29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

NINI UWOYA, MOBETTO … UMEMWONA SANCHOKA?

NA CHRISTOPHER MSEKENA


WIKI mbili zilizopita mastaa wenye mvuto katika anga la burudani za Bongo, Irene Uwoya na Hamisa Mobetto, walitiwa nguvuni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kosa la kukiuka kanuni za maudhui zinazomtaka msanii kuhakiki maudhui anayochapisha mtandaoni kama yana usalama na hayamuumizi mtu.

Wawili hao walifikishwa katika Kamati ya Maudhui TCRA na kutoa maelezo juu ya picha zisizo na maadili walizozichapisha katika kurasa zao za Instagram na kamati ikabaini kuwa, Uwoya na Mobetto wamekiuka kanuni hizo, hivyo kupewa onyo na kutakiwa kuiomba radhi jamii.

Kilichowakuta Uwoya na Mobetto kiliwahi kuwakuta Diamond Platnumz na Nandy, ambao nao waliwahi kuitwa na Kamati ya Maudhui TCRA kutoa maelezo ya picha na video walizozichapisha mtandaoni.

Unaweza ukajiuliza, katika sekta ya burudani Bongo ni mastaa hao pekee ndio wanachapisha picha zisizo na maadili? Swaggaz tunakusogezea orodha ya warembo ambao ni pasua kichwa huko mtandaoni kwa kuchapisha matukio na picha zenye ukakasi zaidi ya zile za Uwoya na Mobetto.

Sanchoka

Jane Rimoy (Sanchoka), ambaye ni mrembo maarufu zaidi kwa umbo lake la kibantu anayetambaa katika mtandao wa Instagram akitumia jina la  @Sanchiword.

Ana wafuasi zaidi ya 600,000 wanaozitazama picha zake tata anazochapisha mtandaoni akiwa katika mapozi tofauti yenye ukakasi zaidi ya zile zilizomtia matatani Irene Uwoya.

Sanchoka ni binti wa Tanzania anayeishi zaidi Afrika Kusini, akipiga mitikasi yake na kampuni mbalimbali zinazotumia umbo lake kunadi bidhaa zao akiwa kama balozi.

Tuerny

Anaitwa Lisa Dedee, maarufu katika mtandao wa Instagram kama Tuerny, wengine wanamwita pacha wa Wema Sepetu, kutokana na midomo yake kufanana na mrembo huyo.

Mwaka jana alionekana kuwa karibu na staa wa Nigeria, Davido, kiasi cha kuibua tetesi za wawili hao kuwa ni wapenzi, ila haikuwa hivyo, baada ya yeye mwenyewe kuthibitisha kuwa Davido ni mshkaji wake tu.

Mpaka sasa Tuerny, ambaye amejipambanua kama msanii wa ‘make up’, ana wafuasi zaidi ya 200,000 wanaotembelea ukurasa wake wa Instagram kujionea picha tata ambazo mara nyingi amekuwa akizichapisha akiwa amevaa mavazi yanayoacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake zaidi ya zile ambazo Uwoya na Mobetto walizichapisha.

Sister Fey

Faidha Omary, maarufu kama Sister Fey na katika mtandao wa instagram anatumia jina la @fey_tanzania, ambaye bado haijafahamika sanaa ipi anaifanya kati ya muziki, filamu na nyinginezo, licha ya kuwa na wafuasi zaidi ya 100,000 wanaomfuata.

Wiki tatu mfululizo ameuteka mtandao huo kwa matukio yake ya kimapenzi anayoyafanya na kijana anayetambulika kama Hollystar.

Si kosa kwa mwanamke kutoka kimapenzi na kijana mdogo kama ambavyo Fey anafanya (kwa mujibu wake), ila kunapokuwa na matukio yanayovunja kanuni ya maudhui ya kimtandao hapo panaweza kuwa na tatizo.

Video za kimahaba ambazo Fey na ‘mpenzi’ wake wamekuwa wakichapisha katika Instagram zimekuwa zikilalamikiwa na asilimia kubwa ya mashabiki, ambao hutoa maoni yao chini ya picha au video hizo, ni wachache wanaompongeza.

Lynn

Anaitwa Irene, maarufu katika mtandao wa Instagram kama @officiallyyn ambaye ni video vixen aliyeanza kujipatia ustaa baada ya kunogesha video ya msanii wa WCB, Rayvanny, inayoitwa Kwetu.

Mpaka sasa ana wafuasi zaidi ya 300,000 katika mtandao huo, ambao amekuwa akichapisha picha mchanganyiko. Zipo zile zenye heshima na zile ambazo zinaacha maungo yake wazi.

Wapo wengi, hawa ni baadhi yao ambao wamekuwa wakichapisha picha na kufanya matukio yenye ukakasi katika kurasa zao za Instagram, zaidi ya Hamisa Mobetto na Irene Uwoya, ambao walitambuliwa na TCRA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,335FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles