25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MO AMTIMUA OMOG SIMBA KISAYANSI


Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Simba kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam, mfanyabiashara maarufu nchini na mwanachama wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, amemwomba kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, ajiuzulu nafasi hiyo.

Simba ilichapwa penalti 4-3 na Green Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) hivyo kuondoshwa katika kinyang’anyiro cha Kombe la Shirikisho la Azam, mchezo uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kabla ya kufikia hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti, timu hizo zilikamilisha dakika 90 zikiwa zimefungana bao 1-1 na hata zilipoongeza nyingine 30 matokeo hayakubadilika.

Lakini kipigo ilichokipata kimeonekana kubadilisha hali ya hewa, ambapo jana Mo aliamua kumfungukia Omog akimtaka aachie ngazi.

Tajiri huyo kwa sasa ndiye mwekezaji mkuu katika klabu ya Simba akimiliki hisa asilimia 49, huku nyingine 51 zikibaki kwa wanachama, baada ya kushinda zabuni ya uwekezaji.

Kabla ya Mo kushinda zabuni hiyo, ulifanyika mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji katika klabu ya Simba kutoka ule wa kadi za uanachama hadi kuwa wa hisa, ambapo ulichukua zaidi ya mwaka mmoja kukamilika kwake.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, Mo aliandika maneno yanayoonyesha kutofurahishwa kwake na matokeo iliyoyapata Simba katika mchezo dhidi ya Green Warriors.

Mo aliandika hivi: “Kwa kuwa bado sina mamlaka ya maamuzi kwenye klabu ya Simba, kama mwanachama na mshabiki wa Simba, namwomba Omog kwa heshima na taadhima ajiuzulu.”

Shinikizo dhidi ya Omog halikuanzia kwa Mo kwani lilitanguliwa na lile la Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara, ambaye naye kupitia akaunti yake ya Instagram aliandika maneno yaliyoonyesha amemchoka kocha huyo Mcameroon.

Andiko hilo la Manara liliambatana na picha ya kikosi cha Simba.

“Shame (aibu), fedheha, haivumiliki, tumewaumiza fans (mashabiki) wetu zaidi ya milioni 20, nimeumia kuliko siku zote toka nimeanza kazi Simba.

“Wanachama na washabiki wetu tumewasikia na tumewaelewa, hivi karibuni mtasikia.

“Maamuzi sahihi na magumu hufanywa wakati mwafaka,” aliandika Manara.

Omog alipotafutwa ili kuzungumzia ushauri wa Mo hakuweza kupatikana mpaka gazeti hili linaenda mtamboni.

Oktoba 19 mwaka huu, Simba pia ilimtimua aliyekuwa msaidizi wa Omog, kocha Mganda, Jackson Mayanja, ambapo nafasi yake ilizibwa na Mrundi, Masoud Djuma.

Wekundu hao walitwaa ubingwa huo msimu uliopita baada ya kuichapa Mbao FC mabao 2-1 na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Mei mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na klabu ya Simba jioni kupitia kwa Manara, ilithibitisha kuachana rasmi na kocha huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles