HARARE, ZIMBABWE
TUME ya Uchaguzi nchini Zimbabwe (ZEC) imemtangaza Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii, lakini mgombea wa muungano wa Upinzani, MDC Alliance, Nelson Chamisa amekataa kutambua ushindi huo na kubainisha kuwa watafungua kesi Mahakamani kupinga matokeo hayo.
Kwa mujibu wa ZEC, Emmerson Mnangagwa, mshirika wa zamani wa Robert Mugabe, ameshinda baada ya kujipatia asilimia 50.8 ya kura dhidi ya Nelson Chamisa wa chama cha MDC, Â aliyepata asilimia 44.3 ya kura.
Akitangaza matokeo hayo mbele ya vyombo vya habari nchini humo, Mwenyekiti wa ZEC, Priscila Chigumba, alisema kura alizopata mgombea wa chama cha ZANU-PF, Emerson Mnangagwa ni zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa za nafasi ya urais.
Ili kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais, mgombea anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura. Mgombea wa chama cha upinzani MDC alifanya vizuri katika maeneo ya mjini, wakati Mnangagwa alipata kura nyingi vijijini.
Uchaguzi huo umefanyika kujaribu kurejesha demokrasia nchini humo, kufuatia miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe.
Kwa upande wake, chama cha upinzani MDC kimesema kitapinga matokeo hayo mahakamani, ambapo ameituhumu ZEC kutangaza matokeo yaliyochakachuliwa.
Mgombea wa upinzani, Nelson Chamisa, amewalaumu Polisi kuvamia makao makuu ya chama hicho na kuzuia kompyuta, huku wakiwa hawana kibali cha kufanya upekuzi. Katika upekuzi huo, watu 16 walitiwa mbaroni, kufuatia tukio hilo.
Walati hayo yanajiri nchini humo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametoa mwito kwa Wazimbabwe kukubali kuchaguliwa kwa Mnangagwa kuwa rais wa nchi hiyo na iwapo wana pingamizi lolote wafuate taratibu za kisheria.
Tangu Zimbabwe ijipatie uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1980, taifa hilo limekuwa na marais wawili tu, ikiwa ni pamoja na Mugabe aliyeongoza kwa mkono wa chuma katika kipindi cha miaka 37 na mshirika wake wa zamani, Emerson Mnangagwa, aliyeteuliwa kushika madaraka hayo baada ya Mugabe kujiuzulu Novemba mwaka jana, kufuatia shinikizo la jeshi.
Kucheleweshwa kutangazwa matokeo hayo kulisababisha maandamano na vurugu, hali iliyosababisha wanajeshi kuingilia kati kuzuia ghasia zozote.
Watu 6 wameripotiwa kufariki dunia baada ya wanajeshi hao kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji wa chama cha upinzani waliokuwa wakidai kuna udanganyifu katika uchaguzi huo.
Wanajeshi pamoja na polisi waliweka ulinzi mkali katika mitaa mbalimbali ya jiji la Harare, wakiwaaamuru watembea kwa miguu na wafanyabiashara kuondoka maeneo hayo, huku chama cha upinzani cha MDC kikisisitiza kuwa chama tawala ZANU-PF kilimefanya udanganyifu.
Idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi ilikuwa ni asilimia 80, karibu katika majimbo yote kumi ya nchi hiyo.
Kabla ya vurugu za baada ya uchaguzi, waangalizi wa Umoja wa Ulaya katika taarifa yao ya pamoja walisema hakukuwa na mazingira sawa kwa vyama vyote wakati wa mchakato wa uchaguzi huo pamoja na kulaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia wasio na silaha.
Kiongozi wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ambaye awali aliwataka wapiga kura kukikataa chama tawala ZANU-PF, alipiga kura pamoja na mkewe mjini Harare.
Rais mteule Mnangagwa sasa atalazimika kufufua uchumi wa taifa hilo ulioporompoka wakati wa Mugabe na kutafuta suluhisho la ukosefu wa ajira, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mfumuko wa bei.