya Ludewa, Bakari Mfaume, alisema idadi ya wagombea waliofika kuchukua fomu ya ubunge wamefikia 10 wakati waliotangaza nia walikuwa 25.

Alisema wengine wanatarajiwa kuendelea kujitokeza licha ya kuwa ni siku ya mwanzo huku fomu za udiwani zikitolewa kwenye kata husika. “Zoezi limefunguliwa leo (jana) tarehe 14 hadi 17, watu wamejitokeza pamoja na kwamba leo ni siku ya mwanzo na zoezi la kuchukua fomu za udiwani wa kata zinafanyika kwenye kata zenyewe.

“Lakini kwa udiwani viti maalumu Katibu wa UWT wilaya ndiye anayeshughulikia kuchukua hizo fomu na mpaka sasa zoezi limeanza na linaendelea vizuri,” alisema Mfaume.

Aidha ametoa wito kwa wagombea kuendelea kufuata kanuni na utaratibu wa chama hicho ikiwemo wanachama kutoruhusiwa kufika katika ofisi wakiwa katika hali ya mikusanyiko.

“Yako mambo ambayo haturuhusu na ambayo tunaruhusu, katika uchaguzi huu wa ndani ya chama haturuhusu wagombea kusindikizwa na watu, mbwembwe haziruhusiwi kwa sababu huu ni uchaguzi wa ndani na sisi tunaamini wanachama wote ni sawa.

“Lakini vile vile tunakataza kufanya kampeni za aina yoyote kuanzia kuweka katika mitandao au kuwa na vipeperushi au kuwatembelea wanachama,” alisema Mfaume.

Katika Jimbo la Lupembe mkoani humo, watu watatu akiwemo wakili msomi wa kujitegemea Edwin Swale, walijitokeza na kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea ubunge.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Wanging’ombe, Juma Nambaila, wanachama 20 wamejitokeza kuchukua fomu akiwamo aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Gerson Lwenge ambaye amechukua na kurudisha tayari.

Katibu wa CCM Wilaya ya Makete, Amina Imbo, alisema hadi jana waliochukua fomu ni 23, wanaume wakiwa 21 na wanawake wawili.

TANGA

Kwa siku ya jana, Ofisa kutoka Ofisi ya Rais na Utawala Bora, Mariam Mwanilwa pamoja na wanasiasa wengine walijitokeza kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika Jimbo la Handeni Mjini.

Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni, Salehe Kikweo alisema hiyo ni fursa pekee kwa wanachama wanaojiona wanatosha kuongiza katika nafasi hizo ili mradi wazingatie masharti waliyowekewa.

Alisema tangu jana kuanzia saa mbili asubuhi wanachama mbalimbali wamejitokeza kuchukua fomu hizo katika nafasi tajwa ambapo idadi kamili itafahamika mara baada ya kufungwa kwa dirisha hilo.

“CCM ina vigezo vyake ambapo tayari miongozo imetolewa na sisi hatuna haja ya kupiga tarumbeta kwa sababu tuliyoyafanya yanaonesha dhahiri tunatosha kushika tena dola na kubadili uchumi wa nchi yetu,” alisema

Kikweo.
Waandishi wa gazeti hili waliokuwa

wamepiga kambi nje ya Ofisi ya CCM Wilaya ya Handeni ambapo shughuli hiyo ilikuwa ikifanyika, walishuhudia wanachama wa chama hicho wakipishana kwa nyakati tofauti kuchukua fomu hizo.

MTANZANIA ilizungumza na mtia nia Mariam Mwanilwa ambaye amechukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Handeni Mjini.

Alisema kwa kuwa yeye ni mwanamke, sasa amejipanga kuhakikisha analeta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa kada zote huku akisema kuwa anasubiri uratibu wa chama.

“Leo sina la kusema zaidi ila wakati ukifika nitasema, lakini kikubwa nahitaji kuibariki Handeni Mji.

“Kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa hapa nalifahamu vizuri jimbo hili na ninahitaji kushirikiana na Rais Dk. John Magufuli kuendelea kutatua kero mbalimbali wanazokabiliana nazo wananchi wa hapa hasa wanawake wajawazito na watoto,” alisema Mariam.

KILIMANJARO

Idadi kubwa ya wanachama wa CCM wamejitokeza kwa siku ya jana kuomba fomu za uteuzi wa kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Katika Jimbo la Siha, wana CCM 19 wamejitokeza akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri na Ofisa Elimu Wilaya Moshi, Leornad Massawe.

Katibu wa CCM Wilaya ya Siha, Mwanaidi Mbisha alisema uchukuaji wa fomu ya ubunge na udiwani wa kata umeanza jana na hadi sasa idadi ya wanachama waliochukua imefika 19.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti mara baada ya kuchukua fomu, wanachama hao wamepongeza mfumo huo wa sasa wa uchukuaji wa fomu ambao unaijenga chama.

Massawe alisema kuwa ameamua kuchukua fomu ya kugombea akidai kwamba yeye ndiyo mtu sahihi ambaye akipitishwa na chama anaweza kukivusha.

“Uwezo ninao wa kuwa kiongozi kutokana na kwamba nimeitumikia nafasi ya ofisa elimu msingi, nimeweza kufanya vizuri,” alisema Massawe.

Kwa upande wake, Mwanri alisema kuwa suala la kuchukua fomu ni hatua za awali huku akisubiri chama kiamue ni nani mtu sahihi atakayeteuliwa kuwania ubunge kupitia CCM.

Kwa upande wa Jimbo la Moshi Vijijini, idadi ya wagombea 35 wamejitokeza kwa siku yajanaakiwamomwanahabariDeogratius Temba pamoja na mwenzake wa ITV, Idda Mushi.

Kwa upande wa Jimbo la Vunjo, idadi ya wagombea wamefika 26 hadi jana saa 10 jioni. Akizungumza jana na MTANZANIA, Katibu wa CCM Wilaya ya kichama ya Moshi Vijijini, Miriam Kaaya alisema utoaji fomu nafasi ya ubunge na udiwani bado unaendelea. Kwa upande wa Jimbo la Moshi Mjini, waliojitokeza ni pamoja na Pricus Tarimo, Ibrahimu Shayo, Alfha Kiwango, Evance

Mgase na Fraji Swai.
Jimbo la Same Mashariki, idadi ya

wagombea ubunge hadi jana alasiri imefika 21 huku kwa Jimbo la Same Magharibi ikiwa ni wanachama 23 waliojitokeza kwa siku ya jana.

Jimbo la Mwanga idadi ya wagombea ubunge waliojitokeza jana ilikuwa 31 na katika Jimbo la Rombo waliojitokeza walikuwa 35 huku uchukuaji fomu ukiendelea hadi Julai 17, mwaka huu saa 10 jioni.

MOROGORO

Jumla ya wanachama 19 wa CCM katika Jimbo la Kilosa wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge ikiwa ni siku ya kwanza tu tangu zoezi la uchukuaji fomu kupitia CCM lianze rasmi.

Mmoja wa watu waliojitokeza kuchukua fomu za kugombea katika jimbo hilo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi.

Mara baada ya kuchukua fomu hiyo alisema baada ya kulitumikia taifa kwa ujumla kupitia taaluma yake sasa ni wakati

ARUSHA

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ni miongoni mwa makada 29 wa CCM waliochukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini.

Jana kuanzia majira ya saa mbili asubuhi hadi majira ya saa nane mchana, makada 29 wa chama hicho walishachukua fomu za kuomba ridhaa hiyo.

Wengine waliochukua fomu ni pamoja na aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, Wakili Edmund Ngemela, mfanyabiashara maarufu jijini hapa, Philemon Mollel, Thomas Munisi na Noel ole Varoya.

Wengine ni mfanyabiashara Mustafa Panju, Alpha Laizer, Steven Lyamuya, Ambroce Malai, Humphrey Soka, Hillary Mollel, Anna Mwambapa, Swalehe Kiluvia, Loota Laizer na Ezra Mollel.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Gambo alisema moja ya yaliyomfanya awanie nafasi hiyo ni pamoja na kuvutiwa na kazi aliyofanya Rais Magufuli na kuwa atakuwa tayari kwa matokeo yoyote.

“Niwaahidi kwamba nitafuata taratibu na maelekezo yote ya chama na tutazingatia miongozo yote iliyotolewa na chama, hakutakuwa na mbwembwe za aina yoyote kwa sababu kazi ya kugombea ni kazi moja na kuteuliwa ni kazi nyingine.

“Tutaenda kuomba kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilaya na baada ya hapo tutasubiri hatma ya vikao mbalimbali vya chama na nitakuwa tayari kukubaliana

– PICHA: MPIGAPICHA WETU

wa kushirikiana na wananchi wa Kilosa ili kutatua changamoto zinazowakabili kutokana na uzoefu wa kiutendaji alioupata.

Alisema kuwa hakwenda jimboni humo kutafuta umaarufu bali amekwenda kuitumia taaluma na uzoefu wake kwa kushirikiana na wananchi wa eneo alikozaliwa na kukulia ili kutatua changamoto mbalimbali, hususani migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha mauaji pia kulifanya jimbo hilo kuwa eneo la kimkakati kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara.

Kaimu Katibu wa CCM, Wilaya ya Kilosa, Filbert Kapenda alisema mwamko wa uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo hilo ni mkubwa na kwamba kwa siku ya jana jumla ya wanachama 19 wamejitokeza huku Jimbo la Mikumi wakiwa wamejitokeza wanachama 20.

MWANZA

Baada ya CCM kufungua dirisha la uchukuaji wa fomu za kuwania uongozi mbalimbali tayari wagombea wameanza kujitokeza kwenye Jimbo la Nyamagana.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana baada wa kuchukua fomu za kuwania ubunge kwenye jimbo hilo, Wakili wa kujitegemea, Remigius Mainde alisema ameamua kuchukua fomu hiyo kwa sababua amejitathmini na kuona anaweza kuongoza na kuwatumikia wananchi wa rika zote.

Alisema kuwa lengo la kuchukua fomu hiyo ni kutaka kupeperusha bendera kama chama chake kitampa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo.

Kwa upande wake, John Nzwalile alisema ilani ya chama inamruhusu kuwania nafasi hiyo kwani amejitathmini kuwa anaweza kuwaongoza wananchi na kuwaletea maendeleo.

“Nimejitathmini nikaona naweza kuwaongoza wananchi ndiyo maana nikachukua fomu ya kuwania ubunge kwenye Jimbo la Nyamagana. Endapo chama kitanipa ridhaa ya kupeperusha bendera ya kuwania nafasi hii nitafanya mambo mengi ya maendeleo,” alisema Nzwalile.

Hadi jana waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwnaia ubunge Jimbo la Nyamagana ni Mainde, Robart Masunya, Daudi Kidyamali, Nzwalile, Herman Luhanya na Nelson Ibrahim.

na maamuzi yoyote ambayo yataamuliwa na chama chetu,” alisema Gambo.

SINGIDA

Waliochukua fomu kuomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge Jimbo la Iramba mkoani Singida wameahidi kumsaidia Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuleta maendeleo endelevu ya taifa.

Wakizungumza jana baada ya kuchukua fomu za kugombea ubunge katika jimbo hilo wamesema wako tayari kumsaidia Rais Magufuliendapowatapataridhaanabaraka za CCM.

Mmoja wa wagombea wa jimbo hilo, Babu Khamis Bulali alisema kuwa nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo ni kuleta changamoto za kimaendeleo kwa vitendo kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. Magufuli inavyopambana na rushwa ili kuhakikisha jamii inapata haki sawa na wale wenye kipato cha juu.

“Sisi vijana ambao tumekuwa wanachama wa chama hiki kwa muda mrefu ambao hatuna kipato cha kutosha, tulikuwa tukishindwa kujitokeza kugombea kwa sababu ya changamoto ya kipato, lakini kwa sasa tumepata fursa ya kugombea.

“Nikizungumzia rushwa siku za nyuma miradi mingi ilikuwa na usimamizi hafifu ambapo rushwa ilifubaza maendeleo ya jamii kwa ujumla,” alisema Bulali.

Kwa upande wake, Dk. Timoth Lyanga alisema kuwa atashirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo ya uchumi katika wilaya hiyo na jamii kwa ujumla.

Alisema ikiwa CCM itampa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo atasimamia kidete shughuli za kilimo cha mwaka mzima kwa mazao ya chakula na biashara.

“Nitahakikisha nashirikiana na wananchi na Serikali ya Dk. John Magufuli kuhakikisha tunatengeneza maziwa kwa ajili ya umwagiliaji kwa kutoa elimu kwa wananchi kukinga maji katika miteremko na kuyahifadhi kwa ajili ya umwagiliaji,” alisema Dk. Lyanga

Naye mgombea udiwani wa Kata ya Kiomboi, Ngoloma Omari, alisema yeye akiwa mwenyeji wa Kiomboi ambao kwa sasa ni mji mdogo, atakuwa bega kwa bega kuhakikisha unakuwa wa kisasa na wananchi wake wanapata huduma muhimu za kijamii.

PWANI

Hekaheka za wagombea kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kupitia CCM zinazidi kupamba moto na hadi sasa tayari wagombea 27 wamechukua fomu.

Fomu hizo zimeanza kutolewa jana katika ofisi za CCM Kibaha Mjini na Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Hafidh Luambano zoezi ambalo litaendelea hadi Julai 17 kwa mujibu wa mwongozo wa CCM.

Miongoni mwa waliochukua fomu hizo ni pamoja na Mohamed Mnembwe, Rashid Baghdellah, Mhandisi Happyness Mgalula na Mwenyekiti wa UVCCM Kibaha Mjini, Godlove Rwekaza.

Wengine ni Brigedia Jenerali mstaafu Yohana Mabongo, Godwin Ndossi, Frida Mushi, Kelvin Haule, Baraka Ngure, John Nyalusi, Henry Msukwa na Venance Mwakilima.

Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Luambano aliwataka wagombea kufuata utaratibu uliowekwa na chama ikiwemo kuepuka vitendo vya rushwa.

Baadhi ya wagombea waliochukua fomu hizo akiwemo Mnembwe na Happyness kwa wakati tofauti waliomba wanachama kuwaunga mkono.

HABARI HII IMEANDALIWA NA FARAJA MASINDE, NORA DAMIAN, ANDREW MSECHU NA CHRISTINA GAULUHANGA (DAR), SHEILA KATIKULA (MWANZA), SEIF TAKATAZA (SINGIDA), JANETH MUSHI (ARUSHA), SAFINA SARWATT, UPENDO MOSHA (KILIMANJARO), GUSTAPHU HAULE (PWANI) NA ELIZABETH KILINDI (NJOMBE)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles