Ramadhan Hassan -Dodoma
WIZARA ya Habari Utamaduni,Sanaa na Michezo, imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha kunakuwa na ukomo wenye tija wa wanasoka wa kigeni, ili kupata wachezaji wenye viwango bora wanaocheza ligi mbalimbali hapa nchini kama ilivyo kwa kiungo Benard Morrison na Meddie Kagere.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo jana bungeni kwa mwaka 2020-2021,Waziri wa wizara hiyo, Dk.Harrison Mwakyembe alisema licha ya uwapo wa lundo ya wachezaji wengi wa kigeni hapa nchini kwa sasa, wenye ubora ni Morrison na kipa Farouk Shikalo wanaoichezea Yanga, mshambualiaji Kagere na beki Serge Pascal Wawa wanaokipiga Simba.
Alisema kwa kuzingatia kwamba klabu kubwa nchini za Simba na Yanga vinajivunia historia ndefu ya soka iliyotukuka bila wachezaji wa nje kuwa mhimili wa timu.
“Na kwamba timu ya Taifa ya soka ya vijana (Serengeti Boys), ya wanawake ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens) na ya wanawake ya Taifa (Twiga Stars) ambazo zinafanya vizuri sana kimataifa na zinaundwa na vijana wanaotoka kwenye shule au vilabu visivyo na wachezaji wa nje,”alisema.
Alisema nchi zote zenye mafanikio makubwa katika soka duniani hazina sera ya ‘mlango wazi’ kama tuliyonayo Tanzania, ambapo kila mwanasoka bila kujali daraja analocheza ili mradi anatoka nje anaweza kucheza Ligi Kuu ya Tanzania.
Alisema wizara yake imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha kunakuwa na ukomo wenye tija wa wachezaji wa kigeni kwa michezo yote. Alisema lengo kuhakikisha kuna kuwa na umakini zaidi katika kuingiza nchini wachezaji bora tu wenye sifa stahili kama ilivyo kwa Morrison, Kagere, Shikalo na Wawa.