26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mochi: Chakula pendwa kinachoua wengi Japan

VITAFUNWA vya Japan ni vitamu. Ni vyakula vya asili  vinavyochanganywa na rangi mbalimbali na hivyo kuvifanya kuwa maarufu duniani.

Sehemu kubwa ya tamtam za Japan ni mchanganyiko wa keki zinazoitwa mochi, matunda na jamii ya karanga.

Wajapan wanapenda vyakula na wanaupenda zaidi mchele. Hivyo si ajabu kuona sehemu kubwa ya mlo wa Japan ikiwamo mochi unatokana na mchele.

Kwa bahati mbaya, licha ya utamu wa mochi na kupendwa kwake si tu nchini Japan bali pia kote duniani hasa kwa wapenzi wa vyakula vya Kijapan, chakula hicho kinacholiwa zaidi wakati wa sherehe huwa kinaua.

Watu wawili waliwahi kufariki dunia na wengine 13 kulazwa hospitalini baada ya kukabwa na chakula hicho.

Mwaka 2016 chakula hicho hicho kama ilivyokuwa mwaka huu, kiliua watu tisa na wengine wengi kulazwa.

Ni chakula kinachotengenezwa kwa mfano wa keki zilizopikwa kutokana na mchele.

Chakula hicho kinaonekana kutokuwa na madhara yoyote, lakini kila mwaka kimekuwa kikiua watu kadhaa na hivyo kusababisha onyo kutolewa kwa umma.

 

Mochi ni chakula gani?

Ni keki nzuri zinazopikwa kutoka kwa mchele unaonata, ambao huchemshwa na kisha kupondwa na kukorogwa.

Kile kinachotokana na kupondwa kwa mchele, hufinyangwa na kisha kuokwa au kuchemshwa kupata keki zikiwa na rangi mbalimbali kama nyeupe, kijani na nyingine kutegemeana na matakwa ya mteja.

Namna gani huua?

Keki za mochi hunata, na kutokana na ukubwa wake zinahitaji kutafunwa kwa muda mrefu kabla ya kumezwa.

Kwa sababu hiyo, mtu yeyote ambaye hawezi kutafuna vyema wakiwamo watoto au wazee hujikuta wakipata ugumu wa kula na kukabwa kooni wakati wa kumeza.

Kwamba, ikiwa mtu atashindwa kuzitafuna vizuri keki hizo zinaweza kukwama kwenye koo na hata kusababisha kifo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Japan, asilimia 90 ya wale waliokimbizwa hospitalini walikuwa ni watu walio na miaka kuanzia 65 na kuendelea.

 

Nini cha kufanya ili chakula kiwe salama?

Njia nzuri ni kutafuna kwa muda mrefu na iwapo mtu hawezi kufanya hivyo, basi keki zinapaswa kukatwa vibande vidogo vidogo.

Kila mwaka, mamlaka huwaonya watu hasa wazee na watoto kula mochi zikiwa zimekatwa vibande vidogo.

Licha ya onyo hilo kutolewa, kila mwaka bado hutokea vifo vinavyosababishwa na chakula hicho.

Aidha, vifo vinatokea licha ya mwaka 2013 kuelekea mwaka mpya wa 2014, kampuni kadhaa zilijitokeza zikiuaminisha umma kwamba zimekuja na siri inayoweza kuepusha hatari za kiafya zinazowakabili zaidi makumi kwa mamilioni ya wazee nchini humo.

Kumbuka Japan ni taifa lenye wazee wengi duniani kutokana na uwapo wa wastani mkubwa wa umri wa kuishi nchini humo.

Mkakati wa kampuni hizo ulihusisha kutengeneza mochi salama zilizopunguzwa kiwango cha mnato wakati zikiendelea kuwa na ladha ile ile ya wanga.

Awali mwaka 2010, Tume ya Usalama wa Chakula Japan, iliiweka mochi miongoni mwa vyakula vinavyoongoza kwa kusakama kooni na ambavyo waathirika wake wakuu kwa zaidi ya asilimia 80 huwa  ni wazee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles