Veronica Romwald, Dar es Salaam
Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania umeipatia Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), msaada wa vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 186.
Akikabidhi vifaa hivyo leo Mei 15, Balozi wa Kuwait nchini Jassem Al Najem kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema msaada huo umelenga kusaidia matibabu ya watoto waliozaliwa ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi.
“Msaada huu ni sehemu ya mpango wa serikali ya Kuwait uliotengewa kiasi cha Dola 500,000 kusaidia nchi mbalimbali zenye uhitaji,” amesema.
Balozi huyo amekabidhi msaada wa miguu bandia kwa watoto wawili wenye uhitaji na kuahidi kuendelea kusaidia wanaohitaji msaada wa miguu na mikono bandia.
Balozi huyo ameomba ushirikiano zaidi na wa karibu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili azidi kusaidia jamii ya Tanzania ikiwamo kupatiwa barua rasmi ya Wizara.
Akizungumza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile ameagiza watumishi waliopo chini yake kuwasilisha barua hiyo kwa ubalozi huo ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.