HARARE, ZIMBABWE
RAIS wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amewakaribisha waangalizi wa kimataifa wakiwamo wa Umoja wa Mataifa wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.
Rais Mnangagwa ametoa ukaribisho huo alipofanya mahojiano na gazeti la Financial Times la Uingereza, akiachana na msimamo wa mtangulizi wake Robert Mugabe aliyewatenga waangalizi hao.
Mnangagwa safari hii ametumia mtazamo wa kidiplomasia zaidi tangu alipochukua madaraka Novemba mwaka jana, baada ya kuondolewa kwa Mugabe aliyekuwa madarakani miaka 37.
Aidha kauli yake imekuja siku chache tu baada ya kutangaza kuwa chaguzi zitafanyika katika kipindi cha miezi minne hadi mitano ijayo.
“Tunataka uchaguzi huru, wazi na wa haki. Napenda Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya waje kushuhudia na iwapo Jumuiya ya Madola itaomba kuja, nipo tayari kuzingatia ombi lao”, alisema Mnangagwa.
Zimbabwe ilizuia waangalizi wa kimataifa wakati wa kipindi cha utawala wa Mugabe, ambao unadaiwa kuendesha chaguzi zilizojaa udanganyifu na ukandamizwaji mkubwa wa upinzani.
Mnangagwa, ambaye alikuwa miongoni mwa washirika wa karibu zaidi wa Mugabe ndani ya chama cha ZANU-PF, amekuwa akituhumiwa kuwa sehemu muhimu ya ukandamizaji huo.
Lakini tangu alipochukua madaraka ya urais ameendelea kujisogeza karibu na jumuiya za kimataifa ikiwamo mtawala wake wa zamani wa ukoloni, Uingereza.
Uingereza ilikuwa mkosoaji mkubwa wa Mugabe, ingawa Mnangagwa alitabiri kuimarika kwa uhusiano baada ya Taifa hilo kuamua kuondoka Umoja wa Ulaya mwaka ujao.
Aidha alisema yuko tayari kuomba kurejea Jumuiya ya Madola, ambayo inahusisha mataifa yaliyowahi kutawaliwa na Uingereza.